Ajali, fidia na Mtanzania
NI wakati kama huu wa ajali ndipo Watanzania wengi wanapotambua kwamba sio tu hawana kinga dhidi ya ajali lakini pia baada ya ajali kutokea wanaweza wasipate msaada wa maana kuendelea na maisha yao.
Watetezi wa umma, hata hivyo, huu ndio wakati wa kuingilia kati na kujaribu kuubadili mfumo uliopo ili uangalie pia maslahi ya wanyonge na wasio nacho katika jamii.
Wenye nacho na walioko madarakani hawana sababu ya kuwapenda wanaotetea maslahi ya walio wengi. Lakini vile vile watetezi wa umma hawana sababu ya kuwaogopa wenye nacho na walioko madarakani katika kutetea haki za wanyonge. Huu ni wito na sio kazi ya kutafuta cheo au ukubwa au utajiri.
Mfumo uliopo
Mfumo wa bima na fidia uliopo hivi sasa umejengwa katika mihimili ya kuwasaidia walionacho na wakubwa.
Mnyonge hana nafasi katika mfumo huu. Ukitaka ushahidi nenda kawahoji walioathirika na ajali kama zile za MV Bukoba, ajali mbalimbali za mabasi na majini nchini kwa miaka tuseme saba tu iliyopita. Kadhalika kawahoji watu wa Merelani kwa matukio mawili matatu na usikie fidia waliyopata.
Ukitoka hapo kaangalie upande wa pili na mahesabu ya mashirika ya bima kuhusu ajali zilizowahusu walionacho na wenye nchi.
Baada ya maswali na udadisi huo utagundua kuwa mfumo wa bima na fidia upo kwa ajili ya tabaka fulani tu katika jamii na sio kwa umma wote.
Swali linakuja. Je, huu ndio mfumo nchi kama yetu yenye asili ya kijamaa unaostahili kuwa nao? Kweli kuna sababu ya kuruhusu mfumo huu uendelee au kwa maneno mengine kwanini mfumo huu bado unalindwa? Je, maslahi ya wengi yakiangaliwa yale ya wachache yatapotea?
Kama mabadiliko yanahitajika, je, nchi hii inahitaji mfumo gani wa bima na fidia kwa faida ya umma?
Mashirika ya umma na fidia
Eti kwa kuwa TANESCO, DAWASA, TRC, ATC na mashirika mengine enzi hizo yalikuwa ya umma ilikuwa haiyumkiniki mtu kufidiwa kitu.
Si mnakumbuka wale ambao friji, TV, redio na vyombo vyenu vingine vya nyumbani vilivyoharibiwa na umeme wa TANESCO? Wangapi kati yenu walilipwa fidia?
Treni hadi leo ikisababisha ajali hata kama ni kwa uzembe wa shirika husika eti ni wewe mpita njia ndiye unayewajibika na sio wao. Makubwa haya jama.
Pamoja na haya yote ni kwamba hakuna shirika linalowajibishwa hapa nchini hivi sasa kwa kushindwa kutimiza upande wake wa mkataba iwe ni kutoa huduma au kuuza bidhaa mbovu kwa wananchi.
Mtanzania kwa kifupi hana haki kabisa dhidi ya mashirika yanayotakiwa kumpatia bidhaa au huduma. Yakimpatia huduma au bidhaa safi na bora sawa. Yakitoa huduma ovyo na bidhaa zilizooza sawa! Hataweza kuyashtaki na kuambulia chochote katika mfumo uliopo.
Sheria na udhibiti wa uzembe
Ieleweke kuwa kazi mojawapo ya sheria na katiba ya nchi yoyote ile ni kulinda raia na mali zao. Sheria na katiba inayoshindwa kufanya hili inakuwa na walakini.
Vyombo vya sheria vina jukumu sio tu la kuona kuna sheria fulani lakini kuhakikisha kuwa sheria hizo zinakwenda na wakati na zinatimiza yale ambayo katika macho ya jamii ni haki na wajibu.
Mojawapo kati ya mambo hayo ni kuona kuwa raia na wasio raia wanapata fidia maridhawa pale wanapofikwa na janga lolote nyumbani, kazini au safarini. Jingine ni kuhakikisha kuwa sheria inatumika kama kinga dhidi ya ulegevu na uzembe unaoweza kusababisha kifo au mtu kuwa kilema maisha yake yote.
Kifo kinapomkuta, kwa mfano, msafiri wa treni ina maana kuna familia na hasa watoto watakaokosa baba au mama. Je, ni nani atawalea hawa? Sheria ina haki kunyamaza kuhusu hili?
Jamaa huyo huyo anaweza akawa pia alikuwa akitegemewa na wazazi wake-baba, mama na pengine kwa mila zetu za Kiafrika-babu na bibi. Na pengine baba huyo ndio wale jamaa waliostaafishwa na jumuia ya Afrika Mashariki na kulipwa sh. 320 kama mafao. Ni nani atawatunza wazee hawa? Sheria inaliona hili?
Katika kujadili masuala kama haya ni wazi kuwa hatma ya yote itaonekana kuwa Tanzania haina mfumo wa bima na fidia unaoweza kuwalinda Watanzania walio wengi wakati wa maafa ya aina yoyote ile.
Kwa mantiki hii kazi iliyobaki ni kwa vyombo vya sheria vikipata changamoto kutoka vikundi vya hiari na taasisi nyingine zinazotetea maslahi ya wanyonge kuhakikisha nchi inakuwa na sheria zitakazowesha kuwa na jamii na uchumi usiotetereshwa na maafa na majanga.
Aidha ni muhimu kuwa na mfumo unaolinda nchi na watu wake dhidi ya uzembe wa wenye mali.
Kwa mfano, hivi kuna ugumu gani kuwa na sheria itakayotaka familia ifidiwe shilingi milioni 5 -10 kwa kupoteza jamaa yao? Fidia ya milioni 1-2 kwa mtu kuvunjika mguu?
Je, kwa namna hii kuna dereva, meneja au mwenye gari au chombo cha usafiri atakayecheza na maisha ya watu.
Kwa mantiki hii kama inaonekana uzembe ulifanyika na kisha kusababisha ajali basi fidia inaweza kuwa mara mbili au zaidi ya hapo.
Fidia ni njia pekee inayoweza kuwasaidia watoto na wajukuu wanaobaki bila mtafuta riziki wake. Fidia ni njia pekee inayoweza kuwasaidia wazazi waliozeeka wanaoachwa bila mtu wa kuwasaidia.
Fidia ni njia pekee inayoweza kumsaidia mtu anayefanywa kilema katika ajali fulani aweze kujitegemea kimaisha. Kukiwa na mfumo wa bima na fidia unaowezesha hayo hapo juu ni dhahiri kuwa nchi itanufaika pia kiuchumi.
Kutokana na kuzungusha upya pato la nchi linalokwenda aghalabu zaidi kwa wachache basi kunakuwa na msukumo mkubwa zaidi wa uzalishaji mali utakaonufaisha sehemu mpya na sio zile za asili tu.
Ulaya, Marekani na fidia
Ingawa Tanzania haiwezi kuwa kama Marekani na Ulaya katika masuala ya bima na fidia ni muhimu hata hivyo kujifunza falsafa iliyowafanya waheshimu na kuendeleza mfumo wa sheria unaowanufaisha watu wanaoathirika kwa maafa mbalimbali.
Anayeumia kidole kazini, kwa mfano, huko Ulaya au Marekani anaweza akajikuta ametajirika fumba na kufumbua.
Watoto na wazazi wanaowategemea wengine huwa hawaambulii patupu wanapompoteza mtafutaji wao katika ajali iliyosababishwa na uzembe wa wengine na pengine hata maafa yalio nje ya kazi za binadamu. Kwa mfano moto unaochanja mbuga huko Texas hivi sasa. Hakuna aliyeusababisha lakini wote waliopoteza makazi yao huko wanaweza kuja kufidiwa kwa namna moja au nyingine.
Huu ni mfumo kwa kweli unaowapa watu imani na nchi yao, wananchi wenzao na serikali yao. Nadharia yake sio ngeni katika masikio yetu. Miaka kadhaa iliyopita Mwalimu J.K. Nyerere katika Ujamaa wa Kiafrika alilizungumzia hili.
Kama jamii ya wakati huo iliweza kumpa msaada mtu na kumwezesha kurejea maisha yake ya zamani kwa kiasi fulani kwanini leo nchi na taasisi zake za fedha ishindwe kuiga mfano huu unaotokana na mila na utamaduni wetu?
Bima ya umma
Ni dhahiri kuwa hakuna mwenye basi, mwenye meli au ndege atakayesumbuliwa na suala hili la bima na fidia kwa wanaofikwa na balaa wakisafiri katika vyombo vyao.
Huu ndio ukweli wa binadamu na mali yake. Hujali mali yake zaidi kuliko maisha ya watu wengine. Kama ndivyo, je, sio jukumu la serikali ya watu kuingilia kati hapa.
Ninapendekeza kuwa kwa kila abiria anayesafiri na basi, meli, ndege serikali itoze sh. 100 tu kuanzisha mfuko wa Bima dhidi ya ajali za vyombo vya usafiri.
Tusiwasumbue wenye vyombo vya usafiri katika hili. Njia rahisi ni kukadiria kuwa kwa mwezi chombo fulani, mathalan, treni ya TRC inabeba abiria elfu ishirini na TRC wanastahili kulipa shilingi laki mbili kwa mwezi. Iwe vivyo hivyo kwa mabasi na ndege.
Wakati wa fidia mwenye chombo atalipa nusu ya fidia na nusu iliyobaki italipwa na mfuko huu kwa fidia yoyote itakayoamuliwa. Kazi kwenu wawakilishi wa umma Dodoma kuchambua pendekezo hili.
Tume za maafa na faida zake
Vyombo vya habari ndani na nje za nchi inaelekea havioni umuhimu wa Tume zinazoanzishwa kuchunguza maafa kama haya ya juzi na jana. Yaani Merelani na Dodoma. Kwa upande mwingine, hata hivyo, kama Tume ya Ajali ya Treni Dodoma itashughulikia na masuala yatakayochangia pia kuubadili mfumo wa bima na fidia kama njia ya kudhibiti ajali zinazotokana na uzembe ingefaa iungwe mkono. Vinginevyo, fedha itakayoliwa na wajumbe hao wapewe wafiwa na mejeruhi.
Sunday, March 27, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment