Sunday, October 2, 2011

Huwezi kupambana na soko huru, kubali yaishe....

MANENO kama magendo, uvushaji mali mipakani, njia za panya, rushwa, ujangili, uhujumu uchumi ni maneno ya wanasiasa na mangimeza uchwara ambao wameshindwa kuukubali utandawazi na kwenda na wakati kwa kuilalia sekta moja ya uchumi na kuinufaisha zaidi sekta nyingine.

Penda usipende ukishaamua kufuata soko huru, ni ujinga kutaka kupambana na soko hilo kwani lina nguvu zake zisizoonekana na hizo ndizo zinazofuatwa na sio kauli za wanasiasa.

Safari, kauli na maneno ya wanasiasa yanayotolewa hivi sasa ni jitihada za kujikosha na kujisafisha baada ya kushindwa kufanya kazi wanayostahili kuifanya na badala yake kurukia yale yanayostahili kufanywa na soko bila ya kushinikikizwa na mtu.

Kwa mfano tunaona maamuzi ya EWURA yanavyochangia zaidi kunganya watu badala ya kunufaisha umma kwa sababu taasisi hiyo inataka kuingilia moja kwa moja maamuzi ya soko badala ya kuandaa na kuendeleza mazingira ambayo yatafanya sekta husika kufanya maamuzi yanayofaa kutokana na ujenzi wa ushindani na kuongeza sauti ya walaji nchini.

Sukari ni bidhaa inayotokana na zao la miwa. Miwa hii inapochakatwa ndipo sukari huzalishwa. Inavyoelekea ni rahisi sana kuachia soko huru kufanya kazi pale uuzaji miwa kwa wenye viwanda unapohusika, lakini ni rahisi kuingilia soko huru pale uuzaji sukari unapowanufaisha zaidi wenye viwanda na wafanyabiashara kuliko wananchi. Huu ni walakini wa mipango na sera. Na mipango na sera havifanywi kwa kushtukia bali ni vitu vinavyochukua muda.

Nilishawahi kuzungumzia jambo hili katika kesi ya saruji. Ghafla saruji ya Tanzania ilijikuta ina soko zuri nchi jirani. Kama ilivyo kawaida wanasiasa walichoona ni kuzuia saruji isiuzwe nje. NIkadai hilo ni kosa. Nikashauri kwamba, Malawi na Afrika Kusini na nchi za mbali zilikuwa na sukari nzuri tu iliyokuwa ikiuzwa kwa bei nafuu kuliko yetu, hivyo sisi tukubali kuuza yetu kwa bei ya juu kwa majirani na sisi tununue saruji ya bei rahisi toka nje. Hii ni akili ya kuzaliwa ya kibiashara na sio jambo kubwa kiasi hicho.

Ninarudia tena ni makosa kuingilia soko ila tu kama tunataka kuonesha unafiki wa kisiasa na machozi ya mamba eti tunawapenda sana Watanzania.

Kama tunawapenda Watanzania tatizo sio bei ya sukari, bali ni gharama za uendeshaji viwanda vya sukari na mashamba ya miwa. Mipango na sera za kuwapenda Watanzania zilikuwa zinatakiwa kuanzia huko kwa kuhakikisha kuwa bei ya dizeli, gesi na umeme, gharama za usafirishaji, nauli, upatikanaji umeme na mipango mibadala kiuchumi inakuwepo kwa wakati na hatufanyi kazi zetu kama vile zimamoto.

Nimewahi kuongelea pia juu ya ukubwa wa nchi hii ambao umeegemea zaidi kunufaisha mkoa wa Dar es salaam na wakazi wa Dar es salaam kuliko watu wa sehemu nyingine yoyote nchini. Kwa sababu hiyo bei za Dar es salaam ni rahisi kuliko za Ujiji, Tunduma, Mtwara, Peramiho, Bukoba, Holili, Namanga, Mwanza na Tarime.

Hali hii ya unafuu kwa Dsm na ughali kwa mikoa iliyo pembezoni ni kosa la kimipango na kisera linaloendelea kufanywa na serikali na chama tawala kwa kushindwa kutimiza ahadi na nadhiri yake ya kuufanya Dodoma kuwa mji mkuu wa nchi na vilevile kukaidi ushauri wa baba wa Taifa wa kupeleka madaraka mikoani au angalau kwenye ngazi ya kanda.

Makao makuu ya serikali yangelikuwa ni Dodoma ni dhahiri jiji la Dar es salaam lingebaki la kibiashara na hivyo kunufaika zaidi kibiashara na sio pia kisiasa na kiutawala kwa ofisi nyingi za kisiasa na zile za kiserikali kuwa na makao yake makuu mkoani hapa. Mikoa pembezoni ingelinufaika sio haba na kile Dar inachonufaika nacho leo, na hivyo wananchi wake kuwa na nafuu kubwa zaidi maishani.

