Sunday, March 27, 2011

Uhalifu na mfumo wa kijamii-uchumi

Tuanze na mchapo. Huko Uganda walimu wa shule za msingi siku moja walijikuta wanafanya mitihani ile ile waliyokuwa wakiwapa wanafunzi wao. Wengi wao walifeli. Serikali ikawafukuza kazi.

Huko huko Uganda mamia ya askari polisi wanaodaiwa awali walikuwa walevi hivi sasa wanapigishwa kwata la nguvu. Atakayeshindwa mazoezi hayo, yakiwemo, kukimbia, kubeba mizigo mizito na kadhalika atakuwa kajifukuzisha kazi.

Na huko Uganda tena, hivi sasa bila angalau digrii moja sahau kuwa mwandishi wa habari maisha.

Wenzetu wamecharuka. Wanataka kama mtu ameajiriwa kwa kazi fulani basi kweli si tu aagizwe ifanyike lakini aonekane akiifanya kazi hiyo.
Nchi haiwezi kuwa na maendeleo ya kweli, Waganda wanaamini, kama una wababaishaji sehemu za kazi muhimu na sio wachapa kazi.

Katika mtiririko wa haya yote Waganda wanayoyafanya inaelekea wana mkakati fulani wa kuijenga jamii yao iwe imara kiuchumi na kijamii.

Kwanini ujambazi unakuwa tishio?
Tuache utani. Ujambazi sasa ni tishio kwa biashara na makampuni nchini. Kila mtunza-fedha au mbebaji fedha wa kampuni au taasisi nyingine daima yuko katika hofu ya kutolewa roho.

Hvi leo jamaa hawa wanaweza wakaibukia sehemu yoyote wakafanya vitu vyao na wakaondoka na asitokee polisi yeyote kwa kitambo kiasi. Katika hali kama hii kila mtu anajiona ni yeye na lwake. Wakati kila raia ameanza kupoteza imani kabisa na jeshi lao la polisi.

Kwa kifupi watu wamekata tamaa na wanaamini kuwa unaweza kushambuliwa wakati wowote na usipate msaada. Na hii ndio sababu ya ujambazi kuwa sasa ni tishio la kitaifa linalochipukia.

Hata hivyo, wanasiasa bado wamekaa kimya na hakuna anayezungumzia jambo hili kwa uzito unaotakiwa. Pengine wakiamini kuwa unaweza kulifumbia macho nalo likapita. Lakini hili kwa nionavyo mimi sio jambo la kupita. Ni kitu tutakachokuwa nacho siku zote kama vile tutakavyokuwa na maskini siku zote.

Vita vinaweza kuliyumbisha taifa. Ujambazi ukikithiri hulisambaratisha taifa. Na ukitaka kuiona mifano nenda Somalia.

Kama ndivyo basi huu ni wakati wa viongozi nchini kujiuliza maswali mengi kadri iwezekanavyo ili kupata majibu sahihi na mikakati ya kuitumia ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili.

Maswali ya kujiuliza
Ingawa mimi sio bingwa wa masuala ya sayansi ya jamii, hata hivyo, nina maswali kadhaa ya kuuliza ambayo natarajia yakipata majibu yatatupa mwanga juu ya tatizo linalotukabili.

Ni kwa kiasi gani mpito toka ujamaa kuingia siasa isiyo na jina (Ubepari usiotajwa) hapa nchini unachangia kuongezeka kwa wimbi la ujambazi wa kutumia silaha.

Wakati ule tunavaa Chou-en-lai inaelekea wote tulijiona kuwa ni sawa. Kwa malezi ya Baba wa Taifa kila mtoto alijiona hana tofauti na mtoto mwenzake. Na hili alilifanya kuanzia nyumbani kwake mwenyewe.

Hivi leo mtoto wa muuza samaki feri ambaye kuambulia elfu moja ni kazi akiwa rafiki wa mtoto wa mwanasiasa au meneja ambaye baba yake humpa laki moja atumie kwa siku! Ni binadamu gani ataacha kuwa na maswali ya kujiuliza na yeye afanye nini awe kama huyu wa pili? Hebu fikiri!

Achilia mbali watoto; leo wazazi wanashindana kwa wingi wa majumba, magari, nguo na kila aina ya vikorokoro. Wazazi wengine wanona ilhali wengine hawana uwezo na wanabaki kumezea mate na matumbo kuwanguruma. Watoto wao siku ya siku wanapofanya vitu vyao dhidi ya hao ‘wanaoringa’ mzazi atakataa nyumba mpya anayopewa? Mark II na dereva ikija nyumbani na kuambiwa ni yake aitumie jinsi anavyotaka? Mzazi atasema nini? Atamlaumu mwanae? Amelogwa? Achekwe?

Katika hali tuliyo nayo sasa baadhi ya wazazi wanaowaona watoto wao ‘wezi’ kuwa ni kina Robbin Hood wa miaka yetu. Kama humjui jamaa huyu basi nikuelezee kwa kifupi. Huyu alikuwa ni jambazi maarufu wa Kiingereza ambaye alikuwa anawaibia matajiri na kuwapa maskini. Unaona hiyo?

Fursa finyu
Katika miji yetu mbalimbali kumezuka ubia usio mtakatifu kati ya wanasiasa-wafanyabiashara na watumishi wa serikali kuwapora vijana mabanda ya biashara; viwanja vya michezo; tenda; vibali na kila aina ya fursa ambayo ingelimuwezesha kijana kujiendeshea maisha yake na pengine kutajirika bila kutumia njia haramu. Sasa tujiulize kama mtu ananyimwa fursa halali za kuukata afanye nini. Ashukuru. Atoe Allhamdullilahi kisha asahau?

Elimu bila kazi
Mamia ya vijana wanaomaliza shule ndani na nje ya nchi hivi sasa hawapati kazi. Ni nini kitakachotokea hapa. Tumewahi kujiuliza swali hili? Biblia inatuambia: ‘mikono isiyo na kazi, shetani ataitafutia kazi bila wasiwasi wowote!’

Watu waliosoma hawawezi kuwa sawa na vibaka. Hawa ni watu wenye akili eti. Wengine wamesomea udaktari wa mifugo; wengine wahandisi; wengine wanasayansi na kadhalika. Na ole wako wakikutana watu zaidi ya wawili kama hawa mambo wanayoweza kuyafanya ni ya ajabu. Tatizo ni pale ambapo wanachokifanya ni biashara ya uvunjaji sheria. Nani ataona ndani?

Sheria zinazopendelea
Vijana wa Kitanzania sio vipofu, sio viziwi. Wanaona kila siku, wanasikia kila kitu. Na aghalabu wanajua kuwa kuna seti mbili za sheria. Moja ni ile ya walalahoi, na nyingine ni ile ya vigogo na vizito. Mlalahoi ama ni kuvunjiwa vyombo vyake na kupoteza mtaji wake wa kimaskini au ni kulipa faini au ni kwenda jela. Sheria hiyo hiyo kwa upande wa vizito ni kuhakikisha mali yao inalindwa kwa jino na ukucha wa polisi wetu wenyewe; kutokulipa faini na kutokwenda jela hata wakifanya kosa gani.

Katika hali kama hii inafaa tuwaulize wanasayansi-jamii je watu na hasa vijana wenye wingi wa jazba na pupa ya maisha watalichulia hili suala namna gani. Ni vyema kufuata sheria na kunyanyasika hata pale wewe unapostahili kuwa ndiye mdhulumiwa au mtu aliyeonewa, au ni kuvunja sheria na kuhakikisha vyombo vya sheria havikubambi hata siku moja? Na wakikuzingira basi uchukue njia ya Mkwawa?

Hili linaendana na haki kununuliwa. Hivi sasa kwa sababu moja au nyingine mtu mwenye fedha au mwanasiasa anaweza akakukosea. Lakini badala ya wewe uliyekosewa kulipwa fidia ukajikuta wewe ndiye unayedaiwa kama sio kwenda lupango kabisa.

Katika kijiji ambacho sitaki kukitaja jina visa kama hivi vimetokea. Na watu wasiokuwa na hatia, na hasa vijana, labda kwa sababu ya kugombea mwanamke na kumshinda tajiri anajishtukia yuko ndani na kosa halijui. Hili linafanyika vijijini, ninaamini, karibu vyote Tanzania na sio hicho kimoja tu nilichotolea mfano wake.

Njaa na umaskini
Hapana haja ya kusema mengi kuhusu hili. Maana ni wazi kuwa kuna njaa na umaskini wa kutisha katika jeshi letu la polisi. Hatusemi wakimwagiwa fedha basi ujambazi utakwisha. La, hasha. Tuwaachie wanasayansi-jamii watupe majibu ya swali hili: je, mishahara midogo na umaskini wa polisi unachangia kwa kiasi gani matatizo ya usalama nchini? Na kwa kiasi gani hili linachangia haki ya mtu kuuzwa au kununuliwa?

Uharamia na ushindani
Pengine ni muhimu kwa wanasayansi-jamii kuuliza pia kama ushindani ambao ni matokeo ya soko huru nchini unaweza kusababisha uharamia wa kibiashara? Je, mfanyabiashara fulani anaweza kukodi majambazi ili wapore kutoka kwa mshindani wake na hivyo kumkomesha mwenzie? Au pale biashara au kampuni fulani zinapopewa upendeleo na mamlaka na wengine kutaka kujibu mapigo?

Je, watu wanaofukuzwa kazi ovyo katika makampuni na taasisi siku hizi wanaweza kutumbukiwa na nyongo na kuamua kula sahani moja na majambazi ili kuwakomesha waajiri wao?

Kisaikolojia hasa ni kitu gani kinachomfanya mtu kudiriki kutoa roho ya mwenzie na pengine mtu anayemjua kwa sababu ya shilingi millioni 10, 30 au hata 100?

Elimu, uwezo na vifaa vya polisi
Aidha katika hili ni muhimu kujiuliza kama elimu waliyo nayo polisi waliofaa kulinda usalama wakati wa siasa ya ujamaa kama inatosha kulinda usalama katika enzi za ubepari na ushindani?

Wananchi wengi wanaamini kuwa polisi wetu wana elimu duni na hawawezi kabisa kukabiliana na hali inayojitokeza sasa. Hawa, inadaiwa, ni watu waliofundishwa kutumia zaidi nguvu na sio akili. Kadhalika mbele ya mitandao kama ile ya simu za mikononi na kompyuta ni rahisi polisi wetu ‘kuchengenywa’ na wasijue chochote kinachoendelea. Maana ni polisi wangapi wenye simu za mkononi au wanaojua kutumia kompyuta?

Mfumo unaofaa
Ni dhahiri ujamaa ulikuwa una kasoro nyingi. Kadhalika ndivyo ilivyo kwa ubepari. Wenzetu katika nchi za Scandinavia walitambua hili miaka kadhaa iliyopita. Wao hawafuati ujamaa moja kwa moja, wala hawafuati ubepari kichwa na miguu. Wamebuni siasa inayoitwa ujamaa-wa-kidemokrasia.

Mfumo unaomruhusu kila mtu kutajirika kwa kadri ya uwezo wake, lakini wakati huo huo hauruhusu mtu kufa njaa au kukosa kabisa eti ili fulani tu atajirike. Huu ni wakati muafaka wa vyama vya siasa kupitia siasa za nchi hizo na kuona ni mazuri gani tunayoweza kuyaiga kama sehemu ya mapambano yetu ya muda mrefu dhidi ya uvunjaji sheria nchini mwetu.

Bila shaka majibu yoyote yatakayopatikana hapa yatalazimu kuibadili katiba ya nchi na vyama vyetu. Maana badala ya maneno ujamaa na kujitegemea lazima pawe na maneno yasemayo kuwa nchi yetu ni nchi inayofuata ujamaa-wa-kidemokrasia.(Ujaki) Kwani mfumo huu utawapiga jeki wasionacho! Aidha mfumo huu si mgeni hapa nchini; ulikuwepo Zanzibar enzi za marehemu Karume. Wakati Zanzibar ilipokuwa haina wizi, umalaya, madawa ya kulevya na uhalifu mwingine uliopo hivi sasa. Mwenzetu alijua anachokifanya, je sisi tunajua tunachokifanya?

No comments:

Post a Comment