Sunday, February 6, 2011

Ujambazi na mfumo wa kijamii-uchumi

Tuanze na mchapo. Huko Uganda walimu wa shule za msingi siku moja walijikuta wanafanya mitihani ile ile waliyokuwa wakiwapa wanafunzi wao. Wengi wao walifeli. Serikali ikawafukuza kazi.
Huko huko Uganda mamia ya askari polisi wanaodaiwa awali walikuwa walevi hivi sasa wanapigishwa kwata la nguvu. Atakayeshindwa mazoezi hayo, yakiwemo, kukimbia, kubeba mizigo mizito na kadhalika atakuwa kajifukuzisha kazi.

Na huko Uganda tena, hivi sasa bila angalau digrii moja sahau kuwa mwandishi wa habari maisha.

Wenzetu wamecharuka. Wanataka kama mtu ameajiriwa kwa kazi fulani basi kweli si tu aagizwe ifanyike lakini aonekane akiifanya kazi hiyo.
Nchi haiwezi kuwa na maendeleo ya kweli, Waganda wanaamini, kama una wababaishaji sehemu za kazi muhimu kama una wababaishaji na sio wachapa kazi.

Katika mtiririko wa haya yote Waganda wanayoyafanya inaelekea wana mkakati fulani wa kuijenga jamii yao iwe imara kiuchumi na kijamii.

Kwanini ujambazi unakuwa tishio?
Tuache utani. Ujambazi sasa ni tishio kwa biashara na makampuni nchini. Kila mtunza-fedha au mbebaji fedha wa kampuni au taasisi nyingine daima yuko katika hofu ya kutolewa roho.

Hvi leo jamaa hawa wanaweza wakaibuikia sehemu yoyote wakafanya vitu vyao na wakaondoka na asitokee polisi yeyote kwa kitambo kiasi. Katika hali kama hii kila mtu anajiona ni yeye na lwake. Wakati ameanza kupoteza imani kabisa na jeshi lao la polisi.

Kwa kifupi watu wamekata tamaa na wanaamini kuwa unaweza kushambuliwa wakati wowote na usipate msaada. Na hii ndio sababu ya ujambazi kuwa sasa ni tishio la kitaifa linalochipukia.

Hata hivyo, wanasiasa, bado wamekaa kimya na hakuna anayezungumzia jambo hili kwa uzito unaotakiwa. Pengine wakiamini kuwa unaweza kulifumbia macho nalo likapita. Lakini hili kwa nionavyo mimi sio jambo la kupita. Ni kitu tutakachokuwa nacho siku zote kama viile tutakavyokuwa na maskini sikuzote.

Vita vinaweza kuliyumbisha taifa. Ujambazi ukikithiri hulisambaratisha taifa. Na ukitaka kuiona mifano nenda Somalia.

Kama ndivyo basi huu ni wakati wa viongozi nchini kujiuliza maswali mengi kadri iwezekanavyo ili kupata majibu sahihi na mikakati ya kuitumia ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili.

Maswali ya kujiuliza
Ingawa mimi sio bingwa wa mausala ya sayansi ya jamii, hata hivyo, nina maswali kadhaa ya kuuliza ambayo natarajia yakipata majibu yatatupa mwanga juu ya tatizo linalotukabili.

Ni kwa kiasi gani mpito toka Ujamaa kuingia siasa isiyo na jina (Ubepari usiotajwa) hapa nchini unachangia kuongezeka kwa wimbi la ujambazi wa kutumia silaha.

Wakati ule tunavaa Chou-en-lai inaelekea wote tulijiona kuwa ni sawa. Kwa malezi ya Baba wa Taifa kila mtoto alijiona hana tofauti na mtoto mwenzake. Na hili alilifanya kuanzia nyumbani kwake mwenyewe.

Hivi leo mtoto wa muuza samaki feri ambaye kuambulia elfu moja ni kazi akiwa rafiki wa mtoto wa mwanasiasa au meneja ambaye baba yake humpa laki moja atumie kwa siku ni binadamu gani ataacha kuwa na maswali ya kujiuliza na yeye afanye nini awe kama huyu wa pili? Hebu fikiri!

Achilia mbali watoto leo wazazi wanashindana kwa wingi wa majumba, magari, nguo na kila aina ya vikorokoro. Wazazi wengine wanona. Hawana uwezo na wanabaki kumezea mate na matumbo kuwanguruma. Watoto wao siku ya siku wanapofanya vitu vyao dhidi ya hao ‘wanaoringa’ mzazi atakataa nyumba mpya anayopewa? Mark II na dereva ikija nyumbani na kuambiwa ni yake aitumie jinsi anavyotaka? Mzazi atasema nini? Atamlaumu mwanae? Amelogwa? Achekwe?

Katika hali tuliyo nayo sasa baadhi ya wazazi wanaowaona watoto wao ‘wezi’ kuwa ni kina Robbin Hood wa miaka yetu. Kama humjui jamaa huyu basi nikuelezee kwa kifupi. Huyu alikuwa ni jambazi maarufu wa Kiingereza ambaye alikuwa anawaibia matajiri na kuwapa maskini. Unaona hiyo?

Fursa finyu
Katika miji yetu mbalimbali kumezuka ubia usio mtakatifu kati ya wanasiasa-wafanyabiashara- na watumishi wa serikali kuwapora vijana mabanda ya biashara; viwanja vya michezo; tenda; vibali na kila aina ya fursa ambayo ingelimuwezesha kijana kujiendeshea maisha yake na pengine kutajirika bila kutumia njia haramu. Sasa tujiulize kama mtu ananyimwa fursa halali za kuukata afanye nini. Ashukuru. Atoe Allhamdullilahi kisha asahau?

Elimu bila kazi
Mamia ya vijana wanaomaliza shule ndani na nje ya nchi hivi sasa hawapati kazi. Ni nini kitakachotokea hapa. Tumewahi kujiuliza swali hili? Biblia inatuambia: ‘mikono isiyo na kazi, shetana ataitafutia kazi bila wasiwasi wowote!’
Watu waliosoma hawawezi kuwa sawa na vibaka. Hawa ni watu wenye akili eti. Wengine wamesomea udaktari wa mifugo; wengine wahandisi; wengine wanasayansi na kadhalika. Na ole wako wakikutana watu zaidi ya wawili kama hawa mambo wanayoweza kuyafanya ni ya ajabu. Tatizo ni pale ambapo wanachokifanya ni biashara ya uvunjaji sheria. Nani ataona ndani?

Sheria zinazopendelea
Vijana wa Kitanzania sio vipofu, sio viziwi. Wanaona kila siku, wanasikia kila kitu. Na aghalabu wanajua kuwa kuna seti mbili za sheria. Moja ni ile ya walalahoi, na nyingine ni ile ya vigogo na vizito. Mlalahoi ama ni kuvunjiwa vyombo vyake na kupoteza mtaji wake wa kimaskini au ni kulipa faini au ni kwenda jela. Sheria hiyo hiyo kwa upande wa vizito ni kuhakikisha mali yao inalindwa kwa jino na ukucha wa polisi wetu wenyewe; kutokulipa faini na kutokwenda jela hata wakifanya kosa gani.

Katika hali kama hii inafaa tuwaulize wanasayansi-jamii je watu na hasa vijana wenye wingi wa jazba na pupa ya maisha watalichulia hili suala namna gani. Ni vyema kufuata sheria na kunyanyasika hata pale wewe unapostahili kuwa ndiye mdhulumiwa au mtu aliyeonewa. Au ni kuvunja sheria na kuhakikisha vyombo vya sheria havikubambi hata siku moja? Na wakikuzingira basi uchukue njia ya Mkwawa?