Madaraka mikoani yangeruhusu mikoa iliyoko pembezoni moja kwa moja kufanya biashara na nchi jirani na kunufaika kijamii na kiuchumi kuliko ilivyo hivi sasa. Hakuna haki yoyote kuwazuia wazalishaji wa kitu chochote hapa nchini kupata bei nzuri soko la dunia au masoko ya nchi jirani. Hiyo siyo kazi ya wazalishaji wahusika, kupata vitu vya bei nafuu ni kazi ya serikali na sio lazima iwalazimishe wazalishaji wauze kwa bei serikali inayotaka. Wakijaribu kufanya hivyo kwenye sekta ya viwanda, hakuna (kama kweli bado nchi ina viwanda) kiwanda kitakachokubali na kubakia kuzalisha hapa nchini. Hii ni amri ya soko huru. Na soko huru sio tu katika bidhaa za viwanda bali pia katika mazao ya kilimo ambayo pengine ni muhimu zaidi kuliko kwa maisha na uhai kuliko bidhaa za viwandani.

Aidha, wakati umefika kuipa sekta ya kilimo uhuru ambao tayari sekta ya biashara na viwanda unayo, kama kweli tunataka kuona mapinduzi ya kilimo yakizuka nchini.

Tuliwahi kuongelea huko nyuma juu ya kuzifanya balozi zetu za nje kuwa ni balozi za kiuchumi na kimkakati. Huu ni wakati muafaka balozi zetu kuwa na watu wanaofuatilia masoko na pale inapoonekana mazao na bidhaa zetu yana bei nzuri nchi za nje basi tuuze, na sisi kama walivyo seremala badala ya kukaa kwenye viti tukae kwenye mbao tukijua kwamba kwa kufanya hivyo tunaweza kuja kuwa na samani bora zaidi siku zijazo.

Afrika ina kasoro moja kubwa. Na hii siyo nyingine ila ni kule kuongoza nchi na kuishi kama vile mambo 'yatajiseti' yenyewe, na wahusika wakaacha kuwa na mipango na mikakati hai ambayo inaweza kuleta utofauti mkubwa katika mustakabali wa nchi na watu wake. Hii ni lazima iwe ni visheni ya muda mrefu na sio mpango wa papo kwa hapo.

Ukichangia na kasoro mbalimbali katika mifumo, miundo, uratibu, udhibiti na utekelezaji ni rahisi kuona kwanini wanasiasa Afrika huona kuwa kuingilia soko huru ni njia ya mkato katika kufanikisha malengo yao ya kisiasa hata kama yale ya muda mrefu kiuchumi yanaharibika.

Fedha ambazo sasa serikali za mikoa/mitaa inazibeba katika vita visivyo na tija dhidi ya wauza sukari nje, ni bora zitumike kutatua matatizo ya wakazi wa mkoa husika kuliko kufujwa kama zinavyofujwa.

Ni vita isiyo na tija maana kimahesabu katika suala zima la magendo mipakani changamoto sio kuzuia tu bidhaa isivuke mpaka bali kubwa zaidi ni kuona hali, silaha za Kisaikolojia na maisha ya wale unaotaka washiriki katika vita hivyo. Ni dhahiri vita dhidi ya magendo ya sukari mipakani tayari vimekwishashindwa hata kabla havijaanza kwa sababu mlolongo mzima wa wale wanaotakiwa kuzuia sukari kuhusu nje kwa bahati mbaya ni orodha ya watu wenye njaa na kiu kali ya hali bora ya maisha na ambao hivi sasa wanaona kifo kwao ni karibu zaidi kuliko malengo mbalimbali waliyojiwekea kimaisha.

Ni polisi gani atakataa milioni 20 achilia mbali milioni 40 huko mpakani; ni ofisa uhamiaji gani atakataa milioni 100 katika mipaka yetu na kuna kioingozi gani mwenye uthubutu wa kukataa zaidi ya hizo katika mikoa yetu inayoongozwa na viongozi ambao hawakuchaguliwa bali wanateuliwa na wakubwa na aghalabu sio wazawa wa mikoa husika na hawana mapenzi wala uchungu na mkoa au wilaya wanaoyoisimamia!

Vita dhidi ya magendo kwa kutumia watu wenye dhiki, njaa, ukata na mishahara duni ni muhali kufanikiwa. Kinachoweza kufanikiwa hapa ni mipango na sera zinazoendana na soko huru na sio vinginevyo. Maana mwisho wa yote, badala ya wafanyabiashara tu kuwa ndio wanaonufaika basi unafaidisha pia wengine kiulaini kama vile watumishi vyombo vya ulinzi, maofisa kodi, maofisa uhamiaji na watu kama hao kwa hasara ya nchi nzima na wananchi wote kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment