Mtu mmoja mmoja kwa ujumla wao ndio wanaounda taifa. Inapofikia mwisho wa mwaka inafaa kila mtu kujipima na kuona amefanikisha nini na ameshindwa nini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Wengi wanaamini kuwa wamekuwa wakipiga ‘maktaimu’ kwa kipindi chote hicho na sababu kubwa ikiwa ni kuwa kipato hakilingani kabisa na mahitaji yao ya kimaendeleo na matumizi ya kawaida.
Hii haiondoi ukweli kuwa katika nchi hii bado kuna visiwa vya utajiri na kila siku iendayo kwa Mungu tunaona maghorofa yakisimamishwa, magari mapya yakinunuliwa, biashara mpya zikifanyika na ‘dili’ za mabilioni zikitangazwa.
Hata hivyo kwa Watanzania walio wengi mwaka 2002 ulikuwa mwaka wa mapambano ambayo hayakuweza kutoa washindi lakini kuna wengi waliokata tamaa na kushindwa.
Taifa linalotaka kuwa imara kiuchumi lazima lichunguze kwa makini kwanini hali kama hii inatokea. Haiwezekani kuona kuwa kuna maendeleo ya kiuchumi katika nchi lakini mifukoni mwa wananchi hamna kitu na wao wamebaki pale pale walipokuwa mwaka mmoja au miwili iliyopita.
Utasema nini juu ya hili? Mtu anatumia vibaya fedha yake? Mahitaji yake yameongezeka kupita uwezo wake au mfumo wa kuzawadiwa umepitwa na wakati?
Ukitaka kujua kwa undani maisha ya familia nyingi za Kitanzania ni zile zisizoweza kula nyama sembuse kuku au samaki wasioshikika bei mpaka sikukuu tu.
Kama sera ni kuzuia mzunguko wa fedha ili watu wajifunze kubana matumizi basi sera hiyo imegonga ukuta maana imefikia kikomo cha watu kufunga mikanda na sasa wanaona serikali yao haiwatakii mema.
Familia zilizokuwa na watoto wasiokwenda shule mwaka 1995 serikali ya awamu ya tatu ilipoingia madarakani hivi leo zina watoto wanaokwenda shule za msingi, walioko sekondari na wanaokaribia kuingia Chuo Kikuu.
Ukitazama mfumo wetu wa elimu kama ulivyo hata kama kuna madai ya kuwepo elimu ya bure hapa na pale bajeti kubwa ya Mtanzania katika miaka michache iliyopita imeishia kwenye elimu na nyumbani watu wanalazimika kula mchicha, kisamvu na ugali mchana na usiku.
Katika hali kama hii ni dhahiri kuwa japo watoto wanasoma lakini unyafuzi na utapiamlo unawanyemelea kwa kuwa wazazi wao wana kipato duni kulinganisha na mahitaji ya lishe kamili; hali hii haiwezi kuwaachia wafanye vizuri kamwe shuleni.
Huu ni wakati muafaka wa serikali kuu na serikali za mitaa kuangalia ni jinsi gani wanaweza wakamsaidia mtu mmoja mmoja na familia kuongeza kipato chake badala ya serikali zote kukaa mkao wa kucha na meno wa kutaka ima-fa-ima kumtoza mwananchi kodi hata kama hali yake ni taabani na mtu hawezi hata kuitosheleza familia yake.
Kwa kuwa macho yetu yameelekezwa kwa wageni kama wawekezaji tumesahau kabisa kuwa tunaweza kuwahamasisha wanamtaa wakawa na miradi inayochangia kuimarisha kipato chao na hivyo kupunguza makali ya maisha.
Ni dhahiri hili ni kama lilivyo kwa sababu wengi wetu na hasa tulioko serikalini tunataka kuvuna pale tusipopanda wakati tunashindwa hata kuwaandaa watu kulima, kupanda na kupalilia vyanzo mbalimbali vya kodi ya kesho na keshokutwa.
Kama ilivyo kwa mtaa ndivyo ilivyo kwa kijiji. Vijiji vingi vina uwezo wa kuwa na miradi inayoingiza fedha ikiwa ni ya mtu mmoja au makundi ya watu katika sekta tofauti kama vile maji, elimu, usafiri na uchukuzi, kilimo, biashara, utalii na kadhalika lakini kwa kuwa tumekamia kuvuna pale tusipopanda basi kuna serikali chache sana za vijiji zenye mpango wa kuimarisha uzalishaji mali kwanza kabla ya kuanza kutoza kodi. Kodi ambazo aghalabu huua hata zile shughuli chache za kiuchumi na kijamii zinazoanzishwa na wale wanaothubutu kufanya hivyo katika mazingira magumu ya nchi hii ambayo yamemsahau mwekezaji wa ndani kwa kumkumbatia mwekezaji wa nje.
Kodi ‘kichaa’
Kwa kukosa ubunifu Tanzania sasa hivi sio tu ina utitiri wa kodi zinazowachanganya wananchi lakini pia zina kodi kichaa. Kodi kichaa ni zile ambazo gharama ya kuzikusanya ni kubwa kuliko mapato yanayopatikana kutokana na chanzo husika. Kodi kichaa ni zile zinazoua miradi michanga au miradi ambayo ndiyo kwanza inaanza kubuniwa.
Kodi kichaa ni zile zinazomuonea mlipakodi mfanyakazi ambaye hana njia ya kuzikwepa maana ni ‘fixed and unavoidable’ lakini zinampa mwanya mfanyabiashara anayeingiza mara elfu au elfu kumi au milioni ya mfanyakazi huyo kukwepa kodi kubwa ambayo ingeliweza kuwa nafuu kwa mfanyakazi wa Tanzania.
Mfanyakazi huyo huyo akienda sokoni, dukani au kupata huduma yoyote ya kimaisha au ya kuanzisha mradi bado anakumbana na kodi nyingine nyingi kichaa ambazo aghalabu humfanya ajiulize hivi kweli-‘serikali hainiibii kumnufaisha mtu mwingine na ni nani huyo…?’
Maana kila akizunguka huku na huko haoni kazi iliyofanywa na kodi aliyokatwa. Na zile zinazofanyika zinafanyika nusu nusu tu.
Fedha zinaoza benki
Wakati huo huo, vyombo vya habari vinaruka na habari kuwa kuna mabilioni yamekaa benki kwa sababu hakuna wa kukopesha.
Hakuna wa kukopesha kwa sababu Benki yetu kuu haina utaratibu wa kumnyanyua mzawa kwa mikopo ya riba nafuu wala kuchangia kwenye miradi inayoweza kuajiri malaki ya vijana wa Kitanzania wasio na ajira leo.
Fedha zinaozea kwenye mabenki mengine yale ya ndani na ya nje kwa sababu yanataka kujiendesha kama benki zinavyoendeshwa huko Ulaya au Marekani na sio kama Benki ya Grameen huko Bangladesh.
Juu ya hayo benki zimekosa uongozi kupitia BOT unaoweza kupunguza hatari na hasara ya kukopesha kwa kuzifanya benki 5 au kumi kumkopesha mtu mmoja na hivyo kugawa ‘risk’ hiyo kwa wengi.
Kubwa zaidi ni kuwa mabenki yote kwa kiasi kikubwa bado hayajakaa mkao wa kusaidia Watanzania kuzalisha mali na kuongeza utajiri wa nchi kwa huduma na biashara ili mabenki na wananchi wote kwa pamoja wafaidike.
Tanzania ina kila kitu kwa hivi sasa cha kuifanya iwe nchi imara kiuchumi kama mabenki yatajigeuza kuwa vituo vya kuchochea uzalishaji mali, upanuzi wa biashara kimataifa na utoaji huduma za kimataifa katika sekta mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wa nchi kwa kasi zaidi.
Hofu kuwa Watanzania ni wakopaji wazuri lakini wasiolipa haina msingi. Tatizo ni uaminifu wa watumishi wa benki wenyewe, elimu na maarifa ya kuutumia mkopo kwa upande wa wakopaji. Ipo mifano ya kutosha kuwa Watanzania wazawa wakielimishwa kuhusu kukopa na kuzalisha ili kulipa madeni yao wanaweza kuchangia kuujenga uchumi wa nchi hii kwa kiasi kikubwa.
Mzunguko wa fedha katika uchumi wowote ndio kielelezo cha ufanisi na usanifu ikiwa ni pamoja na tija ya nchi husika.
Mzunguko huo hivi sasa kwa Tanzania unakwaza kwa makusudi ili kuwafunza Watanzania thamani ya fedha. Lakini somo limeshasomwa na likirudiwa rudiwa tena tutawachosha wanafunzi. Hivi sasa watu hawazungumzii tena fedha kwa matumizi bali kwa uwekezaji. Ni wakati gani mzuri kama huu wa kuachia mzunguko ufanye kazi yake na wawekezaji wa ndani waanze kufanya vitu vyao.
Tulichopanda katika elimu ni majengo mazuri na vifaa vya kufundishia kuwepo kitu kilichokuwa hakipo huko nyuma.
Lakini ipo haja ya kuangalia ni jinsi gani tunaweza kupanda na kupalilia mapato, lishe na huduma bora kwa wahusika wenyewe yaani wanafunzi na walimu. Hatuwezi kuboresha elimu kama hatutaboresha kipato na mazingira ya kazi ya walimu.
Hatuwezi kuboresha elimu kama hatuwezi kuwasaidia wazazi kuingiza kipato cha kutosha ili watoto wao wale vizuri na hivyo kuwa na afya ya kuweza kumudu masomo darasani.
Katika afya madai ya baadhi ya watu ni kuwa nchi za Kiafrika ikiwemo Tanzania zinang’ang’ana na ukimwi tu na kusahau magonjwa mengine yanayoua maelfu kila mwezi kwa kuwa gonjwa la kwanza lina mfadhili anayetaka kuona dunia nzima ina maadili ya zinaa kama yenyewe na pili gonjwa hilo eti ni la wakubwa na ndio sababu ya kelele zote hizi.
Sijui ukweli uko wapi hapa. Kwangu mimi, hata hivyo, la muhimu ni kutoa kipaumbele kwa magonjwa mengine na kuachana na projekti za kitoto zinazowafaidisha walio kwenye miradi na sio waathirika iwe ni kwa malaria au magonjwa ya zinaa.
Zoezi la Ubinafsi-shaji, kuuza mali ya umma na mifuko minono ya akiba ya hili au lile nayo ni mambo mengine yaliyopandwa na kupaliliwa kwa misingi ya kunufaisha wakubwa zaidi na bila kuwajali wale wanaokatwa pesa zao. Tuuone ukweli huu na sio kuzika kichwa kwenye mchanga kama mbuni mwerevu.
Tanzania imeonyesha mapinduzi makubwa katika Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kinachotakiwa ni kwa viongozi wa serikali kubadilika na kwenda na wakati ili vitu hivi vitumike kuipa nchi nguvu ya kimataifa katika eneo hili la Kiafrika.
Tunaweza kutishwa na wawekezaji katika sekta nyingine lakini sio hii kama serikali itawasaidiwa wazawa barabara. Na kuwasaidia kwenyewe ni kuondoa kodi kichaa na sheria kichaa. Kodi na sheria zinazoua ari ya kukua na kupanua biashara hizo kwa faida ya nchi na wananchi.
Ushindani na ubepari unahitaji Watanzania wasifungwe fungwe na sheria zisizowafunga wawekezaji toka nje.
Hisia kuwa nchi inauzwa kwa wageni inatokana na ukweli kuwa sisi wenyewe tunadanganyana na tunapeana maneno mengi lakini vitendo daima hamna. Tubadilike na tuanze kupanda na kupalilia moyo wa kutaka kuona kila Mtanzania ananyanyuka na kufaidika na maendeleo ya kiuchumi kesho na keshokutwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment