Miaka 39 iliyopita viongozi wa Afrika walikutana huko Addis Ababa, Ethiopia na kuunda Umoja wa nchi Huru za Afrika.
Tarehe 9, Septemba 1999 tamko la Sirte lilianza kufanyiwa kazi ili hatimaye kuundwe Umoja wa Afrika (AU). Waraka wa madhumuni na ushirikishwaji wa nchi za Afrika katika uanzishwaji wa AU ulikubalika rasmi huko huko Sirte mnamo Machi 2001 katika kikao maalum ambacho pamoja na mambo mengine kiliamua kuwa kazi itakwisha pale theluthi mbili ya nchi za Kiafrika zitakaposaini kukubali kuanzishwa kwa umoja huo.
Afrika Kusini na Nigeria zinazokubalika kama nchi viongozi Afrika zilisaini Azimio hilo Aprili 23 na 28 mwaka huo huo na hivyo kufanya nchi zilizosaini kuwa 36 na hivyo kutimiza theluthi mbili iliyokuwa ikihitajika kuundwa kwa AU rasmi. AU inasemekana kisheria ilianza toka tarehe Nigeria walipoanguka saini katika mkataba huo.
Pamoja na maneno mengi yanayosemwa kama vile huu ni mvinyo mpya katika chupa ya zamani ukweli unabakia pale pale kuwa hili ni wazo na ni hatua ambayo wakati wake umefika.
Ndoto kuu ya kina Nyerere, Nkrumah, Kenyatta, Haile Sellasie na wengineo ilikuwa ni ile ya kuiona siku ambayo Afrika itatamka bayana kuwa inadhamiria kuungana na ili tuungane tutafanya moja, mbili, tatu.
Kama ni wazo ambalo wakati umefika kinachobakia sio tena kujadili kufaa au kutokufaa kwake bali kuweka mikakati ambayo kwayo nchi moja moja zitanufaika na kwa upande mwingine bara zima litanufaika kwayo.
Ili tuliweke hili katika mwanga utakaotusaidia kupata hoja za nini Tanzania ifanye ili inufaike na kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika ni muhimu kupitia madhumuni ya OAU kwanza, kisha yale ya AU.
Madhumuni ya OAU
Madhumuni ya OAU yalikuwa kwanza, kuendeleza umoja na ushirikiano kati ya nchi za Kiafrika. Kazi hii imefanyika kwa kiasi fulani lakini bado kazi iliyobaki ni kubwa zaidi na ndio maana kuna umuhimu wa kuwa na AU.
Kuratibu na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Kiafrika ili kupiga vita umaskini na udhaifu wa kiuchumi wa nchi za Afrika. Kazi hii bado kabisa haijafanyika. Afrika bado iko nyuma kiuchumi na ni jalala la bidhaa toka mabara mengine.
Kulinda utaifa, mipaka na uhuru wa nchi za Kiafrika. Kwa kuwa mkoloni hajarudi tena kisiasa tunaweza kusema kazi hii ilifanikiwa. Lakini mkoloni huyo kawahadaa Waafrika karudi kiuchumi na isitoshe hata wasiokuwa wakoloni katika bara la Afrika kama vile Japan sasa wanaitawala Afrika kiuchumi.
Ulinzi; huu pia umetafsiriwa vibaya kiasi cha kuruhusu madikteta kuwaburuza watu wao na OAU kushindwa kukemea vitendo vilivyochangia ukiukwaji wa haki za binadamu na kuongezeka umaskini katika nchi kadhaa za Kiafrika.
Kufutilia mbali ukoloni Afrika. Hili limefanikiwa kwa asilimia 98 na pindi Morocco ikiiachia Sahara itakuwa ni asilimia 100.
Kuendeleza ushirikiano wa kimataifa. Hili limefanikiwa sana maana kila nchi Afrika inategemea nchi moja au mbili au zaidi za nje. Lakini ushirikiano huo wa kimataifa katika ngazi ya nchi za Kiafrika kwa Kiafrika bado ni mchanga ukilinganisha na uhusiano wa nchi hizo na nchi zilizoko nje ya bara lenyewe.
Madhumuni ya AU
Madhumuni ya AU kama nilivyoyaelewa ni kama ifuatavyo:
• Kufanikisha umoja na ushirikiano mkubwa zaidi kati ya nchi za Kiafrika na watu wa Afrika;
• Kulinda utaifa, mipaka na uhuru wa nchi wanachama;
• Kuharakisha kasi ya umoja wa kisiasa na kiuchumi wa Afrika;
• Kuendeleza na kulinda kwa pamoja yale yote yenye maslahi kwa bara hili na watu wake;
• Kupigia debe ushirikiano wa kimataifa kwa kuzingatia Azimio la Umoja wa Mataifa na Tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa;
• Kuendeleza amani, ulinzi na utulivu katika bara hili;
• Kuendeleza misingi na taasisi za kidemokrasia, ushirikishwaji umma na utawala bora;
• Kuendeleza na kudumisha haki za binadamu na haki za watu kulingana na Tamko la Afrika juu ya haki za Binadamu na watu na taasisi zinazohusika;
• Kuweka mazingira muafaka yatakayowezesha bara hili kushika nafasi yake stahilivu katika shughuli za kiuchumi za dunia na mapatano ya kimataifa;
• Kupigia debe shughuli–endelevu katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ikiwa ni pamoja na kujenga uchumi mmoja kwa Afrika;
• Kuendeleza ushirikiano katika nyanja zote za maisha ya wananchi ili kuinua hali ya maisha ya Waafrika;
• Kuratibu na kusawazisha sera zilizopo kati ya maeneo mbalimbali yaliyopo hivi sasa na yatakayoanzishwa ili kurahisisha kufikiwa kwa malengo ya Umoja wa Afrika;
• Kusukuma mbele maendeleo ya bara hili kwa kuendeleza utafiti katika nyanja mbalimbali na hasa sayansi na teknolojia; na
• Kushirikiana na mapatna wa kimataifa mbalimbali wanaostahili ili kufuta kabisa magonjwa yanayofutika na kuwa na huduma bora za afya barani humu.
Sidhani kama kuna Mwafrika atakayekataa kuwa haya sio malengo yake. Kama ndivyo sasa tuone Tanzania tunahitajika kufanya nini ili fursa zinazotokana na AU ziwe zetu zote.
Tanzania ifanye nini?
Kwanza, tusipoteze muda kuwa na Katiba mpya itakayozingatia matarajio ya Watanzania na matakwa ya AU.
Serikali ya Tanzania ijitoe kwa hali na mali kuendeleza Kiswahili ili kishike nafasi yake ya kimataifa na vile vile kurahisisha Umoja wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Serikali ifute sheria ya kuvizuia vyombo vya habari kutangaza kwa zaidi ya asilimia 25 ya nchi na vyombo hivyo visaidiwe ikiwezekana ili visikike Afrika nzima. Vyombo hivyo ni pamoja na redio, televisheni na magazeti yanayotoka kwenye mtandao.
Kituo cha uwekezaji Tanzania (IPC) kisiwe kwa ajili ya watu wanaowekeza tu Tanzania bali pia kiwe na kitengo cha kuwasaidia Watanzania wanaotaka kuwekeza nje ya nchi. Iwe Kenya, Uganda, Msumbiji au hata Ulaya.
Kazi kubwa ya serikali na hasa Balozi zetu za nje iwe ni kusaidia tuwe na miguu ya kiuchumi ndani ya nchi mbalimbali zinazotuzunguka. Wenzetu wa Nigeria wamefanikiwa sana katika hili twendeni tukajifunze kwao.
Kuzisaidia nchi zinazotuzunguka kwa kuwapa walimu, manesi, madaktari, na wafanyakazi au wataalam wengine wanaowahitaji. Kusaidia kuendeleza na kupanua shule za msingi, vyuo na vyuo vikuu ili viweze kupokea wanafunzi toka nje ya mipaka yetu.
Kiingereza, Kiarabu, Kifaransa na Kiswahili yawe masomo ya lazima sekondari na kwa baadhi ya shule za msingi. Hii itawasaidia vijana wa Kitanzania kupata kazi katika shirika lolote la AU bila mikwara.
Tanzania ikubali kuwapokea wageni; wawe Waafrika au wasio Waafrika wenye vipaji au ufundi tusio nao sisi kuja kufanya kazi na ikiwezekana kuwa raia wa Tanzania katika kipindi kifupi tu endapo wanataka wenyewe.
Kuikumbatia na kuieneza teknolojia ya habari na mawasiliano hadi kufikia ngazi za mitaani na vijijini katika muda mfupi kuliko nchi nyinigine yoyote ya Kiafrika ili tuwe na wataalamu wa kwenda kufanya kazi nchi nyingine na kutuingizia mapato kiulaini.
Kuigeuza Tanzania kama soko la Kimataifa kwa eneo hili la Afrika ili kuondoa uwezekano wa nchi yetu kumezwa kabisa kiuchumi na Afrika Kusini.
Kwa kuagiza bidhaa toka Indonesia, Thailand, Taiwan, Korea Kusini, Malaysia kwa bei rahisi na kisha kuziuza tena nje ya mipaka yetu kwa bei nzuri kama Nigeria inavyofanya itatuhakikishia mapato yatakayochangia kufufua uwezo wetu wa kuzalisha baadhi ya bidhaa nchini mwetu.
Askari walipwe mishahara mizuri ili kuhakikisha wanafanya kazi yao ya usalama wa raia na mali zao ili tuwe mfano wa kuigwa na nchi nyingine na askari wetu kupata ajira nje kutokana na rekodi yao nzuri.
Mikakati ya ujenzi na ukarabati wa barabara iwe endelevu na isiyokwama mahala na wakati wowote ili shughuli za uchumi zizunguke saa ishirini na nne bila kusimama.
Maji, umeme na huduma mbalimbali za jamii isiwe kero tena nchini. Vipatikane kama vile hewa tunayopewa bure na Mwenyezi Mungu.
Tuwalipe madaktari na manesi uzuri ili wafanye maajabu. Tuwe na teknolojia ya wakati huu katika mahospitali ili tusilazimike kupeleka wagonjwa wetu nje ya nchi.
Nchi hii ijitosheleze kwa chakula, mavazi na makazi ili kuwapa watu wote heshima na staha wanayostahili.
Magereza yetu yawe na utu na ubinadamu pamoja na kuwa vyuo vya kurekebisha tabia na sio vyuo vya kuozesha tabia.
Kosa kubwa linaloweza kufanywa na Tanzania ni kubakia au kuendelea kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo kama: itakuwa ni kilabu ya kulindana viongozi; itapata viongozi wababaishaji na wasioisogeza hata hatua moja Afrika kuelekea kuungana; itawavumilia viongozi wanaowaua watu wao kwa sababu ya tamaa ya kubaki madarakani; au itakuwa na viongozi ambao dhahiri bin shayiri ni madikteta na watu wasiokubali wala kuipenda wala kuitaka demokrasia kwa lolote lile.
Leo AU wakati wowote kuliko huko nyuma inaonekana ni klabu iliyoundwa na viongozi wa Afrika ili kulindana wenyewe kwa wenyewe. Dhana ya kuingiliwa mambo ya ndani ni dhana iliyopitwa na wakati. Dhana hii haina tofauti na baba mlevi ambaye kashika panga na shoka ndani ya nyumba yake akitaka kumkatakata mkewe na wanawe na dirisha la kioo linaonesha wazi haya, halafu eti majirani waseme si ruhusa kwao kuingilia mambo ya ndani ya baba mlevi huyu wa pombe au madaraka au uanaume wake!
Sunday, March 27, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment