‘Utajiri sio unachozalisha, bali unachobaki nacho!’-Nukuu
Hoja ja kuwa mali aliyo nayo tajiri imetokana na jasho au akili zake mwenyewe ilichambuliwa na J. K.Nyerere vizuri na kwa undani kabisa na kilichodhihiri ni kuwa hakuna mtu mmoja hata awe na akili namna gani anayeweza kuwa na uwezo wa kujitajirisha mwenyewe bila kuinyonya jamii kwa njia moja au nyingine.
Katika medani ya kimataifa ukweli huu ni wazi zaidi. Nchi tajiri ni tajiri kwa sababu zinanunua kwa bei rahisi kutoka nchi maskini na kuwauzia maskini hao hao inachowauzia kwa bei ghali zaidi.
Mishahara katika nchi maskini ni ya kitumwa wakati huko Ulaya mishahara ni mikubwa kutokana na tofauti za kipato kati ya nchi maskini na tajiri.
Kama ilivyo kati ya nchi maskini na nchi tajiri ndivyo ilivyo kati ya tajiri na maskini. Nchi maskini zinataka bei halali, wakati maskini wanataka malipo halali kama mishahara au kipato ili nao wawe na fursa ya kudunduliza na kujikwamua kutokana na umaskini siku moja.
Tunachokizungumza hapa ni kuwa kile kinachozalishwa nchini au duniani kisipogawanywa kwa haki basi tofauti kubwa kati ya maskini huzuka.
Jitihada zikifanywa kuhakikisha kuwa kinachozalishwa kinagawanywa kwa haki zaidi basi na umaskini nao unapungua kwa kiasi kikubwa.
Tunasema India kuna umaskini wa kutisha kwa sababu kina Bill Gates hawaruhusiwi kuchipua huko lakini umaskini wa India sio kukosekana kwa matajiri bali kukosekana kwa mgawanyo mzuri wa keki ya taifa.
Kweli binadamu ni mgumu kubadilika na nchi inatakiwa kujenga mazingira ya kuzalisha kina Bill Gates wengi kadri iwezekanavyo. Lakini kina Bill Gates hao watasaidia asilimia ndogo tu ya Wananchi wa nchi husika kuwa nao matajiri pia.
Kwa Tanzania wawekezaji wanaweza kuchangia kiasi fulani vita vyetu dhidi ya umaskini lakini hili haliondoi ukweli kuwa mchango mkubwa kuuondoa umaskini utatoka kwenye vyombo vyetu wenyewe vya fedha vikiongozwa na Benki Kuu.
Vyombo hivi vikibweteka kama vilivyobweteka sasa katika harakati za kupunguza umaskini tusahau kabisa kuupunguza umaskini hata kwa miaka 300 ijayo.
Mtu binafsi ana ukomo wa maisha. Serikali au vyombo vya fedha havina ukomo wa maisha. Pakijengwa mfumo mzuri wa kiuchumi unaowajibika kuhakikisha pato la Taifa linagawiwa kwa namna ambayo saa zote majaribio ya kuwazalisha kina Bill Gates yanafanyika basi hili peke yake linaweza kuwa chachu inayotosha katika uzalishaji mali na kupambana na umaskini.
Vyombo na taasisi zifanyazo kazi
Tatizo letu Afrika iwe ni wakati tunafuata mfumo wa kijamaa au kibepari ni kuwa na vyombo visivyofanya kazi.
Na pale vyombo hivyo vilipofanya kazi vilifanya kazi hiyo kwa ajili ya waliokabidhiwa vyombo kujitajirisha wao wenyewe na familia zao; kuwatajirisha wageni; lakini sio kutajirisha nchi na watu wake.
Kampuni au shirika liwe katika mfumo wa ujamaa au ubepari kama likiendeshwa kwa namna ya mwenye mali kujinufaisha yeye mwenyewe bila kunufaisha wateja/Wananchi bado tatizo linakuwa palepale.
Sio chombo kinachozalisha ili nchi itajirike bali kinazalisha kumtajirisha mtu mmoja au wachache potelea mbali kama nchi inapoteza kitu fulani kwa kufanya hivyo.
Mali inayozalishwa sio mali isiyohamishika. Na ili mradi wazalishaji wawe ni Wananchi au wawekezaji toka nje wanahamisha mali hiyo na haikai hapa nchini ni muhali kuona jinsi gani tunaweza kuondokana na umaskini.
Biashara hapa itakuwa ni sawa na ya mchumia-tumbo, yaani, kwa hapa mwekezaji mwenyewe ndiye anayefaidika lakini nchi haipati lolote isipokuwa statistiki za uongo na kweli kuwa wawekezaji wameongezeka na uzalishaji mali umeongezeka.
Swali linakuwa baada ya mali na faida hiyo kuzalishwa imebaki nchini au imekwenda nje?
Utajiri sio kile kinachozalishwa bali ni kile watu na nchi inachobaki nacho.
Utamaduni kama mizizi
Mti hustawi pale tu mizizi yake inaposhika ardhini. Uchumi wa nchi hauwezi kujengwa juu ya utamaduni au tabia za kigeni.
Matajiri wanaozuka katika mazingira na utamaduni wa aina hiyo ni sawa na maua yanayochipua jangwani.
Umaskini Afrika kwa kiasi fulani unachangiwa na nchi nyingi kushindwa kudumisha utamaduni wake na kuutumia kama chambo cha kuvuta utajiri wa aina mbalimbali.
Mathalani, Tanzania, nchi inayosemekana kama mama wa Kiswahili imeshindwa kabisa kutumia lugha yake hiyo inayothaminiwa na kila mmoja Afrika kujinufaisha.
Mila na desturi za makabila mbalimbali Tanzania leo imekuwa ni kitu cha kuonea aibu na sio fahari. Kwa mantiki hii mila na desturi hizo pia kwa kutoweka kwake kunachangia umaskini zaidi kwa nchi kukosa asili wala fasili.
Nchi nyingi za Kiafrika tofauti na Uchina au India zimeshindwa kutumia mitishamba yao kujinufaisha kwa sababu walioko katika sekta ya afya tayari wamenunuliwa na makampuni na wafanyabiashara wa madawa ya kizungu. Na wanaona bora kukubali dawa feki kuliko kuboresha dawa zetu asilia.
Michezo kama nyenzo ya utamaduni imara imeachwa kama yatima na matokeo yake leo Tanzania ni kichekesho karibu katika kila aina ya mchezo.
Tukumbuke wakati sisi ni kichekesho majirani zetu leo wanatajirika na kuneemeka kutokana na hiyo hiyo michezo.
Kwa hiyo utamaduni wa uongozi dhaifu unaotegemea fadhila na huruma ya wafanyabiashara umejenga nchi kujidhalilisha na kujiuza kwa bei rahisi kwa yeyote yule anayetaka kutukaanga kwa mafuta yetu wenyewe.
Kwa kukubali tamaduni za wengine kichwa-na-miguu tumejiweka mahala pabaya ambapo hatuna msingi wa kujengea mtaji, teknolojia na utajiri wetu wa asili.
Japan, China, Uarabuni, Korea Kusini, Malaysia tofauti na nchi za Marekani ya kusini kwa kutokubali utamaduni wao kuchafuliwa mno na wageni wamejenga aina ya uchumi ambao sio rahisi kushindwa kufanya kazi labda pale dunia nzima inapokuwa kwenye matatizo makubwa.
Hili ndilo linalotokea Afrika Kusini pia ambako Wazungu wa huko wamekubalina na Waafrika kuunda taifa lenye utamaduni tofauti na ule wa Magharibi au wa kuiga.
Na siri yao wote hawa ni kuwa Wananchi kwa viongozi wanakumbatia na kuenzi utamaduni wao. Hapa kwetu viongozi wetu kama Yuda Iskarioti wanaukana utamaduni wao.
Hivi sasa wamezuka manabii wa kisiasa na kadhalika wanaotaka ghafla bin vuu tuusahau utamaduni wetu na kukubali kukumbatia yale wazungu wanayotaka tuyakubali eti kwa faida yetu wenyewe.
Dawa ya umaskini wetu pamoja na mambo mengine ni kutafuta yote mazuri yaliyokuwepo katika utamaduni wetu na kuyarejesha upya kwa faida ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.
Tusipofanya hivyo kama wana Israel tutaendelea kutangatanga nyikani kwa miaka 4o kama sio zaidi. Wataalamu wanasema kwa uhakika ni miaka 166.
Utamaduni wa uzalishaji mali kwa njia bora zaidi na zenye ufanifu, ufanisi na tija zaidi bado ni mgeni kwa Waafrika.
Ukiangalia kwa undani, hata hivyo, utakuta tatizo sio kitu kingine ila elimu. Elimu inayotolewa hivi sasa ni ile isiyochangia moja kwa moja kwenye shughuli za kibiashara au uzalishaji mali.
Katika dunia hii ya ushindani na kama kweli tunataka kuusogeza nyuma umaskini hatuna muda wa kupoteza kusoma vitu visivyo na maana katika maisha yetu ya kila siku.
Hii ni dunia ya kusoma na kuelewa menejimenti, masuala ya fedha, uchumi, biashara, masoko, teknolojia, uzalishaji mali, uhasibu na staid na taaluma nyingine ambazo moja kwa moja zitachangia kuuondoa umaskini wa mtu binafsi na nchi kadhalika.
Masomo hayo yakifundishwa kwa lugha ya Kiswahili ndiyo itakuwa mteremko kabisa kuupunguza umaskini kwa asilimia kubwa tu.
Katika kufanikisha hili lazima tuwe na utawala bora kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa. Na uongozi bora kwangu mimi ni uongozi usioingia madarakani kwa nia ya kujitajirisha wao wenyewe bali kuwatajirisha Wananchi kwa ujumla wao. Tumeona wangapi waliojitajirisha wenyewe kama viongozi wamekuja na kuondoka lakini nchi wameiacha katika umaskini ule ule. Na wao wenyewe wala hawakwenda na utajiri huo wala kuacha sifa yoyote ya maana ya kusaidia watu wao kupambana na umaskini.
Pamoja na haya yote tukubali kuwa ubepari umeingia nchini, Afrika. Lakini je, tuufuate kama unavyoendeshwa huko Ulaya na Marekani. Au Waafrika wanaweza wakawa na mfumo wa kisiasa na kiuchumi unaoitwa ubepari-wa-kijamaa?
Mfumo unaotoa fursa sawa kwa wote kujitajirisha lakini wakati huo huo unawalinda watu wetu wasiadhirike kama wazungu maskini wanavyoadhirika huko kwao?
Hatima ya umaskini Afrika kamwe haiwezi kuamuliwa kwa misaada au ushauri wa wageni. Hatima yetu itaamuliwa na siasa zetu wenyewe humu ndani, siasa zitakazokataa ubinafsi, ubadhirifu na ulafi ili wote tuweze kuwa na maisha bora.
Sunday, February 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment