Thursday, February 23, 2012

Arusha, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza na Ruvuma na umuhimu wa mikoa inayojiendesha yenyewe

YALIYOTOKEA kwenye mikoa ya Arusha, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza na Ruvuma yakitazamwa kijuujuu yataonekana kama mambo ya kuzuka na kutoweka mara moja.

Kwa upande wangu, siamini hivyo. Ninaamini kuwa yanayotokea mikoani leo ni isdhara tosha kuthibitisha dhana yangu ya mikoa huru inayoongozwa na watu waliochaguliwa na sio watu wa kuteuliwa.

Hii ina maana wakati umefika wa kuwa na mikoa inayoendeshwa kama Zanzibar inavyoendeshwa ili mikoa hiyo inufaike kiutawala na kiungozi kama iliyo Zanzibar kwa hivi sasa.

Mikoa inastahili kuwa na kiongozi atakayechaguliwa na wakazi wa mkoa husika na kuitwa ama Waziri Mkuu au Waziri Kiongozi au Gavana wa mkoa husika; bunge lenye wawakilishi wa makundi maslahi ya kila sehemu ya jamii na Waziri mkuu huyo wa mkoa atashikiana na bunge lake la mkoa kuteua mawaziri wa mkoa na hivyo kuufanya mkoa kujitawala na kujiendesha wenyewe bila kuingiliwa mno na serikali kuu na wakati mwingine na watu wakutoka sehemu zingine za nchi wasioutakia mkoa na wilaya zake na wakazi wake mema.

Ninaandika haya, ili wakazi wa mikoa mbalimbali wachukue fursa ya kutathmini ubora na udhaifu wa kuwa na mikoa ambayo wakubwa wake wote wanateuliwa na rais aliyeko madarakani na chama chake na serikali yake. Na kisha kuamua kama wakati umefika au haujafika kwa wakazi wa mikoani kuchagua mkuu wao kwa mkoa kwa jina kama hilo au jengine kama vile Gavana, Waziri mkuu wa mkoa na kadhalika:


Faida za Mikoa yenye Gavana au Waziri mkuu na serikali yao ndogo

1. Kwanza, mkoa utakuwa na kikosi cha kupigania haki zake ikiwemo zile za ardhi na mali asili ya mkoa kunufaisha wakazi wake na sio watu toka nje na viongozi wa serikali kuu wasiozaliwa katika mkoa husika;

2. Fedha na mapato ya mkoa husika kutumika kwa ajili ya maendeleo ya mkoa husika na sio vinginevyo;

3. Wananchi kutonyang'anywa ardhi yao na serikali kuu na watu wasio na asili wala uchungu na mkoa husika;

4. Serikali ya mkoa kuwa na uchungu na maisha a uhai wa wakazi wake kuliko kitu kingine chochotte;

5. Viongozi wa mkoa kuwa karibu zaidi na wananchi wao kuliko ilivyo hivi sasa;

6. Kuimarisha uchumi na ushindani kwa kasi na haraka zaidi kuliko ilivyo hivi sasa;

7. Kuepuka kuyumba kwa mkoa kama serikali kuu itayumba kwa njia moja au nyingine, kwani serikali ya mkoa (kama ilivyo leo huko Ujerumani) zina uhuru wa kuwa na sera zake za kijamii na kiuchumi tofauti na ilivyo kwetu;

8. Kuupa nafasi mkoa wa kutafuta wawekezaji halali na wa kweli watakaounufaisha mkoa na watu wake pamoja na wenye miradi nao kunufaika pia;

9. Kuwa na hadhi ya kimataifa kushirikiana na nchi za nje zenye uhusiano wa karibu na mkoa na watu wake kwa faida ya mkoa husika na nchi nzima kwa ujumla;

10. Kuharakisha maendeleo ya kiteknolojia na uanzishwaji viwanda vinavyolipa haraka zaidi kwa faida ya wakazi wa mkoa husika;

11. Kuwa na maamuzi huu ya kimipango na kimkakati katika kuboresha elimu, huduma za tiba na afya, uzalishaji nishati; biashara, masoko ya ndani na nje ili mkoa uweze kufikia hadhi ya kushindana sio tu na mikoa mingine bali pia na nchi kamili duniani na hivyo kuvuta uwekezaji bora na wa manufaa zaidi kwa kasi na haraka zaidi;

12. Kuchochea wepesi wa mabadiliko katika huduma na uzalishaji kwa maendeleo makubwa na ya haraka zaidi kiuchumi. Kwa mfano, mkoa unaweza ukawa na hospitali zenye hadhi ya kimataifa na hivyo badala ya kupeleka wagonjwa nje, wagonjwa wakapekelekwa kwenye mkoa huo. Aidha, wagonjwatoka nje wakaja tibiwa katika hospitali za mkoa kama huo. Au mkoa unaweza ukawa na shule na vyuo vikuu vyake vyenye hadhi ya kimataifa na watu badala ya kupeleka watoto wao kwenda kusoma nje wakaenda kusoma huko kama ilivyo kati ya Singapore na Malayasia. Na pia wanafunzi toka nje wakaja kusoma kwenye shule hizo za kimataifa katika mkoa husika;

13. Chama cha kisiasa kinachoshinda viti vingi katika bunge la mkoa hutawala mkoa husika hata kama kitaifa kuna chama kingine kinatawala nchi;

14. Kwa kuwa mkoa una idadi ndogo zaidi kuliko nchi, ni rahisi kupanga na kuweka mikakati na mbinu za kupiga vita maadui kama umaskini, maradhi, ujinga na kuwa nyuma kijamii, kihuduma, kiuzalishaji mali, kibiashara, kiteknolojia, kisayansi, kiuchumi, kiutamaduni na kimaendeleo.

15. Nafasi za Waziri mkuu wa mkoa, mawaziri wa mkoa, wabunge wa mkoa na kadhalika zitakuwa ni Chuo kikuu kwa viongozi wa baadaye wa serikali kuu ya JMT tofauti na ilivyo leo, ambapo mawaziri wengi, makatibu wakuu na watendaji wengine wanajifundisha kazi tayari wameshapewa nyadhifa hizo.