Friday, July 3, 2009

Furaha yangu

1.
Furaha yangu mwenzangu, nawe kushirikiana,
Niwe wako uwe wangu, si usiku si mchana,
Mzigo wako ni wangu, tutakujapokezana,
Siue furaha yangu, kuniacha peke yangu.

2.
Furaha yangu daima, mimi na wewe kuteta,
Waziwazi kuyasema, ya furaha na kujuta,
Maovu pia na mema, kuyamwaga na kuchota,
Siue furaha yangu, kuniacha peke yangu.

3.
Furaha yangu pekee, niwe lako kimbilio,
Itokeapo ujikwae, mbiombio kwangu njoo,
Usijali niegemee, uchechemeapo leo,
Siue furaha yangu, kuniacha peke yangu.

4.
Furaha yangu 'kilia, nifute machozi yako,
Kwa hariri kitambaa, utulie wajihi wako,
Kisha nitakupepea, zirudi pumzi zako,
Siue furaha yangu, kuniacha peke yangu.

5.
Furaha yangu ujue, sisi kama wana pacha,
Nataka ulitambue, wewe si wa kuniacha,
Ni ubavu uning'oe, kweli hai utaniacha ?
Siue furaha yangu, kuniacha peke yangu.

6.
Jasho lako marashi, langu kwako Jasmini,
Bashasha yako nakishi, Utani wangu afueni,
Tomasa yako ucheshi, Papasa yangu hisani,
Siue furaha yangu, kuniacha peke yangu.

7.
Ukichoka kiti chako,kitakachokubembeleza,
Pale ukasirikako, hasira nitaimaliza,
Huko uhangaiko, mie nitakupumzisha,
Siue furaha yangu, Kuniacha peke yangu.

8.
Njoo tuanze chini, tupande juu pamoya,
Nipe hawa masikini, tajiri nitakufanya,
Njoo uwe yangu feni, twenzetu hadi Ulaya,
Usiue furaha yangu, Kuniacha peke yangu.

9.
Nisife na akili hizi, bila kuachia wanao,
Ukazaa na machizi, Na vichwani hamnao,
Akili kitu azizi, Chagua sana uzao,
Usiue furaha yangu, kuniacha peke yangu.

10.
Tamati ninafikia, yakini nikitegemea,
Ujumbe umekufikia, nawe yangu umeelewa,
Mikonowe imetwaa, moyoni mwangu furaha,
Nani wa kunirudishia. kama sio wewe dia ?

Tuesday, June 30, 2009

Mwili na akili

Ukitanguliza mwili,
Nyuma ifate akili,
Hupati pendo la kweli,
Na roho hugawanyika!

Siukimbilii mwili,
Najua wake muhali,
Umkutapo baradhuli,
Pendo sumu hugeuka.

Naitafuta akili,
Tena kwa hali na mali,
Sio kwayo taamuli,
Bali kwayo tajamali.

Naitafuta kauli,
Murua tena sahili,
Itoayo afadhali,
Mashaka yanaponifika.

Nazitafuta dalili,
Za bashasha na adili,
Na pendo bila ubahili,
Nikatakwa, nikataka.

Nazitafuta amali,
Za majibu na maswali,
Kuzijenga zetu hali,
Toka chini, juu tukafika.

Naitafuta asali,
Toka nyuki wa asili,
Na sio ile ya kunakili,
Nilambe na kutosheka!

Sitaki nafuu ghali,
Nikajabwagwa chali,
Bila kisomo cha Laili,
Nyota njema ikishuka.

Sitaki cha bilkuli,
Ima fa ima kivuli,
Cha mshaka ya samli,
Kupika kisichopikika.

Sitaki kiwiliwili,
Nataka yako akili,
Inifanye mie kamili,
Kiroho pia kimwili!

Harufu ya Jasmini

Linasifiwa waridi, tena sana duniani,
Nani hili kulikaidi, asiyelisifu nani?
Ni wachache kwa idadi,waridi wasothamini,
Mfano mie kusifu, harufu ya Jasmini.

Kulienzi sina budi,waridi rangize shani,
Hautimii mradi, kutosifu Jasmini,
Kwalo mimi shahidi, kwa macho na moyoni,
Nd'o kisa mie kusifu, ua lake Jasmini!

Ua hili maridadi, kalijalia Manani,
Linatia ubaridi, joto ukilibaini,
Na lapandisha mdadi, baridi ikikuhaini,
Hakika yanipendeza, harufu ya Jasmini.

Sio wengi hulifaidi, linapenda faraghani,
Mchana katu abadi, harufuye huioni,
Ila usiku taradadi, nje, uani na chumbani,
Utaisikia kokoe, harufu ya Jasmini.

Chumbani bure waridi, ni ndogo yake thamani,
Kitandani hufaidi, ila uwe na Jasmini,
Huba huwa kama Iddi, sikuzote u rahani,
Usingizi laini kwa harufu ya Jasmini!