Wednesday, November 2, 2011

Aljazeera tishio kwa nchi za Magharibi na Afrika

MAREKANI na Ulaya zimekuwa sio tu zikisambaratisha nchi zinazoendelea kwa kutumia vyombo vyao vya habari vyenye uwezo na nguvu za kutisha lakini pia wakati mwingine zimekuwa zikipandikiza redio, magazeti na vyombo vingine vya habari vya jana na leo ili kusambaratisha nchi ambazo zinapuuza maslahi yao na zinazokataa kuwa chini yao.


Hivi leo Marekani na Ulaya zinagaragazwa na Televisheni ya Aljazeera ambayo baada ya muda sio mrefu inafuatiwa pia na Radio Aljazeera tena kwa lugha za Kizungu.

Ni kwanini Aljazeera inakuwa tishio? Inakuwa tishio kwa sababu ya kukataa kutangaza uongo na kufichua ukweli bila kumuonea au kumpendelea mtu au kundi fulani la watu mahala popote pale duniani. Hivi ndivyo uandishi wa habari unavyotakiwa tofauti na tunavyoona jinsi CNN, MSNNBC, Fox, Sky, CBS na wengineo wanavyotumika kwa ajili ya kuficha ukweli juu yao na kuangaza na kuanika uongo juu ya wengine hata isipolazimu kufanya hivyo ili tu wazungu waonekane watu wa maana na sisi wengine tusio na maana.

Hivi sasa kuna maandamano katika nchi kadhaa ulimwenguni ikiwemo Marekani kwenyewe ambako watu wanaukataa mfumo wa uchumi wa kiwizi wa kibepari unaoruhusu asilimia 1 tu ya Wamarekni kula zaidi ya asilimia 90 ya kile kinachozalishwa Marekani na duniani kwa ujumla.

Mfumo huu si mwingine ila ni ule ambao kwao watu wachache pengine maelfu tu na wala sio laki wanadhibiti fedha, mitaji, uchumi, biashara, huduma na uwekezaji duniani. Watu hawa wachache wanaweka tena asilimia kama 10-15 ya watu toka sehemu mbalimbali duniani kudanganya asilimia 85 au zaidi ya watu wao kwa ajira zisizo na tija, mikopo isiyolipika na ufahari usiodumu.

Hali iliyofikiwa na mfumo wa namna hii ndio ile hali Karl Marx alioyoiita ' demokrasia ya kibepari inapotumika ili kukomba fedha zote zilizoko kwenye hazina ya serikali na kisha kuziweka fedha mifukoni mwa wanasiasa na matajiri wachache wanaoishi kwa kutapeli, kulangua, riba, rushwa na ufisadi wa kila namna.' Akatahadharisha demokrasia kama hii si mfumo unaoweza kumfaa binadamu wa jana,leo wala kesho. Utasambaratisha taifa na watu wake hatima ya yote!

Hakuna kitu kibaya duniani kama nchi moja kukubali kuolewa na nchi nyingine kama baadhi ya nchi za Kiafrika zinavyofanya katika mahusiano yake na Marekani, Uingereza, Ufaransa, Uchina, Italia, Urussi na wengineo kwa sababu mwanamme kama taifa bado ni mwanamme asiyetosheka na ambaye hukudharau ukishamtegemea kwa kila kitu.

Aidha, mataifa makubwa duniani yamefanikiwa si haba kwa kuwafanya wananchi wake wajinga, mbumbumbu na wasiojua chochote kinachoendelea katika dunia hii. Na ndio maana wengi wao wamejikuta wako hadharani wakiwa na chupi zilizofika kwenye magoti kiuchumi na kijamii! Aibu yao inazua sio tu wasiwasi bali pia hasira na kutaka kuleta mabadiliko yatakayowafanya waondokane na ujinga na udhalilishwaji wao na mabwana au watawala wao.

Hii ina maana kwamba ukoloni haujawahi kwisha na hautawahi kwisha duniani. Ile asilimia moja niliyoizungumza inaifanya dunia yote koloni lake. Asilimia 10-15 chini yao wanagawana vipande vipande vya dunia. Na katika hawa kuna wakuu wa idara za serikali, matajiri na watawala wa kuzaliwa wenye utajiri wa kurithishwa-kwa maneno mengine wenye mtaji ndio wakoloni wapya katika dunia yetu.

Ndio maana katika kila nchi ya Kiafrika ni sawa ukihesabu kuwa rais na mawaziri wake wote wanatawaliwa na mfadhili au huyo anyejiita mkoloni wa zamani. Si watu huru hasa katika nchi zetu nyingi za Kiafrika. Hawana hiari ya hiki au kile, na hata kuwepo kwao madarakani kunategemea ni nani hao wakubwa wanaomtaka. Kumbuka Kabila wa Kongo, Sankara wa Bourkina Fasso na Machel wa Mozambique.

Hivi sasa katika kutapatapa na kuona mashamba ya bibi ya dunia yanatoweka na Mchina, Mbrazili, Mrussi na Mhindi wanakuja kwa kasi kubwa kujitafutia na wao riziki halali miongoni mwa Waafrika nchi za Magharibi zimeanza kutaharuki na kuanza kuwa za mwanzo kwenda kinyume na maadili ya demokrasia.

Marekani hivi sasa inazuia matangazo ya Aljazeera yasisikilizwe na wananchi wake; Ulaya inataka kuifosi Ugiriki ikubali kuwatunuku wananchi wake ugumu wa maisha usiosthaimilika ili Ugiriki ipate mikopo; Uingereza inataka kuilazimisha Afrika kukubali usenge na ushoga ili nchi za Kiafrika ndiio zifikiriwe kwa mikopo. Hakuna mantiki hata kidogo.

Wanachosahau jamaa hawa ni kwamba, huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote. Aljazeera kwa ujasiri na ubinadamu imeamua kufanya kazi ya kuwazindua wanyonge duniani bila kujali wako kwenye mataifa tajiri au maskini. Na kwa sababu hiyo ile asilimia 1 ya juu kabisa ya mabepari duniani na vibaraka wao katika kila nchi kwa kila hali ni lazima wawe maadui wa Aljazeera.

Hata hivyo zama za ukweli zikishafika ni upumbavu kujifukia kichwa chini kwenye mchanga kama mbuni kwa kudhani kuwa wewe usipoonekana macho au wewe usipoona wengine basi hauonekani kabisa.

Afrika kwa miaka zaidi ya 50 imetenda dhuluma kubwa kwa wazee, wanawake, vijana, wanavijiji, wakulima, wafanyakazi, wanafunzi na watoto wake. Huu ni muda mwafaka wa kuondokana na vyombo vya habari vya kudanganya na kuzaini kwani Aljazeera ikishaanza kutangaza kwa lugha za Kiafrika kwa televisheni na redio zake tutajikuta matatani na wananchi wetu.

Wale wanaopiga danadana na kuruhusu wananchi kuandika katiba mpya, wanaochezea demokrasia, wanoruhusu ufisadi na rushwa, wanaoruhusu maliasili za nchi kuchotwa sawa na bure na wanaoamua kutowathamini watu wao na kuthamini zaidi watu kutoka nje wanapaswa kukoma mara moja na kuutazama mustakabli mpya kwa nia njema ya kujinusuru wao wenyewe, mataifa yao na vizazi vyao. Na wakati ni huu, hakuna kabisa muda wa kupoteza, kusubiri au kungoja ngoja. Chelewa, chelewa, utamkuta Aljazeera keshaingia ndani na mwana tena si wako!

No comments:

Post a Comment