Watanzania ni Waafrika na wiki hii wana kila sababu ya kuishangilia timu pekee ya Afrika iliyobaki katika kinyang’anyiro cha Kombe la Dunia huko Japan na Korea mwaka huu wa 2002.
Kwa kuwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla hazikufuzu basi wawakilishi wetu sasa ni timu ya Taifa ya Senegal, nchi iliyoko huko Afrika Magharibi.
Historia ya Kombe la Dunia inaonesha Afrika Mashariki haijawahi kutoa timu yenye kiwango cha mpira wa Kombe la Dunia. Ni Afrika Kaskazini, Afrika Magharibi na Afrika ya Kati tu zinazochukua nafasi hizo mwaka nenda, mwaka rudi.
Swali hapa ni je, tutaendelea kuwashangilia wenzetu hawa mpaka lini? Nchi za Afrika Mashariki kila moja peke yake na zote kwa umoja wao haziwezi kuweka mkakati wa kuhakikisha zinasaidiana kuwa angalau na timu moja ya nchi hizi (pamoja na Rwanda na Burundi) kwenda Kombe la Dunia?
Njia ya mkato kwenda Kombe la Dunia
Njia ya mkato kwenda Kombe la Dunia ni kuhakikisha kuwa bara la Afrika na nchi ya Marekani (USA) zinagawanya katika sehemu tano tano (kutokana na nchi/majimbo yao).
Kila moja itoe timu 5 za Taifa (ili kuhakikisha uwakilishi unaoenda kwa uwiano wa idadi ya watu na nchi/majimbo). Afrika iwakilishwe na timu 10 kwa utaratibu wa Afrika Magharibi-timu 3; Afrika Kaskazini-timu 2; Afrika ya Kati –timu 2; Visiwa vya Afrika-timu 1; Afrika Mashariki-timu 1 na Afrika Kusini-timu 1.
Hili litakuwa ni jibu zuri kwa Ulaya ambayo inatoa timu nyingi zaidi kuliko wingi wa watu na ukubwa wa eneo hilo la dunia.
Marekani (USA) kwa kuwa ndiyo imeanza kuchangamkia mpira wa miguu itoe timu tano-kila moja toka Kaskazini, Kusini, Kati, Magharibi na Mashariki. Kwa kufanya hivi FIFA itachangia kasi ya kukubalika kwa soka huko Marekani na hivyo kuongeza utamu na sifa ya mchezo huu kuwa namba moja duniani.
Lakini kama nilivyosema hii ndio njia ya mkato kwenda Kombe la Dunia. Kwa bahati mbaya FIFA inaweza ikachukua miaka 10 kufanya mabadiliko kama haya. Je, tusubiri hadi mteremko au tuwe ngangari na kupambana na hali halisi ya sasa ili tutoe timu ya hadhi ya kimataifa?
Uongozi na maendeleo
Tupende tusipende, michezo kwa kiasi fulani inategemea ari ya kiongozi aliyeko kwenye kigoda. Tazama mashirika au taasisi nyingi ambazo zimewahi kutoa timu bora utakuta kiongozi wa juu mahala pale alikuwa mwanamichezo namba moja yeye mwenyewe au shabiki wa kutupwa wa timu yake ya michezo.
Kwa taifa pia hali si tofauti. Kama kiongozi wa nchi anajali, anathamini na anachangia kuendeleza michezo, vijana wake wanaweza kufanya maajabu katika viwanja vya michezo mahala popote pale duniani.
Wala tusiende mbali. Tazama China ya Mao Dze Dung; Ujerumani Mashariki ya wakati ule; na Cuba ya Castro. Karibu na nyumbani Nelson Mandela kama shabiki wa mpira, ngumi na michezo mingine amechangia sio haba kuwafanya vijana wa Afrika Kusini kuwika kimichezo haraka kuliko ilivyotarajiwa.
Ni dhahiri kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na uongozi wa nchi kutilia mkazo michezo majukwaani au bungeni bado kuna kazi kubwa ya wao kuonekana wanaichukulia michezo sio kama michezo (kitu cha bure na kisicho na maana) bali kama kazi au ajira ya uhakika kwa maelfu ya vijana ambao kwa namna nyingine yoyote hawatobahatika kuajiriwa.
Na ajira, mathalani, katika mpira wa miguu ikiwa ni nje ya nchi inalipa mara kadhaa ukilinganisha na kazi zenye vyeo vya juu hapa nchini.
Wizara inayohusika na michezo ina kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa tunaondoa uswahili na ushambenga katika vilabu na vyama vya michezo. Ni lazima viongozi wa vilabu na vyama wawe sio tu ni wanamichezo bali wana taaluma ya menejimenti na uongozi bora ili waweze kuendeleza nchi kimichezo. Huu si wakati wa kuvumilia viongozi wababaishaji, mbumbumbu na wasiojua dunia inakwenda wapi kimichezo.
Uhasibu na Ukaguzi
Viongozi wababaishaji hugeuza vilabu na vyama vya michezo kama mahala pa kutafuna fedha ya wajinga au mali isiyo na mwenyewe. Wakati umefika sasa wa kulazimisha kila klabu na kila chama cha michezo sio tu kuwa na mhasibu wa kutengeneza mahesabu yake lakini pia wakaguzi wa ndani na wa nje kukagua mahesabu hayo kwa vipindi maalum vitakavyowekwa.
Binadamu hakamiliki ila….
Michezo ni sehemu ya utu wetu. Kitendo chochote kinachomnyang’anya Mtanzania michezo ni kitendo cha kupunguza utu na heshima ya Mtanzania.
Na katika miaka ya leo ambapo michezo hutoa ajira maridhawa kuliko tarafu za aina nyingine ni kumpora mtu pia mkate wake wa kila siku na fursa yake ya kuukata kutokana na michezo.
Kama walipa kodi Watanzania wote kwa umoja wao wana haki ya kudai mitaa, vijiji, kata, tarafa, wilaya na mikoa yao kuwapa viwanja vya michezo.
Hivi sasa kumejitokeza tabia potofu ya viongozi mbalimbali kuona, mathalani, kuwa na majengo ya shule tu ni bora kuliko kuwa na viwanja vizuri na michezo kwa watoto wetu.
Na katika shule hizo ni asilimia ndogo tu itakayopata ajira maofisini au katika makampuni mbalimbali nchini. Laiti kungelikuwa na viwanja vya kutosha vya michezo basi wanafunzi wengi zaidi wangelipatiwa fursa ya kujiajiri wenyewe kama wachezaji soka, tenisi, masumbwi, riadha na kadhalika.
Kwa maneno mengine, viongozi wetu bado hawajatambua umuhimu wa michezo kiuchumi na kijamii na bado wanang’ng’ania kutaka kuiendesha michezo kama sehemu ya siasa.
Michezo kama siasa huendeshwa kwa lengo la kuwapatia viongozi sifa. Michezo kama shughuli ya kiuchumi na kijamii huendelezwa ili kuwapatia vijana ajira inayowawezesha kukimu maisha yao na pia kuwanyanyua kimaisha wazazi na jamaa zao.
Haimsaidii kiongozi yeyote wala taifa kupuuza maendeleo ya kimichezo ya kijana yeyote hata kama sio ndugu yake. Kwa yakini kitu kama hicho hulipunguzia taifa nafasi ya kuingiza mapato dhahiri toka nje.
Ili tunyanyue michezo
Kwangu binafsi ni kosa kuwanyima watoto wa chekechea na shule za msingi nafasi ya kucheza na kukua kutokana na michezo.
Wanasaikolojia wanashauri kwa usahihi kabisa kuwa asilimia kubwa ya muda katika chekechea utumike katika michezo ili kuwa na makuzi yanayowiana kati ya mwili na akili; katika shule za msingi muda wa kusoma na michezo uwe ni hamsini kwa hamsini; katika sekondari na vyuo vya juu iwe ni asilimia 75 (masomo) kwa 25 (michezo). Uwiano huu unafaa kufuatwa pia hata baada ya kumaliza chuo kama mtu anataka aepuke magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na kukosa mazoezi ya kutosha (ikiwemo shinikizo la damu, vitambi kwa polisi na viongozi wa michezo).
Kuwekeza katika michezo
Michezo ni kwa ajili ya wote. Kama hivyo ndivyo hii ina maana michezo ni sawa na usalama na ulinzi (kulinda afya za Watanzania na pengine maadili mema); michezo ni sawa na huduma ya afya (kila mtu ahudumiwe); na michezo ni nishati muhimu kuijenga rasilimali muhimu kuliko zote katika taifa-watu.
Kama ndivyo pamoja na watu wenyewe, serikali kuu na serikali za mitaa lazima ziwekeze katika miundo-mbinu ya michezo.
Ianzishwe kampeni ya kuijenga Tanzania upya kimichezo na katika kampeni hiyo kila mtaa, kijiji, kata, tarafa lazima iwe na viwanja vya michezo ya aina zote. Na miongozo na taratibu ziwepo za kuviendesha ili kufikia malengo ya kutoa wanamichezo bora baadaye.
Timu kwa daraja mbalimbali
Pendekezo linaloweza kwenda mbali katika kuendeleza soka na michezo mingine hapa nchini ni kuhakikisha kuwa panakuwa na timu za mtaa, kata, tarafa, wilaya, mikoa na taifa kwa kila mchezo.
Njia zitafutwe kuhakikisha kuwa michezo inakuwa ni sehemu ya kazi/masomo na panakuwa na mashindano wakati wote ili kuhakikisha nchi hii ina wanamichezo walioko kwenye fomu wakati wowote.
Ni muhimu kwa hivyo mitaa, kata, vijiji, tarafa, wilaya, mkoa na taifa kuwa na bajeti za wazi zinazoonesha mapato na matumizi katika michezo mbalimbali. Japan na Korea kama wenyeji wa Kombe la Dunia wamepata faida kadhaa mojawapo ni ile ya kiuchumi au kibiashara. Vijiji, miji, wilaya, mikoa na nchi inatakiwa kuiga mfano huu na kuutumia kujineemesha kwa namna moja au nyingine.
Aidha lazima tuwe na makocha au walimu wa kimataifa na tusijidanganye na watu wasiofuzu au kuwa na uzoefu wa kusimamia timu za kitaifa. Hii si gharama kubwa kama tunaweza kuwalipa mameneja wa kampuni moja tu mamilioni, kwanini tushindwe kwa kocha wa taifa zima? Tena wakati FIFA inamwaga mapesa Afrika.
Kwa kumalizia nirudie tu kuwa kama Tanzania haitajizatiti kwa namna hiyo hapo juu kimichezo basi kuna hatari ya nchi hii kuwa Dunia ya Tatu kama sio ya nne kimichezo katika bara hili hili la Afrika wakati nchi kama Senegal, Cameroun na Bourkina Fasso zikiwa Dunia ya kwanza.
Sunday, March 27, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment