Saturday, October 15, 2011

Mola hawasaidii

Maziwa, mito bahari na chemchemi lukuki,
Nchi iliyo tajiri, lakini haizinduki,
Akili zakifakiri, ndizo zinazotamalaki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Ardhi yake bahari, nini hakistawiki?
Siasa za kikafiri, dhuluma zinahakiki,
Mkulima hanawiri, anyonywa mpaka haki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Wazee na matajiri, nchi wanaimiliki,
Ni heri nusu ya shari, kwao hilo hawaafiki,
Haijai bilauri, njaa yao haishibiki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Kiu yao ya tanuri, katu haimaliziki,
Ukubwa wao jeuri, na kazi haifanyiki,
Watakacho ufahari, wala si mikiki mikiki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Madini yamedhihiri, raia hanufaiki,
Akili zatahayari, uongozi kuafiki,
Ni nani mwenye habari, ambazo haziandikiki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Na misitu kwa ekari, mbao bei haishikiki,
Makazi yatuadhiri, watu hawathaminiki,
Wakubwa waona fahari, nje kwenda kuhakiki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Ndani hamna safari, ila zile za falaki,
Zanyong'onyea suduri, uhai hautamaniki,
Na walio na kiburi, hili halikubaliki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Viwanda tumeghairi, tunawapa mamluki,
Uzalishaji johari, bilavyo hatujengeki,
Viongozi washairi, na tungo hazighaniki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Kuwaomba matajiri, hulka siiafiki,
Twajidhalilisha ari, hamsini hatuamki,
Tuutazame urari, tutumie wetu mkuki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Vijana wanasubiri, na akili wastahiki,
Mapinduzi kuabiri, kama nchi haijengeki,
Na huu si ujibari, nia tutaiafiki,
Wasiojisaidia, Mola hawasaidii!

Friday, October 14, 2011

Dhahabu na madini mengineyo: Ipo bado nafasi ya Watanzania kunufaika zaidi

VIONGOZI wa Tanzania toka chini hadi juu wanakiri kwamba makosa yalifanyika katika kukaribisha wawekezaji katika uchimbaji madini nchini na inaelekea kitu kama hicho pia kinatokea katika shughuli za uchimbaji madini.

Makosa hayo ni pamoja na kufanya maisha na makazi ya wazawa wa maeneo husika kama vile hayana thamani kabisa; hawana urithi katika eneo husika wa madini na mali asili yake; kuwa serikali kuu ndiyo yenye sauti ya mwisho kuhusu maeneo ya wakazi na wenyeji husika; kwamba kuna watu waliopewa chochote kwa jina lolote lile ili kupata mikataba ambayo inawaruhusu kuchimba na kuchukua madini yetu sawa na bure; na kwamba baada ya Watanzania kuwa masikini kwa zaidi ya karibia miaka hamsini toka wawe huru; uwekezaji na ubinafsishaji huu kwa wageni ni hakikisho rasmi kwamba wataendelea kuwa masikini kwa miaka hamsini zaidi ijayo kama sio miaka 100 na zaidi.

Hata hivyo, wahusika wakuu ikiwemo kampuni moja maarufu na yenye jina kubwa duniani na iliyo na mirija katika makontinenti na nchi kadhaa ni kampuni iliyojenga sifa ya kuwatumia viongozi mbumbumbu, waroho na wasio na uchungu na watu wao na maendeleo yao ili kuwekeza kwenye nchi hizo na kuendeleza himaya na utajiri wake katika migodi, uchimabaji na uuzaji madini wakati mwingine katika nafasi ya ukiritmba na faida za kutisha.

Tanzania chini ya uongozi ulioridhika, kutoshekana na unaoamini kwamba Watanzania wengi wanaishi kwa zaidi ya miaka 1,000 hawana haraka kabisa na kulitazama upya jambo hili na kuchukua hatua mwafaka kwa wakati mwafaka. Na hili linafanyika wakati kuna ripoti zisizokanushika kwamba kuna mamia kama sio maelfu ya binadamu na wanyama katika maeneo fulani wanadhurika na wengine hata kufa kutokana na uchimbaji madini wa kampuni hii na nyingine kama hizo ambao zimepewa migodi kama zawadi na viongozi wetu.

Wakati tunaadhimisha miaka 12 ya kifo cha Baba wa Taifa ni wakati mzuri kutafakari kwanini mzee hakuwa na haraka na shughuli za uchimbaji madini. Na kwanini alikuwa mstari wa mbele kuanzisha Kitivo cha Jeolojia pale Mlimani na kisha kuhamasisha nchi zingine za Afrika Mashariki ili Tanzania iwe kituo kikuu cha utafiti wa madini Afrika Mashariki na kati. Juhudi ambazo kwa sababu moja au nyingine zimekwamishwa mahala fulani na leo tunaambiwa eti sababu moja ya kuruhusu uwekezaji sawa na bure eti ni kwa sababu hatuna vifaa wala wataalamu wanaoweza kutuwezesha sisi wenyewe kuchimba madini yetu. Jambo kama hili sio tu ni vigumu kueleweka na kuaminika bali linaonyesha kwamba tuliowapa kazi ya uongozi hawaongozi bali wanacheza na nchi na maisha yetu kutokana na sababu wanazozijua wao wenyewe.

Hata hivyo, nchi za Argentina, Bolivia, Ecuador na Peru zinatuonesha kwamba wananchi wanaweza kuikataa mikataba dhalimu iliyopitishwa kisiri na kiwiziwizi na walioko madarakani na kudai mikataba mipya itakayokuwa na manufaa na maslahi kwa wazawa wa maeneo husika na nchi nzima kwa ujumla.

Kwa wale waliotazama hali ilivyokuwa huko Argentina na jinsi Waargentina walivyosimama kidedea na kuifosi Barricks kubadili mikataba yake ya kidhalimu (Al Jazeera, Oktoba 14, 2011) atakuwa bila shaka amefaidika kwa mengi ikiwemo hatua kikundi cha kijamii kinachohitaji kupitia ili kuhakikisha mapinduzi haya ya kukabili makampuni ya kimataifa yenye tabia za kitapeli na kidhalimu kutokana na kuwatumia viongozi wenye ubinafsi na wanaojali maslahi ya kikundi kimoja katika nchi na wasioona mbali na mbele kwenye nchi masikini kama Tanzania.

Ingawa mikataba ya kuuza au kukodisha migodi kwa wageni imeshasainiwa na wageni wanaendelea kufaidika na dhahabu na madini yetu mengine bado hatujachelewa kabisa kuibadili hali hii. Tunaweza sisi wananchi, tukisaidiwa na wanasheria wetu na vyama vya siasa vyenye viongozi wenye uchungu na dhiki na umaskini wa Watanzania kuidhibiti hali hii na fumba na kufumbua tukajikuta tuna uchimbaji madini nchi wenye manufaa na tija kwa Watanzania walioko kwenye maeneo yaliko machimbo hayo na sisi tunaoishi mbali na maeneo hayo.

Kwa maneno mengine ni ujinga kukata tamaa kwamba kitu kilichoko katika ardhi yetu sisi wenyewe Watanzania hakiwezi kututoa kwenye umaskini wetu, lakini eti kinaweza kwenda kuwapa utajiri wawekezaji waliowekwa na viongozi wasiowatakia mema wananchi wa nchi hii utajiri mara mia au elfu katika kipindi cha miaka michache tu. Na kwamba pamoja na kuishi katika umasikini kwa zaidi ya miaka 50 kabla ya uchimbaji madini, tunaweza tena kwa roho mbaya na ubinafsi wa viongozi wetu kuendelea kuishi kwa miaka zaidi ya 50 kama sio 100 kama masikini wa kutupwa katika nchi yetu.

Ipo bado nafasi ya Watanzania kuwawajibisha viongozi wao na wale waliokula na kufaidika na uwekezaji wa wale wanaochma madini na mafuta nchini mwetu leo. Na sio kunufaika tu, bali hata kutajirika na wale waliohamishwa katika maeneo yanakochimbwa madini na mafuta kuwa na hisa katika makampuni yanayofanya shughuli hizo katika maeneo yao ya kuzaliwa ambayo leo wamefukuzwa na kujikuta hawana tena makwao.
Huu ni wakati mzuri sana wa kutumia mchakato wa katiba mpya kuijulisha bila uoga wala kificho serikali kwamba mali asili na
madini ni ya wakazi wa eneo, tarafa, wilaya na mkoa husika, kwanza kabla ya yote ni mali ya wakazi hao na sio mali ya serikali wala chama chochote cha kisiasa hapa nchini. Sio haki na ni dhuluma iliyopitukia mipaka kwa kiongozi yeyote aliyeko Dodoma au Dar es salaam au popote pale alipo kunufaika na madini ya Bulyanhulu, Merelani, Geita, North Mara na kwingineko wakati mkazi na mzawa wa eneo husika anahukumiwa kulalia utajiri na kuamkia ukata na kufa masikini baada ya kufagiwa toka eneo husika.

Endapo kuna wanasiasa au viongozi yeyote walionufaika kwa kutoa kibali cha umilikaji eneo, uchimbaji na uuzaji madini nje wanastahili kujiwajibisha wao wenyewe kabla hawajawajibishwa na nguvu ya umma.

Tulivyozoea huko nyuma, eti, serikali ilijichukulia kama baba na mama wa Watanzania wote. Na mali yote ya umma ilikuwa ni mali ya serikali. Hivi leo mambo sivyo yalivyo. Kuna kikundi cha watu wachache wanaojifanya wao ndio wanaomiliki mali zote za Watanzania sio kwa kuzitunza kwa faida ya Watanzania wote bali kwa kuzitumia na kuzifuja kwa manufaa yao wenyewe.

Katika hali kama hii, katiba mpya, pamoja na mambo mengine lazima ieleze kinagaubaga kwamba ipo haja ya kutathmini upya mali asili, madini, mafuta na rasilimali nyingine upya na thamani hiyo iwe ni mtaji na mali ya wananchi wa eneo husika na siyo ya kundi la wajanja wachache ndani au nje ya serikali kwa niaba ya wnaasiasa na viongozi fulani.

Laiti ardhi na mali asili kwenye maeneo yanakochimbwa madini na vitu vingine vya thamani leo ingefanyika kwa haki na usahihi hakuna mkazi wa maeneo hayo leo angelikuwa ni maskini na baadhi yao wangelikuw ana hisa nono katika makampuni yaliyopo hivi leo. Ujinga, uoga na kutokujua kwa wanavijiji haki zao kumechangia hili. Na ndio maana baadhi yetu tuna kampeni za kutaka kuona madaraka zaidi kwa mikoa, wilaya, tarafa, kata na vijiji ili viongozi wa juu wa taifa wasitumie mianya iliyopo kunyonya na kuwadhulumu watu wa maeneo fulani nchini.

Hatua za mwanzo kufanyika

Makampuni yaliyopewa migodi sawa na bure yanatambua ukweli huu, kwamba yanatunyonya tena kwa ile mbaya sana. Na baadhi yao wameanza kuzinduka na kuanza kuwagawia Watanzania kama mababu zao walivyofanya huko nyuma, shanga, vioo, nyembe na vipande vya nguo ili sisi kwa ujinga wetu tuendelee kuwaachia kuokota almasi na dhahabu yetu sisi tukiona hicho wanachotudanganya nacho kwamba eti kina thamani. Ninaamini Watanzania wa leo, hata wale wasiokwenda shule, sio wajinga kiasi hicho. Watanzania hawawezi kabisa kudanganyika kwa barabara, maji, shule na vitu kama hivyo ambavyo serikali yao kutokana na kodi wanayotoa na kama viongozi wangelipunguza mishahara na posho zao kwa asilimi hamsini tu wangelivipata.

Wanavijiji wawatafute watoto wao waliosoma sheria, jeolojia na menejimenti kuja kusimamia vuguvugu la kudai haki ya asili na kutajirika na madini na maliasili katika eneo lao.

Kikundi cha kuelimisha, kuelewesha na kuhamasisha kudai haki na utajiri kiandaliwe mapema iwezakanavyo na kazi yake kubwa ikiwa ni kuwafanya wanajamii wote kuwa kitu kimoja katika madai yao ya kutajirika kutokana na madini au maliasili zao na sio mgeni au wageni tu kunufaika na mali zetu, wakati wao tayari ni matajiri wa kutupwa, eti tu kwa kuwa kuna viongozi na wanasiasa wetu fulani, wananufaika na uwekezaji huo. Kitu kama hiki kinaendana kinyume kabisa na maadili aliyotuachia baba wa taifa pamoja na katiba yetu hii chakavu tuliyonayo leo.

Ni vizuri pia kwa viongozi wa jamii kusaidiwa na vyama visivyo vya kiserikali kwenda kwenye nchi ambazo tayari wananchi wake wananufaika na madini na mali asili zao mbalimbali kama vile Argentina, Bolivia, Peru na kwingineko.

Baada ya watu kueleweshwa na kuelimishwa kwamba wana nafasi bado ya kuwa matajiri na kuwa na hisa katika makampuni ya migodi kitakachofuatia
ni kampeni ya nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha kwamba kila mpenda mabadiliko na maendeleo anakuwa ni sehemu ya vuguvugu na kila mtu kukubali kwanza kula shubiri kabla asali haijapatikana.

Baada ya kila nyuma na wakazi wake kulielewa na kulikubali hili kazi inayofuatia ni kuwa na mikutano ya mtaa, kata, tarafa, wilaya na mkoa ifanyike ili kuwafahamisha viongozi sababu, malengo na madhumuni ya vuguvugu la kurejeshewa haki na utajiri wa maeneo ya wazawa yaliyoachiwa wawekezaji kimakosa au kiujanja na baadhi ya wanasiasa na viongozi nchini.

Zoezi hili litapima viongozi mbalimbali kama wanasimama kuwatetea wananchi na maslahi yao au viongozi hao ni vibarakala wa serikali na vyama vya kisiasa na hawana habari kabisa sio tu na kesho ya wananchi husika bali hata leo yao pia hawana habari nayo.


-mikutano ya kuelimisha uongozi wa taifa

Hii ina maana mbunge, mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa ni lazima asimame na kuhesabiwa. Hesabu hii ndiyo itakayoamua kama nchi inafaa kuwa na viongozi wa kuteuliwa au wa kuchaguiwa na wananchi wa eneo husika. Maana unaweza kukuta wananchi sio tu wananyonywa mali asili na rasilimali zao nyingine na serikali kuu na viongozi wake, lakini pia wanabebeshwa mizigo wasiyostahili kubeba.

Masharti muhimu:

Ili kazi hii ya kudai haki na utajiri tokana na maliasili za wananchi ifanikiwe yapo masharti kadhaa:

Kwanza, zoezi zima lazima liendeshwe kwa nguvu za umma chini ya usimamizi ya watoto na wajukuu wa jamii husika waliosomea masuala ya sheria, madini, siasa na utawala, menejimenti, sayansi ya maamuzi, teknohama, fedha na uwekezaji na kadhalika.

Thamani ya mapato kutokana na uchimbaji dhahabu ifanyike kulingana na mapato yatakayopatikana tokana na uchimbaji na uuzaji dhahabu toka mgodi uanzwe kuchimbwa hadi dhahabu kumalizika kuchimbwa. Hii ina maana kama dhahabu imeanza kuchimbwa mwaka 1997 na itamalizika 2047, hii ni sawa na mapato ya miaka 50 na hesabu hii ndiyo itakayogawanywa kuwalipa fidia wanavijiji husika kama wabia pamoja na mwekezaji, serikali kuu, serikali ya mkoa, serikali ya wilya na wanaharakati watakaochangia kufanikisha jambo hili.

Ni lazima baada ya hpo kugawana faida sawa na wawekezaji katika uchimbaji dhahabu na madini kama hayo, na pale kampuni inaposhaurika ni vyema zaidi wananchi wa eneo husika na sio viongozi wasiohusika na eneo hilo kupewa hisa katika kampuni inayoshughulika na uchimbaji wa madini husika.

Uchimbaji dhahabu usilete madhara kwa wanadamu au mifugo, na kampuni au mtu yeyote anayesababisha madhara au vifo vya binadamu au wanayma kutokana na uchimbaji wa madini laima ahukumiwe kwa mujibu wa sheria za mauaji zilizopo hivi sasa.

Ni lazima wanavijiji ambao maeneo yao yalikwishataifishwa na kubinafsishiwa wawekezaji, walipwe fedha wanayostahili na kama fedha hiyo ililiwa na wakubwa basi irudishwe au mwekezaji alipe upya wanavijiji.

Wanasheria wanaojitolea kwa gharama ndogo wasimamie zoezi zima la ulipwaji upya wanavijiji. Wanasheria hawa wachangie pia kupatikana wawekezaji mbadala kutoka Brazili, Uchina, Vietnam, Korea, India, Urussi na kwingineko kule ambako kutawapatia wananchi wawekezaji watakaowanufaisha na kuwatajirisha wao pia kuliko wawekezaji hawa wa kutoka Kanada, Marekani na Afrika kusini waliopo hivi leo na wanaosadikiwa kula na kulindwa na wale walioko madarakani.

Wanavijiji wapewe hisa katika migodi au kampuni za dhahabu na madini mengine kwenye maeneo yote ambako migodi imeanzishwa na wao ndiko kulikokuwa na makazi yao ya awali toka walipozaliwa hadi kuhamishwa kwa mabavu na bila fidia au kwa kulipwa fidia sawa na mzaha!

Sunday, October 2, 2011

Huwezi kupambana na soko huru, kubali yaishe....

MANENO kama magendo, uvushaji mali mipakani, njia za panya, rushwa, ujangili, uhujumu uchumi ni maneno ya wanasiasa na mangimeza uchwara ambao wameshindwa kuukubali utandawazi na kwenda na wakati kwa kuilalia sekta moja ya uchumi na kuinufaisha zaidi sekta nyingine.

Penda usipende ukishaamua kufuata soko huru, ni ujinga kutaka kupambana na soko hilo kwani lina nguvu zake zisizoonekana na hizo ndizo zinazofuatwa na sio kauli za wanasiasa.

Safari, kauli na maneno ya wanasiasa yanayotolewa hivi sasa ni jitihada za kujikosha na kujisafisha baada ya kushindwa kufanya kazi wanayostahili kuifanya na badala yake kurukia yale yanayostahili kufanywa na soko bila ya kushinikikizwa na mtu.

Kwa mfano tunaona maamuzi ya EWURA yanavyochangia zaidi kunganya watu badala ya kunufaisha umma kwa sababu taasisi hiyo inataka kuingilia moja kwa moja maamuzi ya soko badala ya kuandaa na kuendeleza mazingira ambayo yatafanya sekta husika kufanya maamuzi yanayofaa kutokana na ujenzi wa ushindani na kuongeza sauti ya walaji nchini.

Sukari ni bidhaa inayotokana na zao la miwa. Miwa hii inapochakatwa ndipo sukari huzalishwa. Inavyoelekea ni rahisi sana kuachia soko huru kufanya kazi pale uuzaji miwa kwa wenye viwanda unapohusika, lakini ni rahisi kuingilia soko huru pale uuzaji sukari unapowanufaisha zaidi wenye viwanda na wafanyabiashara kuliko wananchi. Huu ni walakini wa mipango na sera. Na mipango na sera havifanywi kwa kushtukia bali ni vitu vinavyochukua muda.

Nilishawahi kuzungumzia jambo hili katika kesi ya saruji. Ghafla saruji ya Tanzania ilijikuta ina soko zuri nchi jirani. Kama ilivyo kawaida wanasiasa walichoona ni kuzuia saruji isiuzwe nje. NIkadai hilo ni kosa. Nikashauri kwamba, Malawi na Afrika Kusini na nchi za mbali zilikuwa na sukari nzuri tu iliyokuwa ikiuzwa kwa bei nafuu kuliko yetu, hivyo sisi tukubali kuuza yetu kwa bei ya juu kwa majirani na sisi tununue saruji ya bei rahisi toka nje. Hii ni akili ya kuzaliwa ya kibiashara na sio jambo kubwa kiasi hicho.

Ninarudia tena ni makosa kuingilia soko ila tu kama tunataka kuonesha unafiki wa kisiasa na machozi ya mamba eti tunawapenda sana Watanzania.

Kama tunawapenda Watanzania tatizo sio bei ya sukari, bali ni gharama za uendeshaji viwanda vya sukari na mashamba ya miwa. Mipango na sera za kuwapenda Watanzania zilikuwa zinatakiwa kuanzia huko kwa kuhakikisha kuwa bei ya dizeli, gesi na umeme, gharama za usafirishaji, nauli, upatikanaji umeme na mipango mibadala kiuchumi inakuwepo kwa wakati na hatufanyi kazi zetu kama vile zimamoto.

Nimewahi kuongelea pia juu ya ukubwa wa nchi hii ambao umeegemea zaidi kunufaisha mkoa wa Dar es salaam na wakazi wa Dar es salaam kuliko watu wa sehemu nyingine yoyote nchini. Kwa sababu hiyo bei za Dar es salaam ni rahisi kuliko za Ujiji, Tunduma, Mtwara, Peramiho, Bukoba, Holili, Namanga, Mwanza na Tarime.

Hali hii ya unafuu kwa Dsm na ughali kwa mikoa iliyo pembezoni ni kosa la kimipango na kisera linaloendelea kufanywa na serikali na chama tawala kwa kushindwa kutimiza ahadi na nadhiri yake ya kuufanya Dodoma kuwa mji mkuu wa nchi na vilevile kukaidi ushauri wa baba wa Taifa wa kupeleka madaraka mikoani au angalau kwenye ngazi ya kanda.

Makao makuu ya serikali yangelikuwa ni Dodoma ni dhahiri jiji la Dar es salaam lingebaki la kibiashara na hivyo kunufaika zaidi kibiashara na sio pia kisiasa na kiutawala kwa ofisi nyingi za kisiasa na zile za kiserikali kuwa na makao yake makuu mkoani hapa. Mikoa pembezoni ingelinufaika sio haba na kile Dar inachonufaika nacho leo, na hivyo wananchi wake kuwa na nafuu kubwa zaidi maishani.

Madaraka mikoani yangeruhusu mikoa iliyoko pembezoni moja kwa moja kufanya biashara na nchi jirani na kunufaika kijamii na kiuchumi kuliko ilivyo hivi sasa. Hakuna haki yoyote kuwazuia wazalishaji wa kitu chochote hapa nchini kupata bei nzuri soko la dunia au masoko ya nchi jirani. Hiyo siyo kazi ya wazalishaji wahusika, kupata vitu vya bei nafuu ni kazi ya serikali na sio lazima iwalazimishe wazalishaji wauze kwa bei serikali inayotaka. Wakijaribu kufanya hivyo kwenye sekta ya viwanda, hakuna (kama kweli bado nchi ina viwanda) kiwanda kitakachokubali na kubakia kuzalisha hapa nchini. Hii ni amri ya soko huru. Na soko huru sio tu katika bidhaa za viwanda bali pia katika mazao ya kilimo ambayo pengine ni muhimu zaidi kuliko kwa maisha na uhai kuliko bidhaa za viwandani.

Aidha, wakati umefika kuipa sekta ya kilimo uhuru ambao tayari sekta ya biashara na viwanda unayo, kama kweli tunataka kuona mapinduzi ya kilimo yakizuka nchini.

Tuliwahi kuongelea huko nyuma juu ya kuzifanya balozi zetu za nje kuwa ni balozi za kiuchumi na kimkakati. Huu ni wakati muafaka balozi zetu kuwa na watu wanaofuatilia masoko na pale inapoonekana mazao na bidhaa zetu yana bei nzuri nchi za nje basi tuuze, na sisi kama walivyo seremala badala ya kukaa kwenye viti tukae kwenye mbao tukijua kwamba kwa kufanya hivyo tunaweza kuja kuwa na samani bora zaidi siku zijazo.

Afrika ina kasoro moja kubwa. Na hii siyo nyingine ila ni kule kuongoza nchi na kuishi kama vile mambo 'yatajiseti' yenyewe, na wahusika wakaacha kuwa na mipango na mikakati hai ambayo inaweza kuleta utofauti mkubwa katika mustakabali wa nchi na watu wake. Hii ni lazima iwe ni visheni ya muda mrefu na sio mpango wa papo kwa hapo.

Ukichangia na kasoro mbalimbali katika mifumo, miundo, uratibu, udhibiti na utekelezaji ni rahisi kuona kwanini wanasiasa Afrika huona kuwa kuingilia soko huru ni njia ya mkato katika kufanikisha malengo yao ya kisiasa hata kama yale ya muda mrefu kiuchumi yanaharibika.

Fedha ambazo sasa serikali za mikoa/mitaa inazibeba katika vita visivyo na tija dhidi ya wauza sukari nje, ni bora zitumike kutatua matatizo ya wakazi wa mkoa husika kuliko kufujwa kama zinavyofujwa.

Ni vita isiyo na tija maana kimahesabu katika suala zima la magendo mipakani changamoto sio kuzuia tu bidhaa isivuke mpaka bali kubwa zaidi ni kuona hali, silaha za Kisaikolojia na maisha ya wale unaotaka washiriki katika vita hivyo. Ni dhahiri vita dhidi ya magendo ya sukari mipakani tayari vimekwishashindwa hata kabla havijaanza kwa sababu mlolongo mzima wa wale wanaotakiwa kuzuia sukari kuhusu nje kwa bahati mbaya ni orodha ya watu wenye njaa na kiu kali ya hali bora ya maisha na ambao hivi sasa wanaona kifo kwao ni karibu zaidi kuliko malengo mbalimbali waliyojiwekea kimaisha.

Ni polisi gani atakataa milioni 20 achilia mbali milioni 40 huko mpakani; ni ofisa uhamiaji gani atakataa milioni 100 katika mipaka yetu na kuna kioingozi gani mwenye uthubutu wa kukataa zaidi ya hizo katika mikoa yetu inayoongozwa na viongozi ambao hawakuchaguliwa bali wanateuliwa na wakubwa na aghalabu sio wazawa wa mikoa husika na hawana mapenzi wala uchungu na mkoa au wilaya wanaoyoisimamia!

Vita dhidi ya magendo kwa kutumia watu wenye dhiki, njaa, ukata na mishahara duni ni muhali kufanikiwa. Kinachoweza kufanikiwa hapa ni mipango na sera zinazoendana na soko huru na sio vinginevyo. Maana mwisho wa yote, badala ya wafanyabiashara tu kuwa ndio wanaonufaika basi unafaidisha pia wengine kiulaini kama vile watumishi vyombo vya ulinzi, maofisa kodi, maofisa uhamiaji na watu kama hao kwa hasara ya nchi nzima na wananchi wote kwa ujumla.