Tafsiri
Mamlaka kwa mikoa ni dhana ambayohaina tofauti na dhana ya kisiasa ya madaraka mikoani. Mamlaka mkoani ni kuuachia mkoa fursa ya kuchagua viongozi wake; mkoa kulinda wakazi wake na rasilimali zao; kuwa na chombo chake cha kutunga sheria na kuwa na mkoa kuwa na mikakati na mipango yake ya kujiendeleza kijamii, kiuchumi, kiutamaduni , kisiasa na kiteknolojia.
Sababu kubwa ya kuwepo kwa haja ya mikoa inayojitawala angalau kiuchumi na kijamii ni kurudisha kwa mujibu wa katiba madaraka na mamlaka kwa wananchi pale walipo. Kihistoria, serikali kuu kwa sababu moja au nyingine ililazimika kuhodhi madaraka na mamlaka hata yale ambayo haikustahili kuwa nayo.
Enzi hizo uadilifu, uaminifu na utiifu kwa uongozi uliopo ulikuwa wa kiwango cha juu zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Mawasiliano, udhibiti na uwajibikaji, hali kadhalika, ni kitu kilichowezekana na kilichokuwa kikifanyika.
Katika miaka hii mikoa imeanza kuwa na mashaka na maamuzi ya wale wanaoongoza serikali kuu na hasa katika masuala ya ardhi, madini na uwekezaji. Wakati wakazi wa maeneo na mikoa husika wamekuwa hawaambulii chochote cha maana, viongozi wa wizara na serikali kuu wamekuwa wakifaidika na mali asili zilizoko katika mikoa ambayo wao hawakuzaliwa huko. Wazawa na wakazi wa mikoa husika wanaona kwa hiyo ipo haja ya kuweka utaratibu na muundo wa serikali utakaohakikisha kuwa rasilimali za mkoa zinafaidiwa na wakazi wake na sio kinyume cha hivyo.
Viongozi wote wa mkoa waliopo hivi sasa wanaonekana kuwajibika kwa serikali kuu na sio wakazi wa mkoa wahusika. Viongozi hawa wamekuwa kama ndio wenye mamlaka na madaraka na wananchi kuwa wasio na nguvu au uwezo wowote juu ya maisha na mustakabali wao kiuchumi na kijamii.
Mathalani, mkuu wa mkoa, awe mtu mbaya au mzuri, hachaguliwi na wananchi wa mkoa husika bali na rais. Wakazi mikoani wanaamini kwamba wakati umefika sasa kwa wao kumchagua mkuu wao wa mkoa kama wanavyochagua wabunge wao. Wanaamini hili litawafanya viongozi wa mkoa kuwajibika zaidi.
Wanataka pia serikali itambue hili na kumpa uwezo kiongozi watakaomchagua wao wenyewe. Badala ya mkuu wa mkoa wa sasa wanaamini kwamba mkoa unastahili kuwa na Waziri Mkuu wa Mkoa au Gavana wa mkoa.
Gavana huyo atapatikana ndani au nje ya bunge la mkoa, kutegemeana na upatikanaji wa mtu mwenye uwezo wa menejimenti, visheni, kipaji cha kubuni mambo mapya, kuzitumia kikamilifu rasilimali za mkoa na ustadi wa kuwa na mikakati na mipango inayowawezesha wakazi wa mkoa kufankisha kile walichoazimia kukifanya kwa wakati na kwa ufanisi na ufanifu wa hali ya juu.
Bunge la mkoa tofauti na bunge la kitaifa litakuwa sio tu na uwakilishi wa wabunge wa kawaida bali pia wa watu kulingana na makundi ya kimaslahi na wale wenye vipaji, uwezo na utaalamu ambao unaaminika unaweza kuwa mtaji kwa maendeleo ya mkoa husika. Kila kitu kitakuwa kimeelezwa katika katiba za mkoa na kanuni na taratibu za utawala wa mikoa huru kiuchumi na kijamii.
Ili kuongeza kasi ya maendeleo ya mikoa, kila mkoa utalazimika kuwa na redio, televisheni na gazeti la umma la mkoa; achilia mbali vyombo vya habari vinavyoanzishwa na vitakavyoanzishwa na wawekezaji mbalimbali toka ndani na nje ya nchi. Urahisi huu wa mawasiliano ukiambatana na ufikivu mkubwa zaidi wa simu za mkononi mkoani utaongeza kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo katika mikoa ambayo sasa haitakuwa imefungwa kwenye mkanda wa suruali ya baba au kamba za sketi ya mama kimaendeleo.
Aidha, katiba za mkoa na sheria zitakazofuatia zitailinda mikoa na ufisadi, wizi, rushwa na matumizi mabaya ya serikali kuu ya kitaifa kama inavyofanyika kwa kawaida katika nchi ambazo zinafuata mfumo wa shirikisho au muungano wa kimikoa, k.m. , Ujerumani, Urussi, Uchina, India, Brazil, Afrika Kusini na kadhalika.
Wabunge katika bunge la mkoa watalipwa mishahara kulingana na elimu na ujuzi walio nao kama wanavyolipwa wakazi wengine. Hii ina maana, kama mbunge ni mwalimu wa sekondari mwenye shahada ya kwanza, atalipwa mshahara wa mwalimu wa sekondari mwenye shahada ya kwanza. Kama ni mhadhiri wa chuo kikuu atalipwa mshahara wa mhadhiri. Na kama ni daktari wa hospitali atalipwa mshahara wa daktari. Kwa utaratibu huu wabunge wa mkoa wataenziwa kazi zao na maslahi yao yataendana na kuendelea kujiendeleza pia katika taaluma zao. Posho zitakuwa zaidi ni za kujikimu tu na hivyo kupunguza sana matumizi ya serikali katika eneo hili.
Hii ina maana kutokana na kuwepo kwa mabunge ya mkoa, bunge la kitaifa sasa, litahitaji muda mdogo tu kuzungumzia masuala ya kitaifa na kimipango. Tunaamini bunge hilo litahitaji juma moja tu kila baada ya miezi mitatu ili kufanya kazi zake na sio zaidi ya hapo. Bunge hilo jipya la taifa litakuwa ni la wawakilishi wa majimbo tu na hakuna uwakilishi wa jumuiya au wabunge wa kuteuliwa. Kwa namna hii nchi itaokoa mabilionikama sio matrilioni ya shilingi zitakazoelekezwa kwenye maendeleo ya wananchi mikoani. Aidha, kwa mantiki hii serikali ya JMT inaweza ikawa na serikali ndogo yenye mawaziri wasiozidi 14 tu ( Angalia makala za nyuma kuhusu hili ).
Kwa mikoa kuwa na Waziri mkuu wa mkoa au Gavana, mikoa italazimisha kisheria kuwa na serikali ya kweli ya Muungano wa Tanzania. Mikoa itakuwa imevunjwa na kuwa Tanganyika ndogongogo zinazojitawala na kujiamulia mambo yake kama Zanzibar na SMZ zinavyofanya. Kumbuka kuna mikoa ambayo ina wakazi wengi mara mbili au hata sita ya wakazi wote wa Zanzibar. Haki katika hili itakuwa imetendeka.
Waziri Mkuu wa Mkoa au Gavana wa Mkoa atachagua mawaziri wasiozidi kumi na mbili kushughulikia hasa maeneo yenye fursa za mkoa kujiendeleza kiuchumi au kutatua kwa kasi matatizo na changamoto zinazowakabili wakazi wa mkoa husika bila ngojangoja kama inayotokea katika muundo na mfumo wa serikali wa hivi sasa.
Serikali za mikoa, mathalani, Kagera inaweza kuamua kuuza sukari yote inayozalishwa mkoani humo Burundi kama soko linaruhusu na kisha wakanunua sukari ya bei rahisi kutoka Uganda au Rwanda au nchi nyinginezo duniani.
Serikali ya mkoa wa Katavi au Rukwa inaweza kuamua kuuza mahindi yake Zambia au Malawi au Kongo kama biashara huko ni nzuri ili mradi inahakikisha wananchi wake wanabakia na akiba tosha ya chakula hadi kufikia msimu ujao iwe kwa kile walicholima au kile ambacho watanunua kutokana na faida ya kuuza mahindi yao nchi za nje. Mkoa uanaweza kujigeuza kitovu cha kudumu cha biashara ya nafaka na nchi zinazouzunguka kwa faida ya mkoa na wakazi wake.
Mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga, Mara, Ruvuma, Tabora, Ruvuma, Mbeya, Iringa na kadhalika inaweza ikapitia upya mkataba wa uchimbaji madini na kuhakikisha wakazi kwenye maeneo husika sio tu wanalipwa malipo halali bali wanakuwa na hisa katika makampuni ya uchimbaji madini. Wachimbaji waliopo wakizira, watatafutwa wawekezaji toka Uchina, Korea, Japani, Urussi na kwingineko kuwanunua na kisha wawekezaji upya wakaendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria mpya za mkoa husika.
Kwa kuwa mkoa utakuwa huru kiuchumi na kijamii, mkoa utaruhusiwa kuingia katika ushirikiano na nchi, makampuni na watu ndani na nje ya nchi kwa maendeleo ya mkoa na wakazi wake. Hii ina maana pia kuwa mikoa itakuwa na haki ya kupokea misaada toka nchi na watu mbalimbali duniani kwa maendeleo yake na wakazi wake.
Ieleweke ya kwamba mikoa huru kiuchumi, kijamii na kisiasa sio lazima iwe inatawaliwa na chama tawala kama chama tawala hakikushinda katika mkoa huo. Chama kinachoshinda mkoani ndicho kitakachounda serikali ya mkoa na sio vinginevyo. Hili litaruhusu kuwepo ushindani wa kweli wa kisiasa, kuchumi na kijamii kwa maendeleo makubwa zaidi ya wakazi wa mikoa bila maendeleo yao kuchafuliwa na siasa na sera mbovu za serikali kuu.
Faida kubwa ya muundo na mfumo huu wa kisiasa ni kwamba utakuwa ni chuo kikuu kwa viongozi wa baadaye wa nchi. Anayekuja kuwa waziri mkuu baada ya kuwa waziri mkuu wa mkoa, hatakuwa na mengi mapya ya kujfunza kama ilivyo kwa wanaoteuliwa kwa nafasi hiyo hivi leo. Kadhalika mawaziri wa mikoa watachangia sio haba kuwa na mawaziri ambao wanajua uwaziri ni nini na hawaendi kujifunza uwaziri katika serikali kuu na kuwapotezea wananchi muda na maendeleo yao.
KUNA wanaoogopa eti tukiwa na serikali za shirikisho tutavunja umoja na amani yetu. Kabla ya kukubaliana au kutofautiana na watu wenye mawazo kama hayo hebu tujiulize na kujaribu kujibu maswali yafuatayo:
. Hivi dunia leo sio inalazimisha watu wa maeneo na jamii ndogo kujitawala ?
. Je, jamii ndogo na maeneo madodo hayastahili kulinda na kuzitumia rasilimali zao kwa faida yao kwanza kabla ya watu wengine?
. Hivi serikali kuu zinakuwa na uchungu na uzalendo wa kutosha kuhusu maeneo na jamii ndogo au kuna unafiki na ubinafsi?
. Ni jamii zinazodhulumiwa au serikali kuu inayowadhulumu ndiyo watavunja amani na umoja wa nchi?
. Je, jamii na maeneo madogo yanaridhika yale yanayokipata toka serikali kuu?
. Je, jamii na maeneo madogo yanaridhika na jinsi misaada toka nje inavyotumika?
. Je, kiuchumi jamii na maeneo madogo yatafaidika zaidi kwa kuwa na serikali zao au kwa kutegemea serikali kuu?
. Je, jamii na maeneo madogo yatafanya biashara nzuri zaidi na nchi jirani au ni taifa zima ndilo linaloweza haya?
. Je, matatizo yanayokabili jamii na eneo dogo yatamalizwa haraka zaidi na serikali ndogo za kijamii au kieneo au serikali kuu?
. Je, fursa za kiuchumi zilizopo mkoani au jamii na eneo dogo zinaweza kutumika haraka zaidi kwa kuwa na serikali ya mkoa au kwa kusubiri serikali kuu ikumbuke mkoa husika ?
. Je, kijamii ni rahisi kujenga nyumba kwa kila familia kwa jamii na eneo dogo au kujenga nyumba kwa kila familia kwa nchi nzima?
. Ni mikoa mingapi yenye vyuo na vyuo vikuu Tanzania hivi leo?
. Ni mikoa mingapi yenye redio ya umma au binafsi ya mkoa inayosikika mkoa mzima hivi leo?
. Ni mikoa mingapi yenye gazeti la umma au binafsi la mkoa linalouzwa mkoa mzima hivi leo?
. Ni mikoa mingapi yenye televisheni ya umma au binafsi ya mkoa inayoonekana mkoa mzima hivi leo?
. Ni mkoa gani unaojua ni mazao au bidhaa au huduma au madini a u mafuta au rasilimali nyingine inayoweza kuharakisha maendeleo ya mkoa kuliko ilivyo hivi sasa?
. Je, mikoa ikiwa huru kiuchumi na kijamii itaweza kujitosheleza katika masuala ya maji, umeme, nishati na huduma mbalimbali za jamii muhimu?
. Je mikoa ambayo vyama vya upinzani vina wabunge au wawakilishi wengi ingetawaliwa na vyama hivyo maendeleo yao yangekuwa duni kama ilivyo hivi sasa ?
Haya ni maswali muhimu kujiuliza, kutafakari na kuyajibu ili kuona kwanini katika nyakati zetu serikali huru za mikoa ni kitu cha lazima na kisichoepukika. Ila ni lazima wananchi wafunguliwe macho kwanza na wao wenyewe waone faida na hasara za kukosa mikoa iliyo huru kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Friday, December 16, 2011
Subscribe to:
Posts (Atom)