Hili linaendana na haki kununuliwa. Hivi sasa kwa sababu moja au nyingine mtu mwenye fedha au mwanasiasa anaweza akakukosea. Lakini badala ya wewe uliyekosewa kulipwa fidia ukajikuta wewe ndiye unayedaiwa kama sio kwenda lupango kabisa.

Katika kijiji ambacho sitaki kukitaja jina visa kama hivi vimetokea. Na watu wasiokuwa na hatia, na hasa vijana, labda kwa sababu ya kugombea mwanamke na kumshinda tajiri anajishtukia yuko ndani na kosa haliju. Hili linafanyika vijijini, ninaamini, karibu vyote Tanzania na sio hicho kimoja tu nilichotolea mfano wake.

Njaa na umaskini
Hapana haja ya kusema mengi kuhusu hili. Maana ni wazi kuwa kuna njaa na umaskini wa kutisha katika jeshi letu la polisi. Hatusemi wakimwagia fedha basi ujambazi utakwisha. La, hasha. Tuwaachie wanasayansi-jamii watupe majibu ya swali hili: je, mishahara midogo na umaskini wa polisi unachangia kwa kiasi gani matatizo ya usalama nchini? Na kwa kiasi gani hili linachangia haki ya mtu kuuzwa au kununuliwa?

Uharamia na ushindani
Pengine ni muhimu kwa wanasayansi-jamii kuuliza pia kama ushindani ambao ni matokeo ya soko huru nchini unaweza kusababisha uharamia wa kibiashara? Je, mfanyabiashara fulani anaweza kukodi majambazi ili wapore kutoka kwa mshindani wake na hivyo kumkomesha mwenzie? Au pale biashara au kampuni fulani zinapopewa upendeleo na mamlaka na wengine kutaka kujibu mapigo?

Je, watu wanaofukuzwa kazi ovyo katika makampuni na taasisi siku hizi wanaweza kutumbukiwa na nyongo na kuamua kula sahani moja na majambazi ili kuwakomesha waajiri wao?

Kisaikolojia hasa ni kitu gani kinachomfanya mtu kudiriki kutoa roho ya mwenzie na pengine mtu anayemjua kwa sababu ya shilingi million 10, 30 au hata 100?

Elimu, uwezo na vifaa vya polisi
Aidha katika hili ni muhimu kujiuliza kama elimu waliyo nayo polisi waliofaa kulinda usalama wakati wa siasa ya ujamaa kama inatosha kulinda usalama katika enzi za ubepari na ushindani?

Wananchi wengi wanaamini kuwa polisi wetu wana elimu duni na hawawezi kabisa kukabiliana na hali inayojitokeza sasa. Hawa, inadaiwa, ni watu waliofundishwa kutumia zaidi nguvu na sio akili. Kadhalika mbele ya mitandao kama ile ya simu za mikononi na kompyuta ni rahisi polisi wetu ‘kuchengenywa’ na wasijue chochote kinachoendelea. Maana ni polis wangapi wenye simu za mkononi au wanaojua kutumia kompyuta?

Mfumo unaofaa
Ni dhahiri ujamaa ulikuwa una kasoro nyingi. Kadhalika ndivyo ilivyo kwa ubepari. Wenzetu katika nchi za Scandinavia walitambua hili miaka kadhaa iliyopita. Wao hawafuati ujamaa moja kwa moja, wala hawafuati ubepari kichwa na miguu. Wamebuni siasa inayoitwa ujamaa-wa-kidemokrasia. Mfumo unaomruhusu kila mtu kutajirika kwa kadri ya uwezo wake, lakni wakati huohuo hauruhusu mtu kufa njaa au kukosa kabisa eti ili fulani tu atajirike. Huu ni wakti muafaka wa vyama vya siasa kupitia siasa za nchi hizo na kuona ni mazuri gani tunayoweza kuyaiga kama sehemu ya mapambano yetu ya muda mrefu dhidi ya uvunjaji sheria nchini mwetu. Bila shaka majibu yoyote yatakayopatikana hapa yatalazimu kuibadili katiba ya nchi na vyama vyetu. Maana badala ya maneno ujamaa na kujitegemea lazima pawe na maneno yasemayo kuwa nchi yetu ni nchi inayofuata ujamaa-wa-kidemokrasia.(Ujaki) Kwani mfumo huu utawapiga jeki wasionacho! Aidha mfumo huu si mgeni hapa nchini. Ulikuwepo Zanzibar enzi za marehemu Karume. Wakati Zanzibar ilipokuwa haina wizi, umalaya, madawa ya kulevya na uhalifu mwingine ulipo hivi sasa. Mwenzetu alijua anachokifanya, je sisi tunajua tunachokifanya?

Mfumo upi wa kiuchumi na kisiasa Tanzania

KARNE ya ishirini ilishuhudia mataifa duniani yakikigawanyika na aghalabu tofauti zao zimetokana na mifumo tofauti ya uchumi kila nchi iliyoamua kufuata.

Toka ukomunisti au ujamaa uliposambaratika huko Urusi na Ulaya ya Mashariki kuna wanaodhani kuwa tofauti hizi zimefikia kikomo.

Lakini tunaweza kufanya makosa tukifanya hivyo. Ikumbukwe kuwa katika miaka ya 1930 wengi waliamini kuwa ubepari umefeli na palihitajika mfumo mwingine wa kiuchumi.

Waliofikiri hivyo waliumbuliwa. Baada ya miaka michache tu ubepari ulirudi na nguvu mpya ingawa ulitofautiana kwa kiasi kikubwa na ule ubepari uliotangalia.

Ubepari umevuka mitihani kadhaa kwa ushindi mkubwa. Lakini leo tena ubepari unakutana na mitihani mingine.

Kuna wanaoamini kuwa mfuko
wa soko huria, himaya za kitaifa na dini hivi leo zinashindwa kukubaliana na matatizo yaliyoko mbele yake.

Matatizo hayo ni pamoja na umasikini, maradhi, ujinga na vita kati ya nchi na nchi na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwaka 1997 ilionekana kwa wengi kuwa ujamaa umeshindwa lakini kama watu wa 1930 walivyofanya makosa kusema kuwa ubepari umeshindwa dalili zimeanza kujitokeza kuwa hilo nalo pia ni kosa.

Kufikia mwaka 2002 ilikuwa ni dhahiri kuwa nchi iliyobebea katika siasa ya ubepari-Marekani na mama yake Uingereza ina matatizo kutokana na mfumo wake wa kibepari.

Kwa bahati mbaya viongozi wa sasa wa Marekani na Uingereza wanaamini kuwa matatizo hayako ndani kwao bali yako nje. Kwa hivyo wameanza kusaka wachawi wao nje, kwanza alikuwa Osama, kisha Iraq, kesho Iran, Korea Kaskazini na keshokutwa sijuia atakuwa nani.

Lakini kinachoonekana ni kuwa ubepari kwa kutegemea mno unyonyaji hauwezi kupona bila kuwepo watu na mataifa ya kunyonya.

Hii ndio sababu iliyoifanya Uingereza na Ufaransa kuwafanya wengine watumwa wao kupitia ukoloni mkongwe.

Na ni sababu kama hiyo pia iliyowafanya Wamarekani kuwatawala Amerika Kusini na pale Wananchi wa nchi husika walipokataa kutawaliwa basi nchi hizi za kibepari zilizua zahama za kila aina ili tu kuonyesha kuwa wengine hawawezi kujitawala ila ni wao tu wanaojua kujitawala.

Leo Marekani ya Kusini imeanza kuamka tena. Inauliza kwanini mambo yao yasimamiwe na Marekani.

Marekani imeanza kuanja mbali. Na ni Afrika tu ambayo haijafikwa bado na nuksi ya kuwepo kwa Wamarekani ndani yake (ingawa huko Angola na Kongo) walikwishaonjwa kidogo.

Damu iliyomwagika Marekani Kusini na kati kwa kiasi kikubwa inalia na Wamarekani.

Nchi hiyo ilipojiingiza pia Mashariki ya mbali ndio mabalaa yakaanza huko, kumbuka China, Korea, Vietnam, Ufilipino na kwingineko.

Hivi sasa nchi hiyo kwa kuruhusiwa na nchi za Kiarabu na baadhi ya nchi za Kiafrika kuweka makambi ya kijeshi katika nchi hizo na kuanza kuwakoroga Waarabu na Waafrika kisiasa na kiuchumi wengi wanaamini mikosi ya Vietnam na Marekani ya Kusini sasa inahamia katika nchi za Kiarabu na Kiafrika.

Ni wajibu wa dunia kuielimisha Marekani kuwa siasa zake za kibabe na unyonyaji wake uliokithiri utaifikisha dunia pabaya. Hakuna mtu au nchi inayoweza kuishi kwa kukopa au kutegemea jasho na rasilimali za wengine. Lakini hiki ndicho hasa kinachofanywa na mabepari.

Katika hali kama hii ambayo kama hadithi ya Mbweha na Mwanakondoo mabepari huwasingizia hata watoto kuwa ndio wanaochafua maji yanayotiririka tokea kule wao waliko ni vema kujiuliza kama kweli ubepari ndio mfumo wa siku zijazo?

Kweli mfumo wa Kisovieti au wa kijamaa ulikuwa na matatizo yake. Lakini tumekaa na kujiuliza matatizo hayao yalikuwa nini?

Mjadala kuhusu mfumo upi wa kiuchumi na kisiasa ambao nchi kama yetu unatakiwa kuufuata ili tuwe na jamii na utawala bora sio mjadala wa kuukwepa. Na viongozi wa kweli katika jamii yaani wafanyabiashara na wazalishaji mali wengine wanstahili kubeba gharama za kuona mjadala huu juu ya hatima ya nchi na siasa zake unafanyika mara kwa mara.

Mijadala kuhusu mfumo upi wa kiuchumi na kisiasa unafaa kufuatwa aghalabu huegemezwa juu ya mifumo mbalimbali iliyopo na kujaribu kuanisha na kuchagua kipi kinachofaa ili kuijenga jamii husika bila kuwepo migogoro inayoweza kuisambaratisha jamii husika.

Katika kufanya uchambuzi wa mifumo ya kiuchumi na kisiasa ni vyema kuanza kwa kufafanua ni kipi kilicho bora na jamii inachostahili kuwa kwa kufanya hivyo tunaweza kujifunza mengi ikiwa ni pamoja na kwanini mifumo yta kiuchumi na kisiasa wakati mwingine hushindwa kuzaa matunda yanayotegemewa.

Wanauchumi wanabainisha kuwa mifumo bora kama ilivyochaguliwa na watu mbalimbali duniani ni pamoja na ule wa soko huria (ybepari mkongwe); ubepari unaodhibitiwa na serikali; uchumi unaosimamiwa na serikali (serikali kushika hatamu); ujamaa unaoruhusu soko huru na mfumo unaoruhusu wafanyakazi kusimamia maisha na kazi zao katika jamii husika.


Ni dhahiri kuwa kila mfumo wa uchumi duniani umeshawahi kuijaribu mifumo mingine wakati fulani na matokeo yamehitilafiana kutoka nchi moja kwenda nyingine.


Ubepari mkongwe ni mfumo wa kiuchumi kama unaofuatwa na Marekani au Uingereza. Nao huwaachia watu kazi zote za uzalishaji mali na serikali huwajibika zaidi katika suala la kukusanya kodi, kutoa huduma muhimu kwa jamii kama ulinzi, ujasusi, usalama na utunzaji mazingira.

Yaani serikali hukifanya kile ambacho watu wakipewa wataumiza watu wengine au kile ambacho watu hawapendi kukifanya kwa sababu hakina faida wala tijara.

Ubepari unaosimamiwa na serikali ni mfumo unaofanana kwa kiasi kikubwa na ubepari mkongwe lakini hapa ni kuwa serikali ina ruksa ya kufanya maamuzi fulani yanayoingilia jinsi kipato kinavyopatikana na kutumika miongoni mwa Wananchi wake.

Hili hufanyika ili kupunguza makali ya ubepari katika unyonyaji na kujaribu kuleta usawa na haki fulani katika jamii kwa kutumia vyombo vya serikali.

Uchumi unaosimamiwa na seirkali sio tofauti na mfumo Tanzania uliokuwa ukifuata toka mwaka 1967 hadi Rais Mwinyi alipoingia madarakani na kuanza kuruhusu soko huria kwa kiasi fulani. Ingawa kabla yake Rais wa kwanza alisharuhusu ulegezaji masharti ya uchumi uliosimamiwa na serikali.

Uchumi wa kijamaa unaokubali soko huru kwa kiasi fulani ni mfumo unaojaribu kunufaika na mazuri ya ubepari katika uzalishaji mali na ukuzaji kipato cha jamii na taifa bila kuruhusu mabaya ya ubepari kutamalaki kila mahala katika jamii na hasa unyonyaji ulikokithiri na uvunjaji sheria wa hali ya juu.

Mifumo inayoruhusu wafanyakazi kuendesha uchumi inapatikana katika nchi ambazo vyama vya wafanyakazi vina sauti kubwa katika kuamua masuala yanayohsu uchumi na siasa za nchi. Ujerumani ina sifa hii kwa kiasi fulani ingawa kwa kiasi kikubwa ni nchi ya kibepari na kuna baadhi ya nchi kadhaa za Marekani ya Kusini na kati ambako vyama vya wafanyakazi vina mchango mkubwa katika maendeleo na amani ya nchi.

Hivi sasa kuna madai kuwa Tanzania haijui iko katika mfumo gani. Lakini wanasiasa na wanaitikadi (kama wapo) wa chama tawala na vyama vingine wameshindwa kuhamasisha majadiliano yoyote ya maana ili nchi ieleweke inatoka wapi na inakwenda wapi.

Pengine hili linatokana na ukweli kuwa ni wachache miongoni mwa wanasiasa hao wanaoelewa nadharia za uchumi muafaka kiasi cha kuzungumza kwa uhakika juu ya masula yanayohusu mifumo inayofaa kufuatwa na taifa.

Kama ndivyo, huu utakuwa mchango wangu mdogo katika kuwafungua watu macho juu ya mifumo iliyopo ili tuweze kuitafiti zaidi na kuanza kuizungumza ili tuweze kuelewashana na hatimaye kufikia muafaka kuwa Tanzania inastahili kujitmbulisha na mfumo upi.

Mfumo wa ujamaa uliwaunganisha Watanzania kwa kiasi kikubwa maana wote tulijatmbulisha nao. Kuna waliokuwa hawautaki lakini kutokana na wingi wa waliokubali ilibidi nao wajitambulishe nao hivyo hivyo ili kulinda maslahi yao ya kiuchumi na kisiasa.

Hivi sasa ni dhahiri kuwa wengi waliokuwa wajamaa jana leo ni mabepari na hawataki kabisa kusikia kitu chochote kuhusu ujamaa.

Lakini maskini hawa ni bendera fuata upepo na watu wanaotanguliza malshi yao binafsi mbele na sio maslahi ya walio wengi.

Swali linabakia pale pale kuwa ni mfumo upi wa kiuchumi na kijamii Tanzania na Watanzania kwa ujumla wao wanastahili kuuiga au kuufuata?

Ni ubepari mkongwe ili tuwe kama Marekani na Uingereza na matatizo yao ya ukubwa, kuishi kwa kunyonya nchi na watu wengine na wakikataa tuwafanyie vita?

Ni mfumo wa ubepari unaosimamiwa na serikali kama ule wa Ufaransa?

Au ni mfumo ule wa zamani kwenye enzi za hayati Nyerere wa serikali na chama kushika hatamu na kuwa na mameneja na viongozi wanaojiiita wajamaa kumbe wabinafsi wakubwa na mabepari walio likizoni?

Au ni mfumo kama ule wa China ambao chama tawala huko kimekubali kutumia mazuri yote ya ubepari katika kuujenga mfumo imara wa uchumi na misingi bora ya maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia?

Lazima taifa lifikie mahala likae, lijadili na likubali na liutangazie umma juu ya uamuzi utakaofikiwa kuhusu ni mfumo gani wa uchumi na kijamii tutakuwa tunaufuata katika karne hii ya 22? Hatuwezi kuendelea kuwaacha Watanzania kwenye giza.

Mwaka Uliopita: Tumepanda, tunapalilia na tumevuna nini?

Mtu mmoja mmoja kwa ujumla wao ndio wanaounda taifa. Inapofikia mwisho wa mwaka inafaa kila mtu kujipima na kuona amefanikisha nini na ameshindwa nini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Wengi wanaamini kuwa wamekuwa wakipiga ‘maktaimu’ kwa kipindi chote hicho na sababu kubwa ikiwa ni kuwa kipato hakilingani kabisa na mahitaji yao ya kimaendeleo na matumizi ya kawaida.

Hii haiondoi ule ukweli kuwa katika nchi hii bado kuna visiwa vya utajiri na kila siku iendayo kwa Mungu tunaona maghorofa yakisimamishwa, magari mapya yakinunuliwa, biashara mpya zikifanyika na ‘dili’ za mabilioni zikitangazwa.

Hata hivyo kwa Watanzania walio wengi mwaka 2002 ulikuwa mwaka wa mapambano ambayo hayakuweza kutoa washindi lakini kuna wegni waliokata tamaa na kushindwa.

Taifa linalotaka kuwa imara kiuchumi lazima lichunguze kwa makini kwanini hali kama hii inatokea.
Haiwezekani kuona kuwa kuna maendeleo ya kiuchumi katika nchi lakini mifukoni mwa wananchi hamna kitu na wao wamebaki palepale walipokuwepo mwaka mmoja au miwili iliyopita.

Utaema nini juu ya hili? Mtu anatumia vibaya fedha yake? Mahitaji yake yameongezeka kupita uwezo wake au mfumo wa kuzawadia umepitwa na wakati?

Ukizitaka familia nyingi za Kitanzania hata hivyo ni zile ambazo haziwezi kula nyama sembuse kuku au samaki wasioshikika bei mpaka siku kuu tu.

Kama sera ni kuzuia mzunguko wa fedha ili watu wajifunze kubana matumizi basi sera hiyo imegonga ukuta maana imefikia kikomo cha watu kufunga mikanda na sasa wanaona serikali yao haiwatakii mema.

Faimilia zilizokuwa na watoto wasiokwenda shule mwaka 1995 serikali ya awamu ya tatu ilipoingia madarakani hivi leo zina watoto wanaokwenda shule za msingi, waliomo sekondari na wanaokaribia kuingia Chuo Kikuu.

Ukitazama mfumo wetu wa elimu kama ulivyo hata kama kuna madai ya kuwepo elimu ya bure hapa na pale bajeti kubwa ya Mtanzania katika miaka michache iliyopita imeishia kwenye elimu na nyumbani watu wanalazimika kula mchicha, kisamvu na ugali mchana na usiku.

Katika hali kama hii ni dhahiri kuwa japo watoto wanasoma lakini unyafuzi na utapiamlo unaowanyemelea kwa kuwa wazazi wao wana kipato duni kulinganisha na mahitaji ya lishe kamili hayawezi kuwaachia wafanye vizuri kamwe shuleni.

Huu ni wakati muafaka wa serikali kuu na serikali za mitaa kuangalia ni jinsi gani wanaweza wakamsaidia mtu mmoja mmoja na familia kuongeza kipato chake badala ya serikali zote kukaa mkao wa kucha na meno wa kutaka ima-fa-ima kumtoza mwananchi kodi hata kama hali yake ni taabani na mtu hawezi hata kuitosheleza familia yake.

Kwa kuwa macho yetu yameelekezwa kwa wageni kama wawekezaji tumesahau kabisa kuwa tunaweza kuwahamasiha wanamtaa wakawa na miradi inayochangia kuimarisha kipato chao na hivyo kupunguza makali ya maisha.

Ni dhahiri hili ni kama lilivyo kwa sababu wengi wetu na hasa tulioko serikalini tunataka kuvuna pale tusipopanda wakati tunashindwa hata kuwaandaa watu kulima, kupanda na kupalilia vyanzo mbalimbali vya kodi ya kesho na keshokutwa.

Kama ilivyo kwa mtaa ndivyo ilivyo kwa Kijiji. Vijiji vingi vina uwezo wa kuwa na miradi inayoingiza fedha ikiwa ni ya mtu mmoja au makundi ya watu katika sekta tofauti kama vile maji, elimu, usafiri na uchukuzi, kilimo, biashara, utalii na kadhalika lakini kwa kuwa tumekamia kuvuna pale tusipopanda basi kuna serikali chache sana za kijiji zenye mpango wa kuimarisha uzalishaji mali kwanza kabla ya kuanza kutoza kodi. Kodi ambazo aghalabu huua hata zile shughuli chache za kiuchumi na kijamii zinazoanzishwa na wale wanaothubutu kufanya hivyo katika mazingira magumu ya nchi hii ambayo yamemsahau mwekezajai wa ndani kwa kumkumbatia mwekezaji wa nje.


Kodi ‘kichaa’
Kwa kukosa ubunifu Tanzania sasa hivi sio tu ina utitiri wa kodi zinazowachanganya wananchi lakini pia zina kodi kichaa.

Kodi kichaa ni zile ambazo gharama ya kuzikusanya ni kubwa kuliko mapato yanayopatikana kutokana na chanzo husika.

Kodi kichaa ni zile zinazoua miradi michanga au miradi ambayo ndiyo kwanzaa inaanza kubuniwa.

Kodi kichaa ni zile zinazomuonea mlipa kodi mfanyakazi ambaye hana njia ya kuzikwepa maana ni ‘fixed and unavoidable’ lakini zinampa mwanya mfanyabiashara anayeingiza mara elfu au elfu kumi au milioni ya mfanyakazi huyo kukwepa kodi kubwa ambayo ingeliweza kuwa nafuu kwa mfanyakazi wa Tanzania.

Mfanyakazi huyo huyo akienda sokoni, dukani au kupata huduma yoyote ya kimaisha au ya kuanzisha mradi bado anakumbana na kodi nyingine nyingi kichaa ambazo aghalabu humfanya ajiulize hivi kweli-‘serikali hainiibii kumnufaisha mtu mwingine na ni nani huyo…?’

Maana kila akizunguka huku na huko haoni kazi iliyofanywa na kodi aliyokatwa. Na zile zinazofanyika zinafanyika nusu nusu tu.


Fedha zinaoza benki
Wakati huo huo vyombo vya habari vinaruka na habari kuwa kuna mabilioni yamekaa benki kwa sababu hakuna wa kukopesha.

Hakuna wa kukopesha kwa sababu Benki yetu kuu haina utaratibu wa kumnyanyua mzawa kwa mikopo ya riba nafuu wala kuchangia kwenye miradi inayoweza kuajiri malaki ya vijana wa Kitanzania wasio na ajira leo.
Fedha zinaozdea kwenye mabenki mengine yale ya ndani na ya nje kwa sababu yanataka kujiendesha kama benki zinavyoendeshwa huko Ulaya au Marekani na sio kama Benki ya Grameen huko Bangladesh.

Juu ya hayo benki zimekosa uongozi kupitia BOT unaoweza kupunguza hatari na hasara ya kukopesha kwa kuzifanya benki 5 au kumi kumkopesha mtu mmoja na hivyo kugawa ‘risk’ hiyo kwa wengi.

Kubwa zaidi ni kuwa mabenki yote kwa kiasi kikubwa bado hayajakaa mkao wa kusaidia Watanzania kuzalisha mali na kuongeza utajiri wa nchi kwa huduma na biashara ili mabenki na wananchi wote kwa pamoja wafaidike.
Tanzania ina kila kitu kwa hivi sasa cha kuifanya iwe nchi imara kiuchumi kama mabenki yatajigeuza kuwa vituo vya kuchochea uzalishaji mali, upanuzi wa biashara kimataifa na utoaji huduma za kimataifa katika sekta mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wa nchi kwa kasi zaidi.

Hofu kuwa Watanzania ni wakopaji wazuri lakini wasiolipa haina msingi. Tatizo ni uaminuf wa watumishi wa benki wenyewe na elimu na maarifa ya kuutumia mkopo kwa upande wa wakopaji. Ipo mifanyo ya kutosha kuwa Watanzania wazawa wakielimishwa kuhusu kukopa na kuzalisha ili kulipa madeni yao wanaweza kuchangia kuujenga uchumi wa nchi hii kwa kiasi kikubwa.


Mzunguko wa fedha katika uchumi wowote ndio kielelezo cha ufanisi na ufanifu ikiwa ni pamoja na tija ya nchi husika.

Mzunguko huo hivi sasa kwa Tanzania unakwaza kwa makusudi ili kuwafunza Watanzania thamani ya feha. Lakini somo limeshasomwa na likirudiwa rudiwa tena tutawachosha wanafunzi. Hivi sasa watu hawazungumzii tena fedha kwa matumizi bali kwa uwekezaji. Ni wakati gani mzuri kama huu wa kuachia mzunguko ufanye kazi yake na wawekezaji wa ndani waanze kufanya vitu vyao.

Tulichopanda katika elimu ni majengo mazuri na vifaa vya kufundishia kuwepo kitu kilichokuwa hakipo huko nyuma.

Lakini ipo haja ya kuangalia ni jinsi gani tunaweza kupanda na kupalilia mapato, lishe na huduma bora kwa wahusika wenyewe yaani wanafunzi na walimu.
Hatuwezi kuboresha elimu kama hatutaboresha kipato na mazingira ya kazi ya walimu.

Hatuwezi kuboresha elimu kama hatuwezi kuwasaidia wazazi kuingiza kipato cha kutosha ili watoto wao wale vizuri na hivyo kuwa na afya ya kuweza kumudu masomo darasanai.

Katika afya madai ya baadhi ya watu ni kuwa nchi za Kiafrika ikiwemo Tanzania zinang’ang’ana na ukimwi tu na kusahau magonjwa mengine yanayoua maelfu kila mwezi kwa kuwa gonjwa la kwanza lina mfadhili anayetaka kuona dunia nzima ina maadili ya zinaa kama yenyewe na pili gonjwa hilo eti ni la wakubwa na ndio sababu ya kelele zote hizi. Sijui ukweli uko wapi hapa. Kwangu mimi, hata hivyo, la muhimu ni kutoa kipaumbele kwa magonjwa mengine na kuachana na projekti za kitoto zinazowafaidisha walio kwenye miradi na sio waathirika iwe ni kwa malaria au magonjwa ya zinaa.

Zoezi la Ubinafsi-shaji, kuuza mali ya umma na mifuko minono
Ya akiba ya hili au lile nayo ni mambo mengine yaliyopandwa na kupaliliwa kwa misingi ya kunufaisha wakubwa zaidi na bila kuwajali wale wanaokatwa pesa zao. Tuuone ukweli huu na sio kuzika kichwa kwenye mchanga kama mbuni mwerevu.

Tanzania imeonyesha mapinduzi makubwa katika Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kinachotakiwa ni kwa viongozi wa serikali kubadilika na kwenda na wakti ili vitu hivi vitumike kuipa nchi nguvu ya kimataifa katika eneo hili la Kiafrika.

Tunaweza kutishwa na wawekezaji katika sekta nyingine lakini sio hii kama serikali itawasaidiwa wazawa barabara. Na kuwasaidia kwenyewe ni kuondoa kodi kichaa na sheria kichaa. Kodi na sheria zinazoua ari ya kukua na kupanua biashara hizo kwa faida ya nchi na wananchi.

Ushindani na ubepari unahitaji Watanzania wasifungwe fungwe na sheria zisizowafunga wawekezaji toka nje.

Hisia kuwa nchi inauzwa kwa wageni inatokana na ukweli kuwa sisi wenyewe tunadanganyana na tunapeana maneno mengi lakini vitendo daima hamna. Tubadilike na tuanze kupanda na kupalilia moyo wa kutaka kuona kila Mtanzania ananyanyuka na kufaidika na maendeleo ya kiuchumi kesho na keshokutwa.

Ubepari na hatma ya umaskini Afrika

‘Utajiri sio unachozalisha, bali unachobaki nacho!’-Nukuu

Hoja ja kuwa mali aliyo nayo tajiri imetokana na jasho au akili zake mwenyewe ilichambuliwa na J. K.Nyerere vizuri na kwa undani kabisa na kilichodhihiri ni kuwa hakuna mtu mmoja hata awe na akili namna gani anayeweza kuwa na uwezo wa kujitajirisha mwenyewe bila kuinyonya jamii kwa njia moja au nyingine.

Katika medani ya kimataifa ukweli huu ni wazi zaidi. Nchi tajiri ni tajiri kwa sababu zinanunua kwa bei rahisi kutoka nchi maskini na kuwauzia maskini hao hao inachowauzia kwa bei ghali zaidi.

Mishahara katika nchi maskini ni ya kitumwa wakati huko Ulaya mishahara ni mikubwa kutokana na tofauti za kipato kati ya nchi maskini na tajiri.
Kama ilivyo kati ya nchi maskini na nchi tajiri ndivyo ilivyo kati ya tajiri na maskini. Nchi maskini zinataka bei halali, wakati maskini wanataka malipo halali kama mishahara au kipato ili nao wawe na fursa ya kudunduliza na kujikwamua kutokana na umaskini siku moja.

Tunachokizungumza hapa ni kuwa kile kinachozalishwa nchini au duniani kisipogawanywa kwa haki basi tofauti kubwa kati ya maskini huzuka.
Jitihada zikifanywa kuhakikisha kuwa kinachozalishwa kinagawanywa kwa haki zaidi basi na umaskini nao unapungua kwa kiasi kikubwa.

Tunasema India kuna umaskini wa kutisha kwa sababu kina Bill Gates hawaruhusiwi kuchipua huko lakini umaskini wa India sio kukosekana kwa matajiri bali kukosekana kwa mgawanyo mzuri wa keki ya taifa.

Kweli binadamu ni mgumu kubadilika na nchi inatakiwa kujenga mazingira ya kuzalisha kina Bill Gates wengi kadri iwezekanavyo. Lakini kina Bill Gates hao watasaidia asilimia ndogo tu ya Wananchi wa nchi husika kuwa nao matajiri pia.

Kwa Tanzania wawekezaji wanaweza kuchangia kiasi fulani vita vyetu dhidi ya umaskini lakini hili haliondoi ukweli kuwa mchango mkubwa kuuondoa umaskini utatoka kwenye vyombo vyetu wenyewe vya fedha vikiongozwa na Benki Kuu.
Vyombo hivi vikibweteka kama vilivyobweteka sasa katika harakati za kupunguza umaskini tusahau kabisa kuupunguza umaskini hata kwa miaka 300 ijayo.

Mtu binafsi ana ukomo wa maisha. Serikali au vyombo vya fedha havina ukomo wa maisha. Pakijengwa mfumo mzuri wa kiuchumi unaowajibika kuhakikisha pato la Taifa linagawiwa kwa namna ambayo saa zote majaribio ya kuwazalisha kina Bill Gates yanafanyika basi hili peke yake linaweza kuwa chachu inayotosha katika uzalishaji mali na kupambana na umaskini.

Vyombo na taasisi zifanyazo kazi
Tatizo letu Afrika iwe ni wakati tunafuata mfumo wa kijamaa au kibepari ni kuwa na vyombo visivyofanya kazi.

Na pale vyombo hivyo vilipofanya kazi vilifanya kazi hiyo kwa ajili ya waliokabidhiwa vyombo kujitajirisha wao wenyewe na familia zao; kuwatajirisha wageni; lakini sio kutajirisha nchi na watu wake.

Kampuni au shirika liwe katika mfumo wa ujamaa au ubepari kama likiendeshwa kwa namna ya mwenye mali kujinufaisha yeye mwenyewe bila kunufaisha wateja/Wananchi bado tatizo linakuwa palepale.

Sio chombo kinachozalisha ili nchi itajirike bali kinazalisha kumtajirisha mtu mmoja au wachache potelea mbali kama nchi inapoteza kitu fulani kwa kufanya hivyo.

Mali inayozalishwa sio mali isiyohamishika. Na ili mradi wazalishaji wawe ni Wananchi au wawekezaji toka nje wanahamisha mali hiyo na haikai hapa nchini ni muhali kuona jinsi gani tunaweza kuondokana na umaskini.

Biashara hapa itakuwa ni sawa na ya mchumia-tumbo, yaani, kwa hapa mwekezaji mwenyewe ndiye anayefaidika lakini nchi haipati lolote isipokuwa statistiki za uongo na kweli kuwa wawekezaji wameongezeka na uzalishaji mali umeongezeka.

Swali linakuwa baada ya mali na faida hiyo kuzalishwa imebaki nchini au imekwenda nje?

Utajiri sio kile kinachozalishwa bali ni kile watu na nchi inachobaki nacho.

Utamaduni kama mizizi
Mti hustawi pale tu mizizi yake inaposhika ardhini. Uchumi wa nchi hauwezi kujengwa juu ya utamaduni au tabia za kigeni.
Matajiri wanaozuka katika mazingira na utamaduni wa aina hiyo ni sawa na maua yanayochipua jangwani.

Umaskini Afrika kwa kiasi fulani unachangiwa na nchi nyingi kushindwa kudumisha utamaduni wake na kuutumia kama chambo cha kuvuta utajiri wa aina mbalimbali.

Mathalani, Tanzania, nchi inayosemekana kama mama wa Kiswahili imeshindwa kabisa kutumia lugha yake hiyo inayothaminiwa na kila mmoja Afrika kujinufaisha.

Mila na desturi za makabila mbalimbali Tanzania leo imekuwa ni kitu cha kuonea aibu na sio fahari. Kwa mantiki hii mila na desturi hizo pia kwa kutoweka kwake kunachangia umaskini zaidi kwa nchi kukosa asili wala fasili.

Nchi nyingi za Kiafrika tofauti na Uchina au India zimeshindwa kutumia mitishamba yao kujinufaisha kwa sababu walioko katika sekta ya afya tayari wamenunuliwa na makampuni na wafanyabiashara wa madawa ya kizungu. Na wanaona bora kukubali dawa feki kuliko kuboresha dawa zetu asilia.

Michezo kama nyenzo ya utamaduni imara imeachwa kama yatima na matokeo yake leo Tanzania ni kichekesho karibu katika kila aina ya mchezo.
Tukumbuke wakati sisi ni kichekesho majirani zetu leo wanatajirika na kuneemeka kutokana na hiyo hiyo michezo.

Kwa hiyo utamaduni wa uongozi dhaifu unaotegemea fadhila na huruma ya wafanyabiashara umejenga nchi kujidhalilisha na kujiuza kwa bei rahisi kwa yeyote yule anayetaka kutukaanga kwa mafuta yetu wenyewe.

Kwa kukubali tamaduni za wengine kichwa-na-miguu tumejiweka mahala pabaya ambapo hatuna msingi wa kujengea mtaji, teknolojia na utajiri wetu wa asili.

Japan, China, Uarabuni, Korea Kusini, Malaysia tofauti na nchi za Marekani ya kusini kwa kutokubali utamaduni wao kuchafuliwa mno na wageni wamejenga aina ya uchumi ambao sio rahisi kushindwa kufanya kazi labda pale dunia nzima inapokuwa kwenye matatizo makubwa.

Hili ndilo linalotokea Afrika Kusini pia ambako Wazungu wa huko wamekubalina na Waafrika kuunda taifa lenye utamaduni tofauti na ule wa Magharibi au wa kuiga.
Na siri yao wote hawa ni kuwa Wananchi kwa viongozi wanakumbatia na kuenzi utamaduni wao. Hapa kwetu viongozi wetu kama Yuda Iskarioti wanaukana utamaduni wao.

Hivi sasa wamezuka manabii wa kisiasa na kadhalika wanaotaka ghafla bin vuu tuusahau utamaduni wetu na kukubali kukumbatia yale wazungu wanayotaka tuyakubali eti kwa faida yetu wenyewe.

Dawa ya umaskini wetu pamoja na mambo mengine ni kutafuta yote mazuri yaliyokuwepo katika utamaduni wetu na kuyarejesha upya kwa faida ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.

Tusipofanya hivyo kama wana Israel tutaendelea kutangatanga nyikani kwa miaka 4o kama sio zaidi. Wataalamu wanasema kwa uhakika ni miaka 166.
Utamaduni wa uzalishaji mali kwa njia bora zaidi na zenye ufanifu, ufanisi na tija zaidi bado ni mgeni kwa Waafrika.

Ukiangalia kwa undani, hata hivyo, utakuta tatizo sio kitu kingine ila elimu. Elimu inayotolewa hivi sasa ni ile isiyochangia moja kwa moja kwenye shughuli za kibiashara au uzalishaji mali.

Katika dunia hii ya ushindani na kama kweli tunataka kuusogeza nyuma umaskini hatuna muda wa kupoteza kusoma vitu visivyo na maana katika maisha yetu ya kila siku.

Hii ni dunia ya kusoma na kuelewa menejimenti, masuala ya fedha, uchumi, biashara, masoko, teknolojia, uzalishaji mali, uhasibu na staid na taaluma nyingine ambazo moja kwa moja zitachangia kuuondoa umaskini wa mtu binafsi na nchi kadhalika.

Masomo hayo yakifundishwa kwa lugha ya Kiswahili ndiyo itakuwa mteremko kabisa kuupunguza umaskini kwa asilimia kubwa tu.

Katika kufanikisha hili lazima tuwe na utawala bora kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa. Na uongozi bora kwangu mimi ni uongozi usioingia madarakani kwa nia ya kujitajirisha wao wenyewe bali kuwatajirisha Wananchi kwa ujumla wao. Tumeona wangapi waliojitajirisha wenyewe kama viongozi wamekuja na kuondoka lakini nchi wameiacha katika umaskini ule ule. Na wao wenyewe wala hawakwenda na utajiri huo wala kuacha sifa yoyote ya maana ya kusaidia watu wao kupambana na umaskini.

Pamoja na haya yote tukubali kuwa ubepari umeingia nchini, Afrika. Lakini je, tuufuate kama unavyoendeshwa huko Ulaya na Marekani. Au Waafrika wanaweza wakawa na mfumo wa kisiasa na kiuchumi unaoitwa ubepari-wa-kijamaa?

Mfumo unaotoa fursa sawa kwa wote kujitajirisha lakini wakati huo huo unawalinda watu wetu wasiadhirike kama wazungu maskini wanavyoadhirika huko kwao?

Hatima ya umaskini Afrika kamwe haiwezi kuamuliwa kwa misaada au ushauri wa wageni. Hatima yetu itaamuliwa na siasa zetu wenyewe humu ndani, siasa zitakazokataa ubinafsi, ubadhirifu na ulafi ili wote tuweze kuwa na maisha bora.

Dalili za Chama Kinachosambaratika

CHAMA chochote cha kisiasa au shughuli nyingine kama ilivyo kwa kundi lolote la watu, liwe kubwa au dogo, likishakaa pamoja kwa muda mrefu na kuzoeana kupita kiasi huwa linapoteza sio tu dira au visheni yake bali pia hekima na busara zake katika kutathmini uhalisia wa mambo na maamuzi ya kimaadili au kiitikeli bali pia hata uwezo na kasi yake ya kufanya maamuzi kwa wakati unaotakikana na pale yanapofanyika haraka haraka, maamuzi hayo yanakuwa hayana ubora unaokubalika.

Chama kinachoathirika na gonjwa la 'ndivyotunavyofikiri' (groupthink) kama ulivyogunduliwa na kuelezewa na guru wa menejimenti ya makundi ya watu, Prof. Irving Janis, sikuzote hudharau njia na fursa mbadala na hujikuta kikifanya maamuzi bomu na yaliyo na sura ya kuvifanya vyama vingine vya kisiaasa na makundi mengine ya watu kuonekana ni ya vichaa, watu hatari na wasiojua watakacho.

Chama au kundi lolote linaweza kuugua ugonjwa wa 'ndivyotunavyofikiri' hasa pale wanaounda chama hicho au kundi hilo wametoka kwenye hali au mazingira yanayofanana na wamefinyangwafinyangwa au wote kulazimisha kuwa na mtazamo au msimamo mmoja pamoja na kufikiri sawasawa kama maroboti.

Ugonjwa huu pia huwaathiri kwa kiasi kikubwa wale wanaoziba masikio na macho yao kuona yanayotokea nje ya chama au kundi lao na wale wasiosikia mawazo au fikra mpya au tofauti toka nje ya chama au kundi husika. Au kwa kifupi wale wote wanaoshindwa kuzisoma na kuzielewa alama za mabadiliko ya nyakati zinazoanza kusheheni kila eneo la kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Aidha, kutokuwepo kwa kanuni na taratibu zinazoeleweka za kufikia maamuzi makubwa yanayohusu chama au kundi na watu wengine nako pia huchangia kupata gonjwa hili la 'ndivyotunavyofikiri'.

Ni rahisi kujua kama chama au kundi linaugua ugonjwa wa 'ndivyotunavyofikiri' kwa sababu Javis ameelezea kuwepo kwa dalili kubwa kama nane hivi. Dalili hizo ni hizi zifuatazo:

• Kujidanganya kuwa hakuna kisichoweza kufanyika na sio rahisi kushindwa na chama au kundi lingine la watu. Hili hujenga kujiamini kupita kiasi kwa viongozi na wafuasi wa chama, jambo ambalo husababisha viongozi na wafuasi hao kufanya majaribio na mambo ya hatari yanayoweza kukigharimu chama na wanachama wake na pengine hata nchi husika;

• Kuhalalisha kwa pamoja kiurahisi bila ya kuhoji uamuzi wowote unaofanywa na chama au kundi. Wanachama huwa hawasikii la muazini au la mchota maji na hudharau maonyo yote wanayopewa na huwa wagumu kubadili mitazamo na misimamo yao juu ya mambo mbalimbali;


• Kudhani wao ni wacha-Mungu, watakatifu na wenye haki zaidi kuliko wengine. Wanachama huamini katika imani na uhalali wa imani au msimamo wao na hivyo hudharau haki na itikeli za mtazamo na msimamo wao wakati wa kufanya maamuzi au jambo lolote linalohusu jamii au jumuiya nzima;

• Hudhihaki vyama au makundi mengine katika jamii. Hisia za sisi ni kitu kimoja au huyu ni mwenzetu na wale ni maadui zetu hutawala na hivyo kusababisha kukosekana kwa matumizi yoyote ya akili, busara na hekima katika kushughulikia migogoro kwa njia sahihi na mujarabu;

• Shinikizo kwa wanaohitilafiana na msimamo wa viongozi wa chama au kundi husika. Wanachama wote, wakiri au wasikiri hivyo, huwa wanapata shinikizo kubwa toka kwa wenzao kutotofautiana kabisa na misimamo na mitazamo ya chama au kundi husika;

• Kujichuja wenyewe. Mashaka ambayo baadhi ya wanachama wanayo juu ya uamuzi au jambo lolote juu ya msimamo wa pamoja uliofikiwa (mathalani, kuilipa Dowans) huwa havipewi fursa na ni adimu kutokeza hadharani.

• Kujidanganya kuhusu juu ya wote kukubaliana jambo kwa pamoja. Fikra, misimamo, mitazamo na uamuzi wa wengi huchukuliwa kwamba ni watu wote kwa pamoja wamekubaliana ingawama mara nyingi ukweli huwa ni kinyume kabisa na hilo. Hakukosekani wanaolikataa wazo au jambo bali hata wakiwa wengi maji hufuata mkondo kwa kwenda na msimamo wa viongozi na wapiga debe wa chama au kundi husika.

Walinzi wa mawazo na fikra wanaojichagua na kujipandikiza wenyewe ili viongozi wasipate habari mbaya au habari viongozi wasizotaka kusikia au ambazo wakisikia watafanya maamuzi tofauti kabisa na yale wanaowazunguka wanayoyataka. Watu wachache hujichukulia wenyewe jukumu la kumlinda kiongozi na wafuasi wake dhidi ya habari zozote mbaya au zinazotoa picha tofauti kabisa na ukweli ulivyo kama unavyoelezwa na habari za kupikwa na kuletwa mezani makusudi kutoa picha ya uongo na kweli kuhusu uamuzi au hali halisi ilivyo. Habari zozote zenye harufu mbaya au picha chafu huchujwa na hazifiki mbali. Hili hufanywa pia kwa kutumia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na chama na serikali husika.

Ndivyotunavyofikiri hutokea pale chama au kundi linapokuwa na umoja unaolazimishwa na panahitajika pafanyike maamuzi makubwa ya kichama, kiserikali au kitaifa. Maamuzi yenyewe yakihusu aghalabu riziki na uhai wa chama na viongozi wake pia. Hili hulazimisha viongozi kukubalina penda usipende juu ya jambo husika; hakuna anayekuwa na motisha ya kulichambua na kulipangua jambo na kulipanga upya ili kupata uamuzi sahihi; na hudharau au kupuuza maamuzi mbadala mengi ambayo huwa hata hayafikiriwi kabisa hata kama muda unaruhusu.

Shinikizo hili husababisha suala la ubora wa maamuzi kutozingatiwa kabisa na uhai na umoja wa chama na viongozi wake kupewa kipaumbele zaidi kuliko kitu kingine. Agjhalabu uamuzi huwa ni bora wote tufe, kuliko tu chama na wanachama wake kufa (kisiasa).

Maamuzi yanayofanywa wakati chama au kundi linaugua 'ndivyotunavyofikiri' huwa hayana uwezekano wa kufanikisha jambo lililokusudiwa hata kidogo.

Katika nchi kama hizi zetu za Kiafrika kutokana na heshima ya ’ubaba wa kitaifa’ na ’ukombozi au uhuru wa bendera’ wale walioshiriki katika harakati za uhuru huwa wanaheshimiwa mno na kubakizwa madarakani muongo baada ya muongo. Lakini sasa subira imeanza kupungua kwa vijana wetu. Wanashindwa kuvumilia kuwa chini ya rais huyo huyo toka wakiwa chekechea, msingi, sekondari, vyuo vikuu hadi wanakuwa joblesi na ’unwanted and unloved’ nchini mwao na bado mtu anang’ang’ania kubaki madarakani.

Pamoja na hili ni kichekecho kuona wale wanaopewa madaraka ya kuwa viongozi wa vyama vikongwe Afrika wanakuwa ni wachekeshaji, wasanii na wababishaji na sio watu siriazi na kile wanachokifanya na wala huwa hawajui wapi dunia inakoelekea.
Aidha, .Viongozi huendelea kukanusha kuwa chama au kikundi hakina tatizo, mgawanyiko wala misiguano hata pale kinapokuwa kinachungulia kaburini;

. Viongozi huwa wanajishughulisha na mambo ambayo yangefanywa vizuri zaidi na watu wa chini, huku wakiacha kufanya yale yanayowahusu wao na hivyo kutumia muda na rasilimali kwa vitu visivyo na faida kwa chama au kikundi husika;

. Hujitahidi kufanya sherehe, mbwembwe na kujionesha kwa kila aina ili kwa nje kionekane kwamba ni chama au kikundi chenye umoja na bado chenye nguvu na uwezo wa kufanya mambo ya maana na kumbe sivyo;

. Huonesha upendeleo wa wazi kwa wake/waume zao, watoto wao, ndugu zao, jamaa zao , marafiki wao na wale wote wanaonufaika kwa njia moja au nyingine kutokana nao;

. Huwa hakijali kabisa muda unavyoyoyoma na kupotea na huamini hakuna anayeweza kukiharakisha kwa hili au line na hakuna sababu ya kuharakisha kitu kwa kuwa kiko madarakani;

Iko mifano mingi ya 'ndivyotunavyofikiri' toka sehemu mbalimbali duniani. Mathalani, mojawapo maarufu ni lile la serikali ya Marekani kushindwa kutabiri kushambuliwa kwa nchi hiyo na Japani zaidi ya mika 60 iliyopita; Uvamizi wa Marekani huko Cuba ulioshindwa vibaya; na vita vya Marekani dhidi ya Vietnam kaskazini isiikomboe Vietnam Kusini.

Hivi karibuni, tumeona matukio ya Blair na Bush, kuziingiza Uingereza na Marekani katika vita dhidi ya Iraq kwa sababu ambazo hazikuwa za kweli na matokeo ya maamuzi hayo kwa nchi hizo na dunia kwa ujumla.

Aidha, jinsi Waafrika walivyolazimishwa na nchi hizo za Uingereza na Marekani kukubali kujiunga na vita dhidi ya ugaidi na fedha chafu bila ya watu wa nchi husika kuachiwa kutoa maoni na misimamo yao juu ya jambo hilo. Matokeo yake yakiwa kupandwa mbegu za chuki dhidi ya Uislamu na Ukiristo Afrika na kwingineko.

Tumeona 'ndivyotunavyofikiri' pia ikiathiri Umoja wa Afrika (AU) kuhusiana na Al Bashir wa Sudan; Mugabe wa Zimbabwe; wachocheaji mauaji ya Rwanda na Kenya na sasa Cote d'Ivoire. Kote huku kwa kiasi kikubwa maslahi ya wasionacho hayakuzingatiwa ila yale ya wale walichonacho tu. Wakubwa wanatambua fika ridhaa yao kwa jambo kama hilo ni kaburi na mauti yao pia kisiasa na hususan kwa madikteta uchwara wanaopora mamlaka ya wananchi katika tawala zao.

Huko nyuma kiasi, wakati Watanzania wakidanganywa na kudhulumiwa na siasa za chama kimoja maamuzi kadhaa yaliyofanyika huko wahusika wakiugua 'ndivyotunavyofikiri' ni pamoja na Azimio la Arusha, Ujamaa na Kujitegemea, kuua serikali za mitaa, uanzishaji wa vijiji vya ujamaa, kuua vyama vya ushirika, kuua michezo mashuleni, kuua matumizi ya lugha za kikabila katika magazeti na redio, uamuzi wa kuhamia Dodoma na maamuzi mengine mengi kama hayo yote yaliathirika si haba na gonjwa la ndivyotunavyofikiri na ziada yake ndivyotunavyokubaliana.

Kiujumla kutokana na uoga na kutokujua nafasi yao kama mhimili pekee katika mihimili iliyopo unaoweza kupiga vita rushwa, wizi wa kura, ufisadi na kuwa na watu waovu kama viongozi vyombo vyetu vya habari na hususan televisheni na redio vimewaangusha Watanzania, na kwa bahati mbaya ni Watanzania wenyewe walioliruhusu hili kutokea.

Hususan, wale ambao kabla ya kuwa viongozi walivienzi vyombo vya habari lakini baada ya kupewa uongozi sasa wanataka kuvigandamiza vyombo vya habari kama sio kuviulia mbali.


Chama si mtu mmoja. Mtu mmoja hufa na husahaulika baada ya muda si mrefu. Chama ni kundi la watu. Kundi ambalo kama likiweza kujizaa upya kila inapohitajika huweza kuishi milele. Kinachotakiwa kwa chama chochote kinachoona kuwa kinaugua gonjwa hili kukaa na wataalamu wa masuala haya na kuanza kukisuka chama upya ili kukabili zama mpya. Na wakati ni huu, hakuna kabisa muda wa kuchelewa.