Sio watu wengi wanaojua kuwa iwapo umefuata taratibu zote za mahakama katika nchi yako na hukuridhika na maamuzi ya mahakama basi unaweza kukata rufaa kwenye kamati maalum ya Umoja wa Afrika inayoshugulikia masuala ya haki za binadamu.
Kamati au tume hiyo hivi sasa iko mbioni kufanywa mahakama kama viongozi wa Afrika wataridhia suala hili kwenye mkutano wa kilele ujao kunako mwezi Juni.
Kwa mfano mjane anayeamini kuwa kanyimwa haki za kurithi mali aliyochuma na mumewe na akapeleka kesi mahakamani lakini ikatupwa nje; akakata rufaa mahakama kuu akashindwa; akakata rufaa tena mahakama ya rufaa na bado akashindwa bado atakuwa na nafasi kama hiyo tena kwenye mahakama hiyo ya Afrika.
Uanzishwaji wa Mahakama Kuu ya Afrika unakwenda sambamba na uanzishwaji wa mahakama ya Umoja wa Mataifa ambayo malengo yake bado yana shabaha ya kufanikisha vita vya haki ya binadamu duniani.
Kwa bahati mbaya sio wengi wanaojua juu ya kile kinachoendelea duniani katika ujenzi wa taasisi na taratibu zitakazohakikisha kuwa haki na usawa mbele ya vyombo vya sheria inakuwa ni ndoto ya kweli kwa kila mtu popote pale alipo duniani.
Hali ilivyo sasa ni kuwa anaweza kuibuka mtu mahala popote pale duniani na kwa kutumia nafasi yake ya uongozi; mipaka ya kile anachoita taifa lake huru; na kwa ushirikiano na wajanja wachache akafanya uhuni mkubwa katika nchi yake ikiwamo kudhulumu watu mali zao; kujitajirisha kwa wizi au rushwa; na hata kuiuza nchi yake na raia katika nchi yake na dunia nzima kwa ujumla isiwe na lolote la kufanya kumkomesha mtu huyo.
Isitoshe yapo matukio kadhaa katika nchi mbalimbali za Kiafrika hivi sasa kuonesha kuwa baadhi ya wale walioko madarakani wanadiriki kuficha au kufukia vitendo viovu, dhuluma, uonevu au vitendo vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika milki yao.
Kwa kuwa na Mahakama Kuu ya Afrika na Dunia na pengine mahakama za rufani katika ngazi hizo pia kutaimarisha uhuru wa mahakama za nchi moja moja na kuboresha haki na usawa kwa raia wa nchi husika.
Inavyoonekana ni kuwa dunia imeona udhaifu wa taasisi za kimataifa ambazo zinakosa meno ya kikatiba na kisheria.
Hali hii imesababisha kwa baadhi ya nchi mahakimu na majaji kuonekana wanawajibika kwa viongozi waliowateua na hivyo kuzifanya mahakama kutokuwa huru.
Ubinafsi pia umejitokeza katika vyombo vya sheria kufikia kiwango cha mwenye fedha kununua haki dhidi ya mnyonge anayestahili haki hiyo.
Maadili yameshuka katika baadhi ya nchi na rushwa sio kitu kigeni katika vyombo vingi vya sheria karibu katika kila nchi Afrika. Mahakama ya Afrika na dunia zitarudisha heshima ya mahakimu na majaji popote pale kwani wale wanaokiuka maadili wataadhiriwa na ngazi za juu.
Uzuri wa Mahakama ya Afrika ni kuwa itakuwa na majaji toka nchi mbalimbali za Kiafrika na pengine hata kutoka nje ya Afrika (kutegemeana na aina ya kesi na uzoefu wa majaji husika). Kitakachopambana katika duru hizi ni ubingwa wa kuitafsiri sheria kwa mujibu wa sheria na mikataba ya kimataifa kwa lengo la kuhakikisha Waafrika wote wanakuwa sawa mbele ya sheria hizo na mwenye haki ndiye anayestahili kunufaika na sio vinginevyo.
Haki za binadamu
Waafrika na wasio Waafrika kwa muda mrefu wamekuwa wakililaumu bara hili kwa kushindwa kuheshimu haki za binadamu.
Vyombo vya dola, yaani polisi, magereza na upelelezi aghalabu vinalaumiwa kwa kukiuka haki za binadamu.
Mathalani, hali ya magereza ya Afrika ukifananisha na yale ya Ulaya au Marekani ni ya kusikitisha na kutisha. Upo uwezekano mkubwa kuwa mahakama ya Afrika itashughulikia suala hili kikamilifu zaidi kuliko mahakama za nchi moja moja ambazo zinaelekea kuistahi au kuihurumia serikali ya nchi husika.
Wenye fedha au madaraka vijijini, kwenye kata, wilaya hadi ngazi za mikoa kwenye nchi mbalimbali wamekuwa wakikiuka haki za binadamu kwa kutumia nafasi zao kunyamazisha vitendo vyao ambavyo sasa vinaweza kumulikwa na kurunzi la mahakama ya Afrika na Dunia.
Demokrasia
Kwa kuwa kumekosekana chombo sahihi cha kushughulikia kutafsiri sheria na katiba katika nchi zetu hivi sasa viongozi walioko madarakani wamepora jukumu hilo na kuanza kutafsiri sheria hizo kwa mujibu wa uelewa wao na kile wanachokiamini wao kuwa ndio haki.
Mahakama Kuu ya Afrika itachangia sio kwa kiasi kidogo kutafsiri demokrasia na nafasi yake katika sheria na katiba mbalimbali za nchi zetu.
Kwa mantiki hii hapatakuwa na seti kadhaa za tafsiri kutegemeana na wale walioko madarakani na kile wanachokitaka wao.
Fujo na matatizo mengine yanayosababishwa na ukiukwaji wa misingi ya demokrasi sasa vinaweza kupata ufumbuzi wa kudumu kwa kuwa na Mahakama ya Afrika na Dunia na jopo la majaji kushughulikia kesi za demokrasia na uchaguzi.
Uwazi na rushwa
Mikataba mingi ya kibiashara ndani na nje ya nchi mbalimbali za Kiafrika inaghubikwa na giza la usiri na kinachofanyika huku kinajulikana na M…. na wahusika.
Mahakama ya Afrika na dunia itamulika masuala yote ambayo ni vivutio dhahiri vya rushwa kama vinafanyika bila uwazi.
Suala la uwazi limekuwa gumu sana kwa viongozi wa Afrika hasa pale maslahi binafsi na yale ya kutaka kuhakikisha chama tawala kinabakia madarakani baada ya kipindi cha utawala wake kwisha. Fedha inahitajika na kiongozi mwenyewe ili aweze kuwa na maisha mazuri baada ya kuondoka madarakani lakini vile vile fedha inahitajika ili kuhakikisha chama kinabakia tena madarakani kipindi kijacho.
Uwazi unakuwa kikwazo mbele ya masaula hayo hapo juu. Na kiongozi hata awe na nia nzuri namna gani kitendo cha kuleta uwazi katika uongozi wake anajikuta katika matatizo makubwa ndani ya chama chake na katika serikali yake.
Hata iundwe tume gani ikifikia kwenye hatua ya uwazi mwanga wa tume hiyo hufifia na kisha kufa kabisa.
Hatuwezi kutegemea viongozi wetu wajikosoe wenyewe; haiwezekani viongozi wetu kujitathmini wao wenywe; na haiwezekani viongozi wetu kujiadhibu wao wenyewe. Ni kwa mantiki hii taasisi ya kimataifa yenye uwezo wa kuwawajibisha hata viongozi au hata kuonesha tu kuwa wana makosa au aibu wanazoficha itasaidia kuongeza hadhi ya utawala katika Afrika.
Utawala bora
Utawala bora hauwezi kuja Afrika bila kuwa na chombo cha juu kinachoweza kukosoa taasisi zetu za ndani.
Mazoea, kutokujua na ukomo wa uwezo wa watendaji katika ngazi mbalimbali siku zote vitachangia kuwa na serikali dhaifu zisizowajibika kwa wananchi.
Hali ilivyo sasa karibu Afrika yote ni ile inayoonesha kuwa watawala ni mabwana na wananchi ni watwana.
Hali hii haiwezi kuruhusiwa kuendelea kama kweli tunataka kuwakomboa watu wetu kijamii, kiuchumi na kimawazo.
Ni pale tu wananchi wetu watakapokuwa na kauli na uwezo wa kuwawajibisha viongozi wao ndio maendeleo ya kweli yataanza kuonekana Afrika.
Mahakama Kuu ya Afrika itaweza pia kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta utawala bora Afrika kwa kusikiliza kilio cha wale wanaoamini kuwa kijiji, mji, wilaya au mkoa au nchi yao haifuati utawala wa sheria wala katiba iliyopo haikidhi haki za chini na za juu za wananchi katika nchi husika.
Msingi wa UA
Mahakama ya Afrika itakuwa jiwe la msingi la Umoja wa Afrika. Misingi mingine ni pamoja na haki ya wananchi kusafiri, kuishi na kufanya kazi popote Afrika; jeshi moja la Afrika; bunge la Afrika ambavyo ni vitu pekee vitakavyoweza kufanikisha kuwa na serikali moja ya Afrika.
Yapo mambo mengine muhimu ya kuzingatiwa na hasa unapoelewa kuwa nchi za Kiafrika hazifanani na kila moja ina historia yake na matatizo yake kutokana na sababu za kisiasa, kijamii na mazingira.
Hata hivyo, misingi hiyo hapo juu inaweza kuwa mwanzo wa kufanikisha kuondoa matatizo ya kila nchi kwani utawala wa sheria na taratibu zinazokubalika zina nguvu na uwezo wa kurahisisha maazimio na mipango mingine kwa kila nchi.
Taasisi zingine ziige mfano
Umoja wa Afrika utaendelea kuwa ndoto kama Waafrika watategemea viongozi wao tu ndio watakaoufanikisha.
Kinachotakiwa hivi sasa ni kwa makundi mbalimbali hapa Afrika kama vile waandishi wa habari, walimu, madaktari, manesi, watumishi wa serikali, maprofesa, wahandisi, wahasibu, vijana, wazee, wanawake na kadhalika kuunda taasisi zao chini ya Umoja wa Afrika na kuanza kuandaa ajenda mbalimbali zitakazoongoza Afrika kule wao na wenzao wote wanakotaka iende.
Heshima na usawa
Umoja na maendeleo ya Afrika lazima ujengwe katika misingi ya usawa na heshima kwa wote.
Bila shaka mahakama ya Afrika itatoa msukumo unaotakiwa katika kuhakikisha kuwa kila nchi inazingatia kuwepo sio tu kwa haki bali usawa na heshima kwa kila mwananchi kama nguzo za kusimamisha mkusanyiko wa watu mkubwa kuliko ule wa utaifa mmoja mmoja kwa nchi mbalimbali za Kiafrika.
Afrika ina nafasi chungu nzima za kujifunza kutoka mabara mengine jinsi ya kufanikisha kuwepo kwa umoja wa Afrika utakaochangia tu sio kuondoa umaskini bali pia kujenga mkusanyiko wa watu utakaopewa usawa na heshima toka popote pale duniani.
Itakuwa ni kitendo cha faraja kama viongozi wetu wataunga mkono kwa hali na mali mpango wa uanzishaji wa mahakama kamili ya Afrika na ile ya dunia.
Sunday, March 27, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment