Katika siku za hivi karibuni nimekuwa nikipata barua-pepe nyingi za watu wa nje wanaotaka kuja kutalii, kuwekeza au kufanya biashara na Tanzania.
Baadhi ya watu hao wala sio wageni ni Watanzania waliokaa nje muda mrefu au ambao wamechukua uraia wa nchi nyingine lakini hivi sasa wanataka kurejea baada ya kuvutiwa na mageuzi ya uchumi yanayoendelea nchini.
Baadhi ya maswali yao yamekuwa magumu kwangu kujibu na nikayaelekeza au nikawaelekeza wahusika kwa taasisi kama vile Wizara ya Mambo ya Nje, TCCIA, taasisi zinazohusika na utalii, Tanzania Investment Center na kadhalika.
Majibu ambayo watu waliowasiliana nami wananipa ni kuwa ama e-mail za wahusika hazifanyi kazi, nyingine zina virusi, na kwa kila hali hakuna anayewajibu wala kushughulikia shida zao.
Kwa mfano, kuna makampuni ya utalii nchini Venezuela na Brazil yaliyokuwa na watu wanaotaka kuja kutalii Tanzania. Hadi leo wanahaha kupata visa za kuja Tanzania.
Ubalozi wa karibu (naomba kusahihishwa) nadhani ni Washington lakini japo ubalozi huo una web-site na email wakala hao wanasema hakuna jibu walilolipata.
Anwani ya websaiti ya ubalozi huo ni http://www.tanzaniaembassy-us.org na kama sikosei email yao ni: balozi@tanzaniaembassy-us.org Wabrazili na Wavenezuela wanasema ni anwani bubu.
Katika websaiti hiyo pamoja na mambo mengine kuna nembo ya taifa, bendera inayopepea lakini inaelekea anwani ya barua pepe yao haipepei na kuna twiga anayekimbia na maneno -TANZANIA ON THE GO- lakini inaelekea kwa hakika sivyo bado Tanzania imelala katika kutumia mtandao ili kukuza uchumi wake kutokana na biashara nyingi ambazo hivi leo zinafanyika kwa kutumia email na internet.
Kuna bwana yuko Uarabuni anataka kuanza biashara ya kununua na kuuza mifugo na Tanzania. Inaelekea huyu kazaliwa hapa maana anazungumza Kiswahili fasaha. Nimejaribu kumuelekeza kwa wahusika lakini anasema hapati majibu anaomba mimi nimsaidie. Lakini ninadhani kuna walioajiriwa kufanya kazi hiyo au sio-pengine Wizara inayohusika inaweza kumsaidia kwa kuwasiliana nami.
Leo ninapoandika makala hii nina barua pepe zaidi ya kumi. Baadhi yake zinataka kununua korosho kutoka Tanzania; Huyu mwingine anataka kujua kama Bombay Bazar na Manek Traders ni kampuni halali na wanaweza kufanya biashara nazo; kuna kijana wa Kimarekani anasema mkimbiaji mbio aliyewika miaka kama 20 iliyopita hivi ni baba yake na anataka kuwasiliana naye (sijui kama ni kweli au uongo), hata hivyo mwanariadha aliyesoma Marekani na anajua ana mtoto huko awasiliane nami nimuunganishe na mwanae; kuna wanaotaka madini; kuna wanaotaka kuuza nguo ili mradi kuna fursa mbalimbali kwa Watanzania na taifa kuongeza kipato chake.
Labda hapa tuwaambie Watanzania wanaotaka biashara hizo au ambao wametajwa hapo juu wawasiliane nami kupitia anwani yangu ya sammy.makilla@columnist.com niwaunganishe na wahusika bila malipo yoyote.
Kwanini email & internet hazitumiki
Hali hii, hata hivyo, imenifanya nijiulize hivi kweli serikali, taasisi mbalimbali na makampuni yaliyoko kwenye mtandao yanautumia kikamilifu ili kuikwamua nchi kutokana na umaskini?
Kuna wizara ambazo katika miaka hii ya sayansi na teknolojia zinatakiwa kuwa na websaiti na watu wanaofuatilia email kwa saa ishirini na nne.
Tanzania haiko tena kwenye miaka ya kulala masaa 16 kila siku jamani. Hivi kweli tutaendelea kama zaidi ya asilimia 60 ya maisha yetu hapa duniani ni ya usingizini au kwenye anasa nyingine?
Kwa mfano websaiti ya Wizara ya Nje ya Afrika ya Kusini inayoitwa Department of Foreign Affairs inayopatikana kwenye http://www.dfa.gov.za Inafanya kazi masaa ishirini na nne.
Ukituma email wakati wowote unajibiwa katika muda usiozidi saa moja. Mnaona hayo na sisi bado tumelala.
Hao wawekezaji watatoka wapi kama wakituma email hakuna anayewajibu? Taasisi zinazohusika na biashara na huduma mbalimbali na hasa kama vile bodi ya utalii, makampuni ya utalii, mahoteli, vyombo vya usafiri na kadhalika navyo kwa namna moja au nyingine lazima ziwe na mtandao hai na unaofanya kazi ikiwezekana kwa saa ishirini na nne.
Dunia ilivyo ni kuwa Tanzania ikiwa ni usiku Marekani na Japani ni asubuhi au mchana.
Bado hatujaamka na kujua ukweli huu? Tusifikiri sisi tunapolala basi watu wote duniani wamelala. Wengine ndio kwanza wanakunywa chai, wengine wamo kwenye lanchi na wengine ndio kazi zimeanza tena.
Makala hii inakusudia kutoa wito kwa Watanzania kuamka na kuanza kuchangamkia matumizi ya email na internet kwa ukamilifu kwa sababu hii sasa ndio njia muhimu ya mawasiliano ya kibiashara pengine kuliko njia nyingine yoyote duniani.
Haifai kuwa na websaiti za mapambo. Websaiti lazima ziwe ni viungo hai vinavyoiunganisha nchi na watu wengine duniani ili biashara au shughuli fulani ifanyike kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Ni tatizo gani linakwamisha…
Wanaojua ni nini kinachokwamisha kwa mfano wizara muhimu kuwa na websaiti na webmasta na wasaidizi wake wanaofanya kazi kwa kupokezana kwa masaa ishirini na nne kila siku ni wizara zinazohusika.
Sababu zinaweza kuwa za kifedha, nguvu kazi, gharama za kuweka kiunganisho cha internet na kadhalika.
Lakini kama haya ni matatizo kwanini tusiyaongelee? Kwanini serikali isivutwe sikio na kuambiwa kuwa kuna tatizo kama hili? Lakini matatizo yote haya kwa upande wangu ninaona ni matatizo ya mficha maradhi tu.
Tatizo la fedha kwa mfano linaweza likawa la urongo na kweli. Maana nina hakika katika nchi nyingi kampuni zinazotoa huduma za mtandao ziko tayari kusaidia serikali na taasisi zote zile zinazotaka kukuza uchumi wa nchi tena wakati mwingine bure. Lakini watu hao wasipofuatwa wakaelezwa shida hii hakuna atakayejua kuwa tatizo ndio hilo la kifedha.
Kuhusu utaalamu hapa serikali lazima ielezwe ukweli kuwa inapaswa kutoa mchango mkubwa ili Tanzania iwe na wataalamu wa kompyuta na shughuli zinazoendana na teknolojia hii.
Na uzuri wa kuwekeza katika sekta hii ni kuwa wataalam wa mambo haya wana soko kubwa karibu kila sehemu duniani.
Nina hakika nchi ikiwa na nia tunaweza kutoa wataalamu wa kujitosheleza na ziada ambao watatuingizia fedha za kigeni kwa kwenda kufanya kazi nchi za nje. Hao wanaobaki nyumbani watatusaidia kuifanya Tanzania kuwa namba wani kikweli kweli katika teknolojia hii muhimu katika enzi za utandawazi na ushindani mkubwa wa kiuchumi.
Serikali inastahili pongezi kwa kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya teknolojia hii kwa bei nafuu sana ukilinganisha na sehemu nyingine Afrika. Na hili ni muhimu liendelee ili kompyuta Tanzania zifike hadi vijijini. Kama wananchi wa Ruvuma vijijini wanaweza kufanya biashara na nchi za nje kupitia mtandao, kwanini vijiji vingine navyo visifanye hivyo?
Gharama za kuunganisha
Baadhi ya wizara na taasisi mbalimbali ninaamini zilianza vibaya kwa kutumia internet ya kupitia kwenye laini za simu.
Njia hii ni ghali sana. Njia bora zaidi ni kutumia kitu kinachoitwa ‘wireless’ au kuunganishwa na mtoa huduma bila haja ya kuwepo kwa simu.
Kwa hakika gharama za mwanzo za uunganishaji ni kubwa lakini baada ya hapo internet inakuwa kama ni bure. Wizara na taasisi zote zinazostahili kuwa na mtandao lazima zitumie wireless na sio vinginevyo.
Gharama hivi sasa zinafikia milioni tatu hivi kuunganishwa. Kwanini serikali na taasisi zinazohusika zisikae chini na kuona ni jinsi gani gharama hizi zinaweza kupunguzwa. Nina hakika gharama zikifika milioni moja sio tu makampuni bali hata watu binafsi wataweza kuwa na huduma hii muhimu katika miaka ya hivi sasa.
Kingine kilichobaki na ambacho nacho kina umuhimu sawa ni hili la kuona kuwa tunakuwa na wataalamu na mafundi wengi kadri iwezekanavyo katika nyanja za kompyuta na internet.
Na hapa serikali na wabia wengine washirikiane ili Tanzania iwe ni mfano wa kuigwa Afrika baada ya Afrika Kusini katika mambo ya internet na matumizi ya kompyuta kwa ujumla.
Sunday, March 27, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment